Maoni

MAONI: Vitisho vya Malala kwa wanasiasa wa UDA ni hewa, hawezi kung’ata

June 3rd, 2024 Kusoma ni dakika: 2

Na CECIL ODONGO

KATIBU Mkuu wa Chama cha United Democratic Alliance (UDA), Cleophas Malala, hana mamlaka yoyote ya kuzomea wanasiasa wanaolumbana katika kambi ya Rais William Ruto na Naibu Rais Rigathi Gachagua mzozo unapoendelea kutokota chamani.

Wiki jana, mwanasiasa huyo aliwaandikia barua viongozi wanaolumbana ndani ya chama tawala, akiwaonya dhidi ya kuendeleza misukosuko na kutatiza uthabiti wake.

Kati ya wale ambao walilengwa ni wabunge Oscar Sudi (Kapseret), Gathoni wa Muchomba (Githunguri), mawaziri Kipchumba Murkomen (Uchukuzi) na Moses Kuria (Utumishi wa Umma) na Gavana wa Nyeri Mutahi Kahiga.

Mabw Sudi na Murkomen wamekuwa wakimshutumu Bw Gachagua kuhusu msimamo wake wa ugavi wa mapato kwa kuzingatia idadi ya watu.

Pia Naibu Rais amekuwa akiwashutumu viongozi wa Bonde la Ufa kwa kuingilia siasa za Mlima Kenya, jambo ambalo halijafurahisha watatu hao.

Kwa upande mwingine, Bi Wamuchomba anaunga mkono msimamo wa Bw Gachagua kuhusu ugavi wa mapato naye Bw Kahiga amekuwa mtetezi sugu wa Bw Gachagua, akisema hatakubali ahangaishwe serikalini.

Mwanzo, naunga kauli za wanasiasa hao kuwa onyo la Bw Malala ni kama upepo unaopita na hauna athari zozote kuhusu siasa zao au msimamo wao.

Bw Malala alinusuriwa tu na UDA na kuteuliwa kuwa katibu baada ya kuanguka vibaya katika kinyang’anyiro cha ugavana wa Kakamega dhidi ya limbukeni Fernandes Barasa wa ODM.

Licha ya kuhudumu kama seneta kati ya 2017-2022, katibu huyo alijipata hoi mbele ya Bw Barasa ambaye hakuwa amejaribu bahati yake kwenye ulingo wa siasa.

Je, mwanasiasa ambaye alilambishwa sakafu na limbukeni anapata wapi nguvu za kuwaonya wanasiasa veterani kama Mabw Sudi, Murkomen, Kuria na hata Gavana Kahiga ambaye anahudumu muhula wake wa pili?

Seneta huyo anastahili kukubali kuwa wadhifa aliopewa UDA ulitokana na hisani na mgawanyiko kati ya kambi ya rais na naibu wake unafanya kazi yake kuwa ngumu.

Yeye hujipata kwenye njiapanda, hajui afuate amri ya rais au naibu wake kwa sababu akiegemea mrengo mmoja, bado atatifua vumbi kali dhidi ya upande mwingine.

Kile ambacho Bw Malala anastahili kufanya ni kuachia rais na naibu wake watoe mwelekeo kuhusu masuala mazito chamani la sivyo, atajizolea maadui wengi.

Mrengo wa Bw Gachagua ndio utamkosesha usingizi zaidi kwa sababu si siri Bw Malala ni kibaraka wa kisiasa wa Rais na Kinara wa Mawaziri Musalia Mudavadi.

Upande wa naibu rais umekuwa ukishindana na mrengo Bw Mudavadi, ukidai anatumiwa kuwahujumu baada ya kupokezwa baadhi ya majukumu makubwa serikalini.

Badala ya kumakinikia kauli za kuwaonya wanasiasa UDA, Bw Malala anastahili amakinikie kujiimarisha ili arejee kwa kishindo Kakamega 2027, akilenga ugavana.

Katibu huyo anastahili kuzua ushirikiano na Gavana wa zamani Wycliffe Oparanya ambaye kwa sasa haonani uso kwa macho na Bw Barasa.

Ushirikiano huo utamsaidia kumwangusha gavana huyo 2027 na apate wadhifa huo ambao utamwondolea mzigo wa kuchunga ndimi za wanasiasa.

Hivi vita vya kukabana koo na wanasiasa wa UDA vitamponza kwa sababu anatumiwa na wakuu wa chama ambao mwishowe watamtema mawimbi ya kisiasa yakibadilika.