Maoni

MAONI: Wabunge waungane kutatua shida za raia walivyofanya kumtimua Gachagua

Na KINYUA KING'ORI October 23rd, 2024 Kusoma ni dakika: 1

MCHAKATO wa kumtimua afisini Naibu Rais Rigathi Gachagua ulitamatika majuzi baada ya Bunge la kitaifa kuidhinisha pendekezo la Rais Ruto kumteua Waziri wa Usalama wa Ndani Prof Kithure Kindiki kuwa Naibu Rais mpya.

Mimi si wakili kuthibitisha hapa ikiwa mchakato huo ulikuwa wa kisheria au kisiasa ila sote tuliounga au kupinga kutimuliwa kwa ‘mtu wa murima’ tunafaa kuamka sasa kuwajibisha wabunge wetu waliopuuza majukumu yao kwa muda mrefu ili kufaulisha njama za vinara wa vyama vyao vya kisiasa.

Naunga mkono kuondolewa kwa kiongozi yeyote anayetishia umoja na utangamano wa kitaifa.

Ni hatari kwa viongozi kupuuza mipango ya maendeleo na kushughulikia maslahi ya kisiasa tukizingatia changamoto nyingi zinazowakumba raia hasa udikiteta, ufisadi, maonevu ya kikabila katika uajiri na aina zingine za unyanyasaji serikalini.

Licha ya wabunge na maseneta kushiriki kumtoa Gachagua ofisini hakuna hata mmoja amejitolea kuhoji ufaafu wa Kindiki ambaye amelaumiwa kuhusiana na madai ya waandamaji kutekwa nyara na wengine kuuliwa wakati wa maandamano ya vijana wa Gen-Z.

Je, wabunge walishindwa kuhakikisha Rais anazingatia ufaafu wa mtu badala ya mikataba ya kisiasa ya 2022 na maslahi ya uchaguzi ujao?

Je, ilikuwa lazima mrithi wa Gachagua atoke eneo la mlima ikiwa kweli Rais haungi mkono kauli ya serikali kuwa kampuni ya hisa?

Ili kufaulu kuwajibikia wananchi, lazima wabunge wakubali kujitolea kama mashujaa wa uhuru waliopoteza uhai kuhakikisha taifa hili limepata uhuru na ukombozi kwa manufaa ya Wakenya wote bila kuzingatia ukabila, dini au rangi.