MAONI: Ushirikiano wa ‘dynasties’ uwe funzo kwa walalahoi
KAMPENI za uchaguzi wa mwaka wa 2022, ziliongozwa na kauli-mbiu mbalimbali za vyama vya kisiasa.
Chama cha UDA ambacho kilijiunga na vyama vingine kuunda muungano wa Kenya Kwanza kilipigia debe uongozi ambao ulilenga kumpa nafasi mwananchi mwenye mapato ya chini zaidi.
Hivyo basi kauli ya ‘hasla’ ilichangamkiwa na wananchi wengi wenye changamoto katika kujiendeleza kiuchumi. Baadhi ya wananchi walilinganisha maisha yao na maisha ya wagombeaji wa viti kwa tiketi ya chama cha UDA.
Hivyo ndivyo waliojiita walalahoi ama ukipenda ‘hasla’ walivyozinasa fikira za wananchi waliojitambua kuwa katika tabaka hilo.
Miaka mitatu tangu Kenya Kwanza kupata uongozi, miungano sasa imekuwa ya watu wenye ushawishi mkubwa katika historia ya siasa nchini Kenya.
Viongozi waliosutwa kwa kuwa mabwanyenye wasiofaa kupata uongozi kwa sababu ya kukosa kuzifahamu shida za walalahoi sasa wamejumuishwa katika jopo la kufanya maamuzi ya nchi.
Kwa mujibu wa Rais alipokuwa akimkaribisha kinara wa chama cha KANU, Gideon Moi, kuwepo kwake pamoja na Raila Odinga na Uhuru Kenyatta ndiko kutaiwezesha Kenya kujikwamua katika orodha ya nchi zinazoendelea na kuwa kati ya mataifa yaliyostawi.
Lakini iweje hivyo ilihali aliwapinga katika kampeni zake na kuwataja kuwa wanasiasa matajiri wasioweza kujali maslahi ya wasiojiweza? Je, hili ni thibitisho kuwa uongozi wa kisiasa nchini umetekwa na familia za waanzilishi wa taifa hili?
Ni kana kwamba ni muhali mwanasiasa yeyote yule kuongoza bila kuwepo kwa familia ya Kenyatta, Odinga na Moi. Ni bayana kuwa uongozi wa kisiasa nchini Kenya umejengwa kwenye msingi wa kihistoria wa familia hizi tajika.
Kwa nini Rais afanye ukuruba na familia ya Moi, Odinga na Kenyatta ili Kenya iendelee?
Hivi ni kusema hakuna kiongozi anayeweza kuongoza Kenya kwa amani iwapo atakosa kufanya mkataba na viongozi kutoka familia hizo za kifalme?
Muungano wa viongozi hawa ni funzo kwa Wakenya wenye mazoea ya kuwachukia wenzao kwa sababu ya mirengo ya siasa wanaoufuata. Ni wazi kuwa wanasiasa huwa hawana uhasama baina yao hata kidogo.
Cheche za maneno wanazorushiana wakati wa kampeni huwa ni njia ya kila mmoja wao kujipigia debe. Wakishaondoka kwenye jukwaa la hotuba za siasa wao ni ndugu wa toka nitoke. Wanafaana kwa hali na mali.
Siasa kwao ni mchezo wa kutathmini ni kiwango kipi cha mgao wa rasilimali kila mmoja wao atakipata. Hawafikirii kuhusu dhiki za wananchi hata kidogo.
Tunapokaribia kampeni za uchaguzi wa mwaka wa 2027, Wakenya wanafaa wajifunze kwa kuiga mfano wa viongozi hawa wa siasa. Wafahamu kuwa hakuna haja ya kumchukia mwenzako.
Siasa ni mchezo wa kuwasisimua wananchi na kuwapa hisia kuwa kila mgombea ni bora kuliko mwingine.
Kuwa kila mwanasiasa anawajali na maisha yao yataboreka iwapo watamchagua. Ukweli ni kuwa, sera ya kwanza wanayozingatia ni ile inayoboresha maisha yao wenyewe.
Kampeni za 2027, ziwe za amani. Walalahoi watambue kuwa wao ndio ‘hasla’ wanasiasa wasiwatumie kama kitega uchumi kujijengea nafsi zao. Fujo izikwe katika kaburi la sahau.