MAONI: Tujizuie kuparamia 2026 na siasa za uchaguzi, tusubiri hadi 2027
KUNA dalili kuwa mwaka wa 2026 huenda ukatawaliwa na mjadala wa mapema wa siasa za 2027, jambo linalozua wasiwasi mkubwa kwa mustakabali wa maendeleo ya nchi yetu.
Badala ya kuutumia mwaka huu kufanya kazi, kutathmini sera na kutatua changamoto zilizopo, kuna dalili kwamba nguvu zitaelekezwa kwa kampeni za mapema, makundi ya ushawishi na mipango ya uchaguzi ujao.
Hali hii itaathiri moja kwa moja utekelezaji wa masuala muhimu ya kitaifa.
Elimu bado inahitaji kuboreshwa pakubwa katika miundombinu, ufundishaji na upatikanaji wa rasilmali.
Sekta ya afya nayo inahitaji uwekezaji endelevu ili kuboresha huduma kwa wananchi wote.
Ajira kwa vijana, ambao ndio kundi kubwa zaidi la jamii, bado ni changamoto inayohitaji sera thabiti na utekelezaji makini.
Haya yote yanahitaji umakini wa dhati, si kuvurugwa na kampeni za mapema za siasa.
Kuzama mapema katika siasa za 2027 kutasababisha viongozi wengi kuanza kufanya maamuzi kwa kuzingatia mvuto wa kisiasa badala ya maslahi ya muda mrefu ya taifa.
Bajeti, miradi ya maendeleo na hata uteuzi wa wakuu wa taasisi utaweza kuathiriwa na hesabu za kisiasa. Matokeo yake ni kupungua kwa uwajibikaji na ufanisi katika utawala.
Aidha, wananchi wanapovutwa mapema katika mijadala ya kisiasa, umoja wa kitaifa unaweza kudhoofika.
Badala ya kujadili suluhisho la matatizo, jamii hugawanyika kwa misingi ya vyama na wanasiasa binafsi. Hii ni hatari kwa taifa linalohitaji umoja ili kusonga mbele.
Mwaka wa 2026 unapaswa kuwa mwaka wa kuweka msingi imara wa maendeleo.
Tukiruhusu siasa za 2027 zitawale mapema, tutakuwa tumesahau masuala muhimu yanayogusa maisha ya wananchi na kuchelewesha maendeleo ya nchi yetu.