Maoni

MAONI: Watanzania wahitaji kupambania demokrasia zaidi kuepuka kunyanyaswa na serikali

Na DOUGLAS MUTUA July 30th, 2025 Kusoma ni dakika: 3

KILA mpenzi wa demokrasia anayefuatilia siasa za Tanzania wakati huu anatamani nchi hiyo jirani ya Kenya isalie ilivyo sasa hivi milele, lakini ghafla anakumbuka hiyo ni Tanzania, si Kenya.

Wakati huu Watanzania wametokea kuwa jasiri mno, hasa mtandaoni, kwa kuikosoa serikali yao, na hasa Rais Samia Suluhu Hassan, bila kuogopa kushughulikiwa vibaya na vikosi vya usalama wa taifa.

Wakati mwingine unatazama au kusikiliza hoja zao nzito kuhusu mambo muhimu wanayopambania, unajiuliza wamekuwa wapi muda huu wote ambapo nchi yao imekaliwa mguu wa kausha na Chama cha Mapinduzi (CCM).

Unawakatia tamaa unapokumbuka kuwa jazba za kisiasa unazoshuhudia wakati huu huwa za kawaida wakati wa kampeni za uchaguzi mkuu, halafu watu wakarejea kwenye shughuli zao za kawaida baada ya matokeo kutangazwa hata yasipowaridhisha.

Na inaonekana wakuu wa CCM wameielewa hulka hiyo ya Watanzania na kuichukulia kama fursa hivi kwamba wanavuruga mchakato mzima wa uchaguzi kwa raha zao, wanaiba kura, wanawanyima haki wagombea na wapigakura na kuipuuzilia mbali mihemko inayofuata.

Uchaguzi huanza kuvurugwa katika ngazi ya mchujo wa kuwateua wagombea kwa kuwa CCM, ambayo huwezi kuitofautisha na serikali, ina mamlaka makuu ya kuwaidhinisha au kuwazuia watu wanaotaka kuwania nyadhifa mbalimbali.

Ndani ya CCM, ikiwa huelewani na mwaniaji wa urais, anaweza kuwaagiza wakuu wa chama wachuje jina lako kutoka kwenye orodha ya wagombea, na huo unakuwa mwisho wa safari yako ya kisiasa katika muda wa miaka mitano ijayo.

Hilo juzi limewakuta asilimia 75 ya wakuu wa sasa CCM waliotia nia ya kugombea uchaguzi utakaofanyika mwezi Oktoba, kisa na maana hawaelewani na Rais Suluhu au hawamuungi mkono kikamilifu.

Wabunge waliohudumu mihula kadha wanaendelea kulia na kusaga meno kwa kuwa CCM imewafungia nje ya uchaguzi ujao kwa kukataa kuwaidhinisha kugombea kwa tiketi yake, na hawana pa kwenda kulalamikia, hata mahakamani!

Kilio kama hicho kinatarajiwa kutokea zaidi katika vyama vya upinzani kwa kuwa ushawishi wa CCM upo hata katika mchakato wa kuamua orodha ya mwisho ya wagombea wa upinzani, kwa hivyo wataidhinishwa inaopendelea.

Hii ina maana kwamba – kwa kuwa hata tume ya uchaguzi ya Tanzania inatumikia CCM bila kificho – chama hicho tawala kina uwezo wa kuamua wabunge wa upinzani watakuwa wangapi katika bunge lijalo.

Watakaonyanyaswa, hata wakiwa maarufu kiasi gani, hawana pa kwenda kutafuta haki. Hivyo ndivyo vigogo wa siasa za upinzani nchini humo walivyonyimwa ubunge wakati wa uchaguzi uliofanyika takriban miaka mitano iliyopita.

Unatarajia kuwa watu wanaoishi katika mazingira mabovu hivyo kisiasa watapambania haki wakati wa uchaguzi na hata baadaye, lakini wapi! Hiyo si tabia yao. Huo si uzalendo eti.

Kila mtu hurejea kwenye shughuli zake za kawaida; wanasiasa wanaohisi kwamba maisha yao yamo hatarini wakakimbilia nchi nyingine, nao wananchi wa kawaida wakaanza kutuhadithia jinsi amani ya nchi yao ilivyo muhimu kuliko matokeo ya uchaguzi mkuu.

Hali huwa tofauti nchini Kenya, ambako uchaguzi unafanyika katika mazingira nafuu zaidi kisheria. Inavyokuwa nchini Kenya, hasa wananchi wakihisi kwamba uchaguzi haukuwa huru, wa haki na wazi, maandamano ya kuwalaani waliotangazwa washindi huanza hata kabla hawajaapishwa.

Kwanza tunawashtaki wanaodhaniwa kuwa wezi mahakamani, na hata huko wakitushinda tunaapa kuwatatiza mpaka wajue hawakuwaibia wajinga, wazembe wala wanyonge.

Maandamano yanafanyika mara moja na kuwanyima uhalali wanaotamani sana, hivyo wanaona aibu kutokea mbele ya dunia nzima kwani wanaonekana kama wezi wa kura wasiokubalika kwao.

Hivyo ndivyo tulivyomfanyia marehemu Rais Mwai Kibaki alipoapishwa usiku baada ya kuiba kura, tukamkaba koo mpaka akakubali kugawana mamlaka na mshindani wake, Bw Raila Odinga, pamoja wakaungana kuleta Katiba ya sasa iliyoidhinishwa mwaka 2010.

Kimsingi, kila msukosuko nchini Kenya huzaa matunda mazuri kwa kuwa wananchi hawakubali kukata tamaa. Watanzania hunyanyaswa na viongozi wao kwa kuwa wanajulikana hawafululizi kupambania haki.

Ni jambo la hakika kwamba tayari uchaguzi utakaofanyika nchini humo mwezi Oktoba umevurugwa, na nyingine nyingi zitaendelea kuvurugwa, hadi pale Watanzania watakapoamua kuwa mapambano si shughuli ya wakati wa uchaguzi pekee.

mutua_muema@yahoo.com