MAONI: Viongozi wanawake watafaulu kuwa mfano bora kwa wasichana wetu?
WAKATI mwingine inakuwa vigumu sana kuwatetea viongozi wa kike na uongozi wa wanawake kwa jumla nchini.
Katika taifa ambamo uongozi wa wanawake unakabiliwa na vizuizi tele kutokana na taasubi ya kiume iliyokita mizizi na itikadi kali za kitamaduni, ungedhani wanawake wanaotwikwa nyadhifa za uongozi, wangetekeleza majukumu yao ipasavyo.
Badala yake, katika siku za majuzi, Wakenya wamekerwa matamshi ya soni kutoka kwa viongozi na wanasiasa mashuhuri wanawake wanaotegemewa na maelfu ya wasichana nchini kama kielelezo bora.
Ukweli ni kwamba, uongozi wa wanawake bado haujakubalika kikamilifu nchini na duniani kwa jumla.
Ndiposa wanawake viongozi wanahitajika kujituma na kumakinika maradufu zaidi ya wenzao wa kiume ili kuondoa shaka yoyote kuhusu uongozi wa wanawake na kuwafungulia milango zaidi wasichana na wanawake wengine katika jamii.
Japo siasa ni mchezo mchafu, kiongozi mwanamke anayejithamini na anayefahamu fika jukumu alilotwikwa, atajizuia kutoa matamshi kiholela yanayoweza kuwa na athari hasi kwa mtazamo wa wanajamii kuhusu viongozi wanawake.
Hata hivyo, tunayoshuhudia sasa ni kinyume kabisa na matarajio hasa wakati huu joto la kisiasa linazidi kupanda.
Viongozi maarufu wanawake waliotunukiwa fursa ya kushiriki maamuzi muhimu wanaropokwa hadharani matamshi ya soni yanayodunisha uongozi wa wanawake na kutweza jinsia ya kike.
Kenya inaandamwa na jinamizi la mauaji, dhuluma za kijinsia na kingono, ambalo limepenyeza hata katika shule maarufu za kitaifa.
Ingetarajiwa wabunge wanawake wangekuwa mstari wa mbele kushinikiza mageuzi muhimu kisheria na kuwasilisha miswada anuai ili kuwalinda wanawake kutokana na maovu hayo.
Badala yake, viongozi wanawake wenye usemi katika jamii wameungana na wenzao wanaume kuendeleza kasumba inayowasawiri wanawake na wasichana kuwa vinyago na vifaa vya ngono, kiasi cha kukubali kutumika kama mifano mchana peupe.
Mapema wiki hii vilevile, korti ilimpiga faini ya Sh10 milioni seneta mwanamke aliyepatikana na hatia ya kumchafulia jina karani wa seneti kwa madai ya kudhulumiwa kingono.
Korti ilieleza kuwa seneta hakuwasilisha ushahidi kuthibitisha madai yake aliyochapisha kupitia mitandao ya kijamii akikusudia kumhini mlalamishi.
Iwapo ni kweli seneta husika alidanyanya kuhusu kudhulumiwa kingono, basi ni pigo kuu kwa wahasiriwa wa dhuluma za kingono wanaosubiri haki.