Maoni

MAONI: Upinzani wasitie baridi, bado wana nafasi nzuri kutua Ikulu

Na PAUL NABISWA October 8th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

HATUA ya aliyekuwa Waziri wa Usalama wa Ndani, Dkt Fred Matiang’i kuhudhuria mkutano mkuu wa wajumbe wa Jubilee imezua mgawanyiko mkubwa katika upinzani.

Matiang’i aliaminika kuwa mmoja wa wale wangekabiliana na Ruto katika uchaguzi mkuu wa 2022 lakini sasa, baadhi wamemtaja kuwa msaliti.

Wenzake wanaona kuwa angekuza chama chake ambacho si Jubilee. Baadhi wameanza kumwita msaliti. Siasa zina mambo.

Mtazamo wa siasa za wakati huu unakaribiana kwa kiasi kikubwa na juhudi za upinzani kutaka kujenga upinzani mkubwa wa kuing’oa serikali iliyo madarakani.

Haijawa kazi rahisi tangu zamani kuwaunganisha viongozi wa upinzani na ndio sababu Rais Moi alishinda katika uchaguzi wa 1992 na 1997.

Ila hili lilitokea pia kabla ya uchaguzi mkuu wa 2002 utata pia ulikuwepo lakini upinzani ukaungana na kuiondoa KANU madarakani.

Katika muungano wa NAK wa Mwai Kibaki, Wamalwa Kijana na Charity Ngilu kila mmoja alikuwa kasema kuwa angegombea Urais.

Muungano huo ulikuwa thabiti na ukaanza kufanya kazi na Profesa Kivutha Kibwana.

Ila baada ya siku chache Profesa Kivutha akauhama na kuelekea katika muungano wa Simeon Nyachae na Safina.

Katika kipindi hicho tu aliyekuwa mbunge wa Gem Joe Donde akasema kuwa ni yeye alitaka kuwa mpeperushaji bendera wa NAK.

Ilimchukua mshirikishi wa kundi hilo Dkt Willy Mutunga stahamala kubwa kumwonya Donde kuhusu misimamo yake ya wakati huo.

Kazi ilikuwa mbele licha ya kuwa katika kundi hilo walikuwa wamekubaliana Kibaki angekuwa mgombea urais halafu Wamalwa awe makamu wake.

Agosti 2002 wabunge waliokasirishwa na hatua ya Rais Moi kumwidhinisha Uhuru Kenyatta kugombea Urais walihama na kuungana na kina Wamalwa wakabuni muungano wa NARC kwa pamoja.

Katika kipindi hicho, upinzani ulikuwa na nia ya kuiondoa KANU kwa vyovyote vile. Kwanza aliyekuwa mbunge wa Kiambu ambaye alikuwa mfadhili mkubwa wa chama cha DP cha Mwai Kibaki alihama upinzani na kujiunga na KANU.

Lilikuwa pigo kubwa mno kwa upinzani lakini wakasema lengo lao lilikuwa ni kuwa wenyeji wa ikulu baada ya uchaguzi mkuu wa mwaka huo.

Hilo halikuwa kuu zaidi. Nyachae na Orengo walikuwa katika muungano huo wa NARC.

Mambo yaliharibika wakati Raila Odinga katika bustani ya uhuru aliposema Kibaki tosha. Nyachae alikuwa na ufuasi kiasi cha haja alihama na kugombea Urais.

James Orengo naye aligombea Urais pia na SDP. Kibaki bado alishinda. Gachagua na wengine wanatakiwa kuwa na subira kutokana na matukio hayo. Wataondokewa na baadhi ila muhimu ni dhamira.

Paul Nabiswa ni mhariri, NTV