Maoni

MATHEKA: Serikali ijifunze kuzingatia ushauri wa wataalamu kuepuka majanga

May 8th, 2024 Kusoma ni dakika: 1

NA BENSON MATHEKA

HATUA za serikali za kukabili hatari zinazosababishwa na mvua kubwa inayonyesha sehemu tofauti nchini ni za kupongezwa japo zilichukuliwa kuchelewa.

Kama hatua hizi zingechukuliwa mapema hasa pale Idara ya Utabiri wa Hali ya Hewa ilipotangaza kuwa mvua kubwa ingenyesha nchini, janga linaloshuhudiwa kwa sasa ambapo watu zaidi ya 200 wamepoteza maisha lisingetokea.

Maafisa wa serikali katika idara zinazohusika na majanga wangechukua hatua mapema kutambua maeneo hatari kwa mafuriko, maporomoko ya ardhi, mabwawa hatari na madaraja yanayoweza kusombwa na mvua kubwa na kukatiza usafiri.

Kwa hakika, hivi ndivyo Idara ya Utabiri wa hali ya hewa imekuwa ikishauri.

Kinaya ni kuwa maafisa wa serikali ambao walipaswa kuchukua hatua mapema na kuepusha janga ndio sasa wanakupuruka baada ya maafa kutokea.

Kinachohuzunisha ni kuwa wanalaumu wakazi waliojenga makazi katika maeneo hatari utadhani hawakuwepo nyumba hizo zilipokuwa zikijengwa.

Na si wakati wa mvua ya gharika pekee. Hali sawa imekuwa ikishuhudiwa wakati wa kiangazi Wakenya wakifariki kwa njaa licha ya hali hiyo kutabiriwa.

Kusema kweli kama viongozi wangekuwa wakizingatia ushauri wa wataalamu kuweka mikakati ya kukabiliana na majanga, hasara inayoshuhudiwa wakati wa kiangazi na mvua kubwa inaweza kuepukwa au hata kupunguzwa.

Japo kila mtu anafaa kuwajibikia usalama wake, serikali ina jukumu kubwa la kutoa mwelekeo.

Haiwezi kuwataka raia kuhama makao yao kwa usalama wao bila kuwatafutia makao mbadala japo ya muda na mbinu za kuhama. Serikali ina uwezo wa kufanya hivi na kama haina, ina uwezo wa kuomba msaada kusaidia raia wake.