Maoni

MAONI: Uhuru hawezi kuaminika katika ushauri wake kwa chipukizi wa Gen Z

Na KINYUA KING'ORI January 22nd, 2025 Kusoma ni dakika: 1

HIVI majuzi, Rais (mstaafu) Uhuru Kenyatta aliwarai vijana wa Gen Z kupigania haki zao na kupinga aina zote za dhuluma dhidi yao.

Akizungumza Katika ibada ya mazishi ya binamuye, Kibathi Muigai kijijini Ichaweri, eneo Bunge la Gatundu Kusini, Kiambu, alitumia jukwaa hilo kuhamasisha vijana wa Gen Z kuhusu umuhimu wa kujitokeza na kupigania kwa ujasiri haki zao wanazonyimwa na serikali au viongozi waliowachagua bila kuogopa vitisho.

SOMA PIA: MAONI: Orengo, Sifuna wataitwa maajenti wa Gachagua wakiendelea na ukosoaji

Japo ni haki ya Uhuru Kenyatta au kiongozi yeyote mwingine kuzungumzia masuala ibuka nchini, inasikitisha kuwa baadhi ya viongozi wa kisiasa wamesuka mbinu ya kutumia vijana wa Gen Z kutimiza malengo yao ya kisiasa.

Kwanza tujiulize, tangu Uhuru astaafu na Gen Z wajitokeze kuandamana ambapo baadhi yao walijeruhiwa na hata kuuawa, alijitokeza kuwatetea kuhakikisha waathiriwa wamepata haki yao?

Je, kuna ithibati gani kuwa atawaunga mkono vijana wakikumbatia ushauri wake?

Rais Uhuru Kenyatta na baadhi ya viongozi ndio wanafaa kulaumiwa kwa kuwa vizingiti na kutatiza juhudi za vijana kukabiliana na serikali.

Wamehujumu harakati za kuhakikisha inatimiza ahadi zake kwa Wakenya na kukomesha utawala mbaya wenye kiburi na ufidhuli.

Hivyo, Uhuru Kenyatta hakusema ukweli kutoka moyoni mwake alipohimiza vijana kujitokeza kupigania haki.

SOMA PIA: Maoni: Raila anakejeli Wakenya kwa kukosoa utekaji nyara wa vijana

Rais huyo mstaafu kwanza angefafanua kwa nini ameruhusu wanasiasa wanaominika kuwa wandani wake kuteuliwa mawaziri katika serikali anayoshauri vijana waipinge kwa kuandamana.

Kiongozi anayeshukiwa kusaidia utawala unaoendeleza utekaji nyara kwa vijana wetu hafai kuaminika kwa sababu anataka kuwatumia vijana wenye nia njema na anafaa kuitwa msaliti.