MAONI: Ukabila ndio unatuzuia kusema mtu jasiri kama Sifuna anatosha kuwa rais
NADHANI mara kwa mara Mwenyezi Mungu huweka mbele yetu, Wakenya, kioo kinachoonyesha picha za viongozi bora wa kutufaa, tukakiangalia kwa makini na, kutokana na imani yetu duni, tukaanza kukigeuzageuza ili kuangalia hapo nyuma pana nini.
Kisha, kwa kutoamini kwetu, baadaye anachoka nasi na kukiondoa kioo hicho ghafla, nasi tukabaki hapo tukitumbua macho angani na kuduwaa, fursa ikatupita hivyo, tukaishia kulalamika kuwa hatuna bahati ya kupata viongozi wema.
Tumetokea kuigawa nchi yetu kwa misingi ya maeneo na makabila hivi kwamba, kila kiongozi anayejitokeza, kwanza kabisa huonekana kwa darubini ya ukabila hata kabla ya kuwekwa kwenye mizani ya kipaji cha uongozi bora.
Katika tawala zote tano tangu Kenya iwe huru, mifano ipo tele ya viongozi walioonyesha dalili za kutuelekeza tulikopaswa kwenda, lakini upumbavu uitwao ukabila umetulemaza na kutuzalia viongozi ambao kila mtu anajua hawafai.
Kila wakati hatukosi fursa ya kubadilisha uongozi kutoka kizazi kizee hadi kichanga na bora, ila tatizo hilo hutulemea, ikawa mabadiliko si muhimu, mradi ‘mtu wetu’ anaongoza au yuko kwenye meza inakonyofolewa nchi kama minofu.
Leo ukithubutu kusema kuwa Seneta Edwin Sifuna wa Nairobi, mja mwerevu na jasiri kupindukia, anatosha kuongoza nchi au angaa kuwa naibu rais, utatukanwa na kukumbushwa kwamba Nairobi amevamia juzi tu, jogoo wa shamba hawiki mjini.
Jasiria kupendekeza kwamba Bw Sifuna akiungana na Mbunge wa Embakasi Mashariki, Bw Paul Ongili (Babu Owino) kisha wachaguliwe rais na naibu wake, yeyote kati yao anaweza kushika nafasi yoyote kati ya hizo mbili kuu nchini, utatukanwa matusi ya kukuumbua kabisa.
Utakumbushwa kwa ukali na bezo kwamba, awili hao ni watu wa magharibi mwa nchi, kwa kuwa kila anayetokea mbele ya mjini Nakuru anachukuliwa kuwa mtu wa magharibi, eti kwa msingi huo pekee hawawezi kutuongoza.
Utadhani si Wakenya.
Hata afadhali mtu akunyamazishe kwa kutilia shaka tajiriba zao – ingawa hata hilo si tatizo mradi taasisi zilizoundwa na Katiba zinawezeshwa kufanya kazi itakiwavyo – badala ya kuangalia walizaliwa wapi ndani ya mipaka ya Kenya.
Swali la kwanza? Iweje tuwaachie Wakamba wawili nchi nzima? Kwani mama zetu hawakuzaa viongozi?
Mashariki mwa nchi walisema Prof Kibwana hapatani kisiasa na kigogo wao, Bw Kalonzo Musyoka, naye Bw Mutula angali mtoto, bado ubwabwa haujamtoka shingoni.
Ukiangalia mifano yote hiyo utatambua kuwa Wakenya tumejichongea wenyewe muda huu wote, kwa hivyo hatuna idhini ya kulalamika kuhusu utawala mbaya kamwe, hasa enzi hii ambapo
mutua_muema@yahoo.com