Orengo ni shujaa kivyake, hategemei cha nduguye!
RAFIKI zake humtambua kama JABO. Yaani James Aggrey Bob Orengo, baadhi humuita Jim.
Majuzi gavana huyo wa Siaya amejipata mashakani baada ya kusema kuwa uhusiano kati ya ODM na serikali jumuishi unatakiwa kuwa wa tahadhari kubwa.
Mbunge Samuel Atandi, mwenyekiti wa kamati ya bunge kuhusu bajeti akamkemea Orengo kwa kumtaka Raila kuwa makini anaposhirikiana na Rais Ruto.
Haijaisha hapo baadhi ya wasomi kutoka Siaya wamemtaka Orengo kuomba msamaha la sivyo atabanduliwa.
Wanaompigia kelele Orengo inawezekana hawajafuata historia yake ya siasa kabla na baada ya kuingia bungeni.
Ni mtu mwenye fikra za mapinduzi katika nyakati zote na anapokuwa vuguvugu mara chache ni kwa masilahi yake tu.
Alianza vita vya ukombozi akiwa bado shuleni, na akafukuzwa kwa mara kwanza shuleni Alliance akiwa kidato cha kwanza. Sasa wangwana wanaotaka kumfukuza saa hizi wafahamu kuwa bwana huyo alizoea kufukuzwa zamani?
Katika Chuo Kikuu cha Nairobi mnamo 1972 akiwa kiongozi wa wanafunzi aliandaa migomo na amejenga historia kubwa ya uongozi wa wanafunzi wa vyuo vikuu nchini.
Wakati wa chama kimoja cha KANU, Orengo na wenzake sita walibuni jeshi imara la upinzani ndani ya KANU maarufu kama “Seven Bearded Sisters” kiasi cha kumtisha aliyekuwa Mwanasheria Mkuu Charles Njonjo ambaye baadaye alikuwa waziri wa sheria.
Wenzake walikuwa Chibule wa Tsuma, Mashengu wa Mwachofi, Koigi wa Wamwere, Lawrence Sifuna na Chelagat Mutai.
Ujasiri wa Orengo ambaye alipoteza kiti chake cha ubunge akipigania haki za wanajeshi waliopanga kuipindua serikali ya Rais wakati huo Daniel Toroitich Arap Moi 1982.
Alizungushwa katika magereza tofauti nchini. Ni mawakili wachache mno waliokuwa na ubavu wa kuwatetea wanamapinduzi.
Mmoja wao alikuwa Moses Wetangula ambaye sasa ni spika wa bunge la taifa.
Orengo mwenyewe anasema alipitia mateso yasiyoelezeka. Sasa mtu wa sampuli hiyo anaambiwa anyenyekee ama atakiona cha mtema kuni.
Sijamaliza simulizi za Orengo. Alikuwa kati ya wanasiasa wachanga waliosukuma ajenda ya ukombozi wa pili hadi kifungo cha katiba cha 2A kikaondolewa kupisha mfumo wa vyama vingi nchini.
Ni hawa vijana ndio waliowashawishi Jaramogi Oginga Odinga, Martin Shikuku, Ahmed Bamahriz na Masinde Muliro kubuni vuguvugu la FORD kabla ya kugawanyika na kuwa FORD – K na FORD Asili.
Je, tunajua Orengo ni kati ya wabunge wanne tu walioshinda katika uchaguzi wa ubunge Luo Nyanza nje ya chama cha NDP cha Raila Odinga 1997?
Huyo Orengo mmoja aliwahi kugombea Urais 2002 tena baada ya kufanya mapinduzi katika chama cha SDP.
Bw Nabiswa ni mwanahabari wa NTV