Maoni

Mbona Wakenya wanaoishi ughaibuni wanachukiwa?

Na DOUGLAS MUTUA March 31st, 2025 Kusoma ni dakika: 2

JARIBIO la mtu fulani kumshinikiza Rais wa Amerika, Donald Trump, amfukuze Gavana wa Nakuru, Susan Kihika, si la kuchekesha tu bali pia linafichua mambo kadha.

Sharti niseme kwamba hilo si suala la jinsia, kwa hivyo wabunge wa kike waliolitwaa na kulifanyia kikao na wanahabari walilipunguzia umuhimu, likakaa kama masuala mengine mengi ambayo huchochea wanawake na wanaume kuhasimiana.

Kila wakati suala lolote likichukua mkondo wa jinsia hushuka hadhi kwa kuwa kuna watu wengi ambao hushughulikia mada kwa uzito wake, wala hawapendi kugawanywa kwa mafungu ya wake kwa waume.

Ukitaka hoja yako iishe pumzi, ifanye ya kijinsia. Hilo ni jambo la kimsingi ambalo wanawake wengi bado hawajagundua, na ndiyo sababu wanarudia kosa hilo kila wakati. Achana nao kwa sasa.

Jaribio hilo linachekesha kwa kuwa Trump hawezi kupoteza hata nukta ya muda wake kufikiria kuhusu athari za gavana wa jimbo lolote la Afrika kutokuwepo kazini.

Trump hajali wala habali. Suala hilo halimhusu ndewe wala sikio. Hata hivyo, sina shaka kwamba aliyejaribisha janja hiyo alijua hili fika, ila akaamua kuwapa watu hoja ya kujadili, iwe na tija au la.

Lakini pia jaribio lake hilo linafichua uhusiano wa tamu-chungu uliopo kati ya Wakenya walio nchini Kenya na wenzao wanaoishi ughaibuni.

Kwa taarifa yako, Bi Kihika alikuwa mwanasheria wa masuala ya uhamiaji na familia katika jiji la Washington, D.C. na majimbo ya Maryland na Virginia kabla ya kurejea Kenya na kuwabwaga wanasiasa mahiri! Hajakwenda Amerika kuomba hela.

Ipo chuki ambayo imekuwa ikiendelea kwa muda, walio Kenya wakiwalaumu walioondoka kwa kukosa uzalendo kamili na kuikimbia nchi, nao walio ugenini wakiwaita waliosalia mahasidi wasio na sababu, wanaowachukia ilimradi tu.

Mtu anayeishi ughaibuni hupigwa darubini zaidi – hasa na watu ambao wangetamani kuishi nje ya nchi – kila anapotaka kuwania wadhifa wowote wa kisiasa.

Ataambiwa hajui chochote kuhusu siasa za Kenya, eti arejee alikohamia, awaachie Wakenya nchi yao, na ikiwa yeye ni mwanamume kamili, basi na awanie vyeo huko anakoishi na ahakikishe ameshinda.

Utadhani wanaosema hivyo wanazuru kila pembe ya Kenya kukusanya habari za siasa, hawazisomi mtandaoni na magazetini au kuzisikia kwenye vyombo vingine vya habari kama hao wanaoishi ughaibuni.

Chuki hiyo huisha kila panapotokea haja ya mchango, anayeishi nje akatakiwa kutoa dola, pauni au euro nono bila kuuliza maswali kwa sababu ‘hata wewe umepewa na Mungu’.

Anayejua siasa za Kenya zilivyo atakwambia lawama anazopata Bi Kihika hazihusiani kwa vyovyote na baraka za mapacha aliotunukiwa na mwenyezi Mungu mapema mwaka huu.

Hazihusiani kabisa na ubora au ubovu wa utawala wake katika Jimbo la Nakuru bali ni njama za kumlemaza kisiasa ili awe dhaifu kabla ya Uchaguzi Mkuu ujao, kinyang’anyiro hicho kikifika abwagike kwa wepesi.

Madai kwamba Gavana huyo amekimbia matatizo yanayoikumba sekta ya afya kwenye jimbo lake akafuata huduma hizo nje ya nchi ni unafiki mtupu, hasa ukizingatia kwamba sekta hiyo inakabiliwa na changamoto kote nchini.

Kikawaida, chuki na wivu wa wanafiki hujitokeza wazi wanapotaka ukose manufaa fulani ili mteseke nyote, badala ya kujiuliza ni kwa jinsi gani wanavyoweza kuondokana na matatizo yao bila kumuumiza mtu.

Ukweli wa Mungu ni kwamba hakuna aliye na mamlaka ya kukupokonya uraia wako pamoja na manufaa yanayoambatana nao ikiwa ulizaliwa nchini Kenya. Naam, watajaribu kila njia, lakini haki itasimama. Wao si Wakenya kukuzidi wewe.

Haiwezekani kwamba jukumu la wanaoishi ughaibuni ni kulipa ushuru bila kuchelewa pekee, wakitaka manufaa fulani uraia na uzalendo wao unawekwa kwenye mizani.