Maoni

MAONI: Nyadhifa kuu serikalini si za kuzawidi familia za wanasiasa

Na MARY WANGARI January 29th, 2026 Kusoma ni dakika: 2

HIVI majuzi, Rais Ruto alimtunuku Ida Odinga, mjane wa marehemu kiongozi wa upinzani na aliyekuwa Waziri Mkuu Raila Odinga, nafasi ya kifahari kama balozi wa Kenya katika shirika la Umoja wa Mataifa, UNEP.

Suala kuhusu iwapo anastahiki au la, si hoja, lakini iwapo umekuwa ukifuatilia kwa muda masuala ya kisiasa katika taifa hili, basi hakuna jipya kuhusu uteuzi huu.

Ulitarajiwa kufanyika wakati wowote ama kupitia wadhifa mkuu serikalini au vinginevyo.

Katika miaka ya hivi karibuni, kumezuka mtindo wa kutatanisha unaozungumziwa kwa minong’ono ya chini hasa katika enzi hii isiyostahimili hisia tofauti.

Kazi za kifahari na nyadhifa za uongozi nchini na kimataifa zimeonekana kuwa hifadhi ya familia, jamaa na wandani wa wanasiasa zinazoridhishwa watoto, wanandoa au mandugu wa viongozi wanapoaga dunia au kustaafu.

Kadri miaka inavyosonga, unasaba na utabaka umegeuka uhalisia mpya unaotekelezwa mchana peupe.

Wakenya wameshuhudia watoto, wake na mandugu wakirithi nyadhifa za jamaa zao wanasiasa au kutafutiwa kazi zenye mishahara mikubwa serikalini bila kujali ikiwa wamefuzu au la, utadhani ni utawala wa kifalme.

Uteuzi wa Ida ulijiri wiki chache tu baada ya gavana Sakaja kumtunukia mpwa wake Odinga, nafasi ya kazi aliyoacha marehemu mamake, katika kampuni ya Maji ya Nairobi.

Katika taifa lenye viwango vya juu vya ukosefu wa ajira ambapo vijana huzomewa kila uchao kwa kukosa ubunifu na kutegemea ajira huku wasomi wakiishiwa na viatu wakisaka ajira bila mafanikio, kushika mabango barabarani na wengine hata kujitia kitanzi kwa kukata tamaa, kuona watu wakirushiwa kazi na kuteuliwa kirahisi kunawaacha wengi na maswali mengi kuliko majibu bila ujasiri wa kusema chochote.

Katika familia nyingi nchini, ni muujiza mkubwa mtu mmoja anapojaaliwa kupata ajira serikalini au katika kampuni ya kifahari wengi wao wakiwa tegemeo la pekee kwa familia, ukoo wote.

Wachache waliobahatika kupata ajira mjini wanafahamu fika uzito wa kubeba jamii nzima mabegani mwao wakilazimika kugawa kidogo wanachopata hata kabla ya kuanzisha familia zao wenyewe.

Umuhimu wa kazi, teuzi na nyadhifa za kisiasa kutolewa kwa misingi ya kufuzu baada ya kupigwa msasa, kushiriki chaguzi na kushinda kwa njia ya haki na ya wazi, hauwezi kusisitizwa vya kutosha.

Madhara yanayosababishwa na ugavi wa nyadhifa serikalini na teuzi kimataifa kwa misingi ya unasaba na utabaka hasa kwa viongozi ni mengi na ni sharti yakomeshwe.

Nyadhifa za uongozi au kazi zinapaswa kutwaliwa kupitia mchakato wenye usawa na wala sio kuzawadia.