MAONI: Wajanja wa siasa watamtusi Rais ili wachaguliwe
WANASIASA wajanja wamegundua mbinu mpya ya kujipa umaarufu: kutafuta ugomvi na rais ili awaadhibu. Ataingia mtegoni na kuwafaa sana ikiwa atawaadhibu kwani atakuwa amewaongezea umaarufu wa kisiasa mashinani.
Usione ajabu watu wanaochukuliwa kuwa washirika wa karibu wa Rais William Ruto wakianza kupiga picha na maadui zake wa kisiasa na kuzipakia mtandaoni bila kuogopa kumkasirisha. Akiwafuta kazi kwa hasira wanaangua vicheko na kushangilia.
Usishangae ukiwaona wanaojiita marafiki zake, hasa wanaotoka eneo la Mlima Kenya, wakimgeuka na kuanza kumtukana hadharani. Ni sawa na mtu anayelengwalengwa na machozi, anasubiri tu mtu amzabe kibao ili yamtiririke kikweli!
Ni mbinu ambayo ilitumiwa na aliyekuwa Seneta wa Murang’a, Dkt Irungu Kang’ata, wakati wa utawala wa Rais Uhuru Kenyatta, akafaulu kuchaguliwa gavana wa jimbo hilo.
Dkt Kang’ata, wakati huo akiwa mnadhimu wa walio wengi katika Bunge la Seneti, alimwandikia Bw Kenyatta barua iliyokuwa kali mno kumwambia pasi na kificho kwamba mpango wa kubadilisha Katiba ya nchi, maarufu kama BBI, ulipingwa na wengi Mlimani.
Kwa hasira za mkizi, Bw Kenyatta alimvua Dkt Kang’ata wadhifa wa mnadhimu, wakazi wa Murang’a na eneo zima la Mlima Kenya wakashangilia na kumpenda zaidi Dkt Kang’ata.
Baadhi yao walianza kuuliza iwapo ingewezekana wakampa Dkt Kang’ata kura zao, akae nazo hadi uchaguzi utakapofanyika, zihesabiwe tu kwa nia ya kuthibitisha kwamba zote ni zake.
Bw Kang’ata naye alijanjaruka haraka na kujiunga na kundi la Dkt Ruto, naibu rais wa wakati huo, ambaye tayari alikuwa amekosana vibaya na mkubwa wake, Bw Kenyatta.
Kwa kitendo hicho cha ujasiri, Dkt Ruto alimpa Dkt Kang’ata jina la msimbo: Kang’ata wa Barua. Seneta wa watu alitamba nalo vilivyo, likageuka kaulimbiu bora zaidi ambayo ilimpeperusha hadi akawa gavana.
Mpaka sasa Dkt Kang’ata angali maarufu mno, na ni vugumu kutabiri ni nani anayeweza kumenyana naye katika uchaguzi ujao, lakini kuna kitu kimoja kinachoweza kutabirika: akisalia kwenye kambi ya Rais Ruto ataishia ‘ningalijua!’
Anatarajiwa kutafuta mbinu nyingine ya kijanja kama ile ya mwanzo ili akosane na Dkt Ruto, au aamke tu asubuhi moja na kutangaza, hata bila sababu yoyote, kwamba hatatetea wadhifa wake kwa tiketi ya muungano wa Kenya Kwanza (KK), na basi!
Hivi majuzi tu, Kamishna wa Tume ya Kitaifa ya Uwiano na Maridhiano (NCIC) Bi Wambui Nyutu alifutwa kazi kwa kile kilichoitwa tabia yake ya kuwa na ukuruba na wanasiasa fulani wa upinzani.
Ukweli wa mambo ni kwamba Bi Nyutu, wakili mchanga na machachari anayenuia kuwania ubunge wa Maragua, ameonekana mara kadha na naibu rais aliyetimuliwa, Bw Rigathi Gachagua, ambaye amegeuka kigogo wa siasa za Mlima Kenya.
Ukweli usiofichika kwa ni kwamba, yeyote anayenuia kuwa chochote kisiasa katika eneo hilo baada ya uchaguzi ujao, ni sharti ajitenge na Dkt Ruto. Hilo ndilo tarajio la kimsingi la wakazi, ambao ndio huamulia mkondo wa siasa.
Bila shaka wapo wanasiasa na watumishi wa serikali kutoka eneo hilo watakaoapa kufa na Dkt Ruto, lakini wanamhadaa tu ili wanufaike kifedha, hawana jinsi ya kumsaidia kisiasa, na wamefanya hesabu zao wakagundua hawawezi kuchaguliwa kamwe.
Kuna fununu kwamba mlimani patatokea kundi jingine la wanasiasa wasiofungamana na Bw Gachagua wala Dkt Ruto, na tayari wenyeji wameanza kunong’onezana kwamba hiyo ni mbinu ya Rais kugawanya mamilioni ya kura za eneo hilo.
Katika enzi hii ambapo Katiba inamtaka mshindi wa uchaguzi wa urais apate asilimia 50 ya kura za kuhesabika, na kura moja ya ziada, kugawanya kura zozote ili ushinde kwa zako chache kunakuwa kugumu mno. Mwanasiasa anazitaka zote kapuni mwake.
Kati ya sasa na uchaguzi ujao, wanasiasa wataisha woga, waseme mambo hadharani ili waponee kisiasa. Ombi langu ni kwamba katika harakati zao hizo wacheze ligi yao, wasiwatenganishe wananchi kwa misingi yoyote ile.
Hata katika mtindo huo wa wanasiasa kutafuta ugomvi ili wachaguliwe, wananchi wanapaswa kuwapiga darubini vilivyo, mbwa-mwitu asije kuvalia ngozi ya kondoo na kula watu. Kila mtu anapaswa kuchaguliwa kwa ubora wake, si mrengo anaoegemea.
mutua_muema@yahoo.com