ODM@20: Oburu hana hoja chakavu kama wengi walivyoamini!
SENETA wa Siaya, Oburu Odinga anasalia kuwa mtu muhimu katika historia ya Kenya kwa hisani ya nduguye mdogo marehemu Raila Odinga.
Nilikuwa kati ya watu waliojiuliza sababu ya Oburu kurithi nafasi ya Raila Odinga alipofariki.
Kamati kuu ya ODM ilimtunuku nafasi hiyo na kuidhinishwa baadaye. Nikajiuliza kama chama kilikuwa cha familia.
Nilimwona awali Oburu kuwa mtu asiyeweza kusukuma ajenda ya mapinduzi.
Nilidhania hoja zake zilikuwa chakavu kutokana na umri wake. Kumbe nilikuwa nimekosea.
Bwana huyo anayejiita kiongozi wa vijana ana sifa toshelevu
Kwanza ili kuwavutia pengine vijana angalau anapiga viatu vya vijana kabisa.
Anasema mambo mengi kwa hekima anapokuwa jukwani.
Huenda asiulize urais kwa kutokuwa machachari kama Raila lakini nina hakika anaweza kutoa mwelekeo wa kadri katika chama cha ODM ambacho kimo katika hatari ya kugawanyika kutokana na nyufa dhahiri miongoni mwa viongozi wa chama hicho kilichodumu kwa miaka ishirini sasa.
Wanaotaka kusukuma ajenda ya ODM na pengine kupalilia mbegu alizoacha Raila Odinga ni sharti wamkaribie.
Inawezekana ana siri kubwa kama kaburi alizoambiwa na Raila ambazo hajazitaja, labda anadondoa polepole.
Maandalizi ya sherehe za maadhimisho ya miaka 20 tangu kuasisiwa kwa ODM ulikuwa mtihani mkubwa kwa Oburu kwa sababu kadhaa.
Kwanza, anaongoza mkutano ambao Raila hayuko hai na pili unafanyika bila mahudhurio ya Raila.
Oburu ana kibarua kuirejesha hadhi ya ODM na kuwa chama cha kitaifa wala si cha kieneo. Kwa kufanya hivyo, chama kitapata sura ya kitaifa jinsi ilivyokuwa katika uchaguzi mkuu wa 2007.
Nguvu za ODM chini ya Oburu Odinga zinatakiwa kutambulika katika uchaguzi mkuu wa 2017.
Je, ODM kitakuwa katika muungano? Kina nafasi ya kubuni serikali ijayo?
Baada ya uchaguzi huo, athari ya ODM katika kumchagua spika wa bunge la 14 na spika wa bunge la seneti pia itatiwa katika mizani.
Akifaulu kwa hilo, atakuwa amepiga hatua kubwa kushinda Raila.
ODM ilipoteza nafsi ya spika kwa Justine Muturi baada ya uchaguzi wa 2013.
Vivyo hivyo, katika bunge la seneti Ekwe Ethuro wa muungano wa Jubilee ndiye aliyekuwa spika.
Hayakuishia hapo katika uchaguzi wa spika wa bunge 2017, Ken Lusaka alishinda kwa seneti na Justin Muturi akachaguliwa kwa mara pili.
Mwanawe Jaramogi ambaye alisomea Urusi atatakiwa pia kuhakikisha mbunge Babu Owino na seneta wa Nairobi Edwin Sifuna hawaondoki kwa chama jinsi inavyodaiwa na baadhi ya watu.
Oburu ana kazi kubwa ya kujenga jina na pia chama.
Paul Nabiswa ni mhariri, NTV.