Maoni

MAONI: Utulivu ndani ya chama cha ODM utachukua muda

Na PAUL NABISWA January 8th, 2026 Kusoma ni dakika: 2

INAVYOONEKANA wakati huu, ODM ilikuwa Raila Odinga na Raila Odinga alikuwa baba halisi wa chama hicho, kwanza kabla ya kuwa wa ‘watu wa Kenya’.

Mawimbi katika ODM yanatishia kuizamisha ngalawa ya chama hicho kabla ya uchaguzi mkuu wa mwaka wa 2027.

Mgawanyiko ni dhahiri kuhusu nafasi ya ODM baada ya kipindi cha kwanza cha Rais Ruto kukamilika.

Rais Ruto amewashawishi wahafidhina wa chama kama mwenyekiti Gladys Wanga na kiongozi wa chama Oburu Oginga kubuni muungano utakaoshinda mkusanyiko wa upinzani tarumbeta ya 2027 itakapolia.

Kwa upande mwingine katibu mkuu wa chama Edwin Sifuna anavuta jugwe hilo kwa njia tofauti.

Amesema hakuna mkataba wowote unaosema chaguo lao ni Ruto.

Yeye yuasema Rais Ruto ni “wantam”. Sijui kama ana uwezo wa kutekeleza hilo. Vurugu mechi katika chama cha ODM wakati huu inatisha wanachama na wasiokuwemo.

Ni mapambano halisi kabisa. Maeneo ya misiba yamegeuka kuwa majukwaa ya kupimana ubabe.

Za “ndani” kama wanavyosema vijana wa mosi hizi zinawekwa hadharani.

Tumeanza kuambiwa Rais Mstaafu Uhuru Kenyatta ana mtaji wa Sh2 bilioni kununua chama cha ODM. Kiongozi wa Wachache bungeni Junet Mohamed ametoa madai hayo bila kupepesa jicho.

Kuongezea uzito kwa hilo Gavana Gladys Wanga amemtaka Uhuru Kenyatta kujitenga na ODM kama jini. Amesema anaharibu chama.

Uhuru katika mazishi ya mbunge wa zamani Cyrus Jirongo bila kusema moja kwa moja aliwataja Wanga na washirika kuwa watu wanaojipendekeza ili wafikie malengo yao.

Alisema waache kuongea mambo ya “ujinga”.

Katika uzi huo huo, katibu mkuu wa ODM Edwin Sifuna alimwomba radhi Uhuru Kenyatta kutokana na matamshi ya Junet.

Sifuna yuasema wenzake katika chama walitafuna fedha za uhuru kama mchwa katika uchaguzi mkuu wa 2022 akiwataka Wakenya kumpa ridhaa ya kuwaongoza.

Sifuna ameibuka kwa meno ya juu na kutaja kuwa mfaidi mkuu wa hela za Uhuru Kenyatta alikuwa Junet Mohamed.

Eti Junet alitoweka kama duma na fedha za mawakala waliotakiwa kuwa jicho la Raila debeni.

Akaiona ikulu kwa paa. Ledama ole Kina amemtaka Sifuna kupunguza kiherehere.

Naibu mwenyekiti wa chama, Otiende Amollo na Millie Odhiambo ‘bird girl’ wamekuja na busara ya kiitikadi, wanataka maagano ya dharura katika Chungwa kufuata taathira aliyoiacha Baba.

Wanasema kasi ya kutaka kumtimua Sifuna kuwa katibu mkuu wa chama ni njia hatari kuliko inayoenda jehanamu.

Wamewataka wenzao kutuliza boli.

Pengine uwanja bado mdogo, ukubwa unaoonekana kuwa mjo wa baadaye.

Kimeumana wanavyosema Wakenya na pamechimbika kwa ndugu Watanzania.

Paul Nabiswa ni mhariri, NTV