• Nairobi
  • Last Updated May 15th, 2024 6:53 PM
MAONI: Uhuru anafaa aache mafumbo, azungumze waziwazi anachomaanisha

MAONI: Uhuru anafaa aache mafumbo, azungumze waziwazi anachomaanisha

 Na LEONARD ONYANGO

MARAIS wastaafu nchini Kenya – Daniel arap Moi, Mwai Kibaki na Uhuru Kenyatta – wamekuwa wakionyesha tabia tofauti katika kuzungumzia masuala muhimu ya nchi.

Moi alipong’atuka mamlakani mnamo 2002 baada ya kuongoza Kenya kwa miaka 24, alionekana jasiri licha ya kuwepo kwa vitisho kutoka kwa wanasiasa wa muungano tawala, National Rainbow Coalition (Narc) kwamba wangemchunguza na hata kumshtaki iwapo angepatikana na hatia.

Lakini Moi hakusita kuzungumzia masuala ya kitaifa kila alipohisi kwamba mambo yalienda kombo.

Wakati wa kampeni za kupigania Katiba ya 2010, Moi alikuwa miongoni mwa viongozi wa kisiasa waliopinga rasimu ya katiba.

Mzee Moi alishikilia kuwa japo alipinga rasimu ya katiba, sababu zake zilikuwa tofauti na zile za mbunge wa Eldoret Kaskazini William Ruto (Rais wa sasa) ambaye pia alipinga rasimu hiyo akidai kuwa ingesababisha Wakenya kupokonywa ardhi zao.

Moi hakuchelea kwenda makanisani kote nchini na kutoa maoni yake kuhusu masuala muhimu ya nchi.

Mwai  Kibaki alipostaafu 2013, aliamua kunyamaza kimya. Hata ilikuwa vigumu kwa Wakenya kuelewa ikiwa aliunga mkono Uhuru Kenyatta katika uchaguzi mkuu wa 2013 ambapo alikuwa akimenyana na kiongozi wa ODM Raila Odinga. Ilikuwa nadra kwa Kibaki kuonekana hadharani hadi alipoaga dunia 2022.

Uhuru Kenyatta alipoondoka mamlakani 2022, alianza kwa kunyamaza sawa na Kibaki lakini alilazimika kujitokeza na kutangaza kuwa hajaondoka kwenye ulingo wa siasa, serikali ilipotishia kumpokonya chama chake cha Jubilee.

Hata wahuni wa walipovamia shamba la familia yake la Northlands katika eneo la Ruiru, Kaunti ya Kiambu, Kenyatta alisalia kimya.

Hivi karibuni, Rais Mstaafu amekuwa akijitokeza na kuongea kwa mafumbo ambayo yamekuwa vigumu kutegua.

Alipokuwa kwenye hafla ya mazishi katika eneobunge la Kipipiri, Kaunti ya Nyandarua miezi mitatu iliyopita, Uhuru alizua gumzo aliposema kwamba alihisi kulia anapoona jinsi mambo yanaendeshwa.

Uhuru pia alisema kuwa viongozi wa Kenya kwanza huenda wakaingiza nchi kwenye mtaro kutokana na tabia yao ya kufuatilia mambo ya zamani badala ya ‘kuangalia mbele’.

Uhuru, hata hivyo, hakufichua ni mambo gani ya zamani ambayo serikali ya Kenya Kwanza inafuatilia.

Wiki kadhaa zilizopita, Uhuru alipokuwa akizungumza wakati wa kutawaza maaskofu wawili wa Kanisa Katoliki jijini Nairobi,  alisema kuwa siasa imesheheni wasaliti lakini hakuwataja – hali iliyoacha Wakenya wakikuna vichwa kujaribu kubaini wasaliti hao.

Viongozi wa Kenya Kwanza walikuwa wameapa kuanzisha uchunguzi dhidi ya Kenyatta pamoja na mawaziri wake – huenda hii ndiyo sababu ya Rais Mstaafu kukwepa kuzungumza wazi bila kutumia mafumbo.

Uhuru anafaa kujua kwamba hata Mzee Moi alitishiwa vivyo hivyo lakini hakuogopa kutoa maoni yake kuhusu masuala muhimu ya kitaifa.

 

  • Tags

You can share this post!

Matumaini kwa raia maskini EU ikitoa Sh800m kuwasaidia...

Idadi ya waliofariki katika mkasa wa bwawa Maai-Mahiu...

T L