MAONI: Wakenya wanajishusha hadhi kutaka wafanyabiashara wa TZ wafukuzwe kulipiza kisasi
TAIFA la kibaguzi la Tanzania limefanya mambo yake tena. Mara hii limepiga marufuku wageni kufanya biashara ndogo-ndogo, na nyingine linazodhani maalum, ndani ya mipaka yake katika hatua inayoaminika kuwalenga wachuuzi Wakenya.
Tangu zamani sijawahi kuipenda kanuni ya Tanzania ambayo ikiwazuia wageni kuajiriwa nchini humo kwa kisingizio cha kuwahifadhia Watanzania fursa za kazi.
Kanuni yenyewe ni ya kipumbavu kwa kuwa si siri kwamba Tanzania ina changamoto kubwa ya upungufu wa nguvu-kazi bingwa katika tasnia mbalimbali zinazohitaji utaalamu wa kiwango cha juu.
Eti kanuni hiyo ikimruhusu mkurugenzi wa kampuni na msaidizi wake pekee kufanya kazi humo, tena msaidizi akiagizwa kushikilia nafasi hiyo kwa muda mfupi huku akimfunza kazi Mtanzania atakayeichukua halafu.
Nakumbuka kisa ambapo wanahabari wa Kenya walioiva kikweli walitua jijini Dar es Salaam kwa nia ya kuzindua na kudumisha gazeti jipya, ila wakarejeshwa Nairobi ghafla na kulazimika kufanyia kazi zao hotelini wakirsubiri idhini ya kurudi huko lakini wapi!
Sheria hiyo ya kuwazuia wafanyakazi ni mbaya mno tayari, lakini hii mpya ya kuwazuia wafanyabiashara ndogo-ndogo inanipa mashaka kuhusu upevu wa wataalamu wa masuala ya uchumi wa taifa hilo.
Labda chuki dhidi ya jirani zao imejifanyia utando akilini wakashindwa kutumia utaalamu wao?
Chuki ilijitokeza wazi wakati wa utawala wa dikteta John Magufuli pale Tanzania ilipopiga mnada ng’ombe zaidi ya 1,300 wa Wamaasai wa Kenya waliovuka mpaka kwenda kutafuta malisho mkoani Arusha mwaka 2017.
Tanzania ilipata Sh10.2 za Kenya.
Mnamo mwaka uo huo, serikali ya Tanzania ilichoma moto vifaranga 6,400 wa thamani ya Sh12.5 za Kenya walioingizwa nchini humo kutoka Kenya kwa madai kwamba wangeeneza homa ya kuku.
Hizo si tabia za jirani anayethamini ujirani mwema.
Hivi ni vigumu kwa Tanzania kuelewa kwamba mjasiriamali wa kigeni, hata wa kiwango cha chini kabisa, ana fursa ya kupanua wigo wake na kuwa mwekezaji mzito, akawaajiri wenyeji wengi zaidi?
Hataleta manufaa mengi kuliko ushindani wa kibiashara?
Kwani Watanzania hawajui mambo yanavyokwenda nchini Kenya? Hawajui kwamba wamiliki wa maduka makuu yanayovuma kote nchini na Afrika Mashariki walianzia kwa vibanda vya kuuzia mboga-mboga?
Bila shaka Kenya na Tanzania ni kama mbingu na ardhi tunapojadili mifumo ya kiuchumi na mitazamo ya kimaisha kwa jumla. Ujamaa na ubepari ni mafuta na maji, havipatani kamwe.
Kwa muda mrefu nchini Tanzania, sera za ujamaa za mwazilishi wa taifa hilo, Mwalimu Julius Nyerere, ziliwakengeusha wananchi hivi kwamba kila aliyetajirika alichukiwa kwa tuhuma kwamba ni mwizi, asipokoma akitafutiwa makosa na kushughulikiwa mpaka afilisike.
Enzi ya Mwalimu Nyerere, umaskini ulionekana kama uzalendo hivi kwamba ni heri mtu angevaa mararu au aende nusu uchi au atembee peku kama bata kuliko kuvaa mavazi yaliyonunuliwa nje ya nchi.
Eti wakati wa baa la njaa ni heri ungeisubiri serikali ikuletee posho ya chakula cha msaada badala ya kutoka kiume na kuhangaika mpaka upate riziki.
Nchini Kenya, tangu zamani, ni vigumu sana kuzichafulia pesa jina. Kila mtu anazitaka, kwa hivyo ukithubutu kuziharibia sifa unaonekana kichaa usiyejua dunia inakwendaje.
Ni kutokana na mapenzi yetu ya pesa ambapo Watanzania hutuita wezi.
Ikiwa wizi ni uchakarikaji unaotia tonge kinywani, basi hizo ni sifa nzuri sana. Umaskini hauna staha, unamfanya mtu mzima kuonekana mjinga, mzembe na mwingi wa utoto.
Wakenya wanaofoka mtandaoni wakishinikiza Watanzania wafukuzwe Kenya wanajishusha hadhi.
Waungwana hawafanyi mambo hivyo, wanaketi kitako na kutazama kwa tabasamu pana vitoto vikichezea udongo viliokanda kwa mate mikojo.
Watanzania watakuwa jirani zetu daima, kwa hivyo ni bora tuwasaidie kupevuka.
Somo la kwanza kwao ni kwamba vikwazo vya kiuchumi na nongwa nyinginezo hudumaza makuzi ya nchi na maeneo, hivyo ni bora tuwe na ushirikiano utakaotufaa sote.
Sheria za kipumbavu kama zinazoagiza kufungwa kwa biashara za wageni wanaovunja sheria zinapaswa kubadilishwa ili biashara zenyewe zihifadhiwe kwa manufaa ya wenyeji kwa kuwa zikifungwa zinawaumiza kuliko wageni.
Pengine muda umefika kwa Tanzania na mataifa ya Afrika kwa jumla yaanzishe mfumo ambapo biashara, hata za maduka madogo, zitasajiliwa kama kampuni huru, ziwe na bima mahsusi, ili tumtenganishe mtu binafsi na biashara yake, tuulinde uchumi.
Katika hali hiyo, mwanzilishi wa biashara akikutwa na hatia, biashara yake inaweza kutwaliwa na shirika rasmi linaloweza kuiendesha kitaalamu au kuiuzia mwekezaji mwingine, pamoja na kulipa madeni ya mhalifu aliyekutwa na hatia na kufungwa gerezani.
Mikakati hiyo ikiwekwa, tutaacha kuhasimiana kibiashara na kuanza kuonana kama washirika, idadi ya watu katika mataifa yetu ianze kuonekana kama rasilmali muhimu na vilevile soko pana la bidhaa na huduma.
Tutakumbatiana, hatutachukiana.
mutua_muema@yahoo.com