Panyako, Karish wasiende kortini, wajipange kwa 2027: Hizi hapa sababu…
WALIOSHINDWA katika chaguzi ndogo zilizoandaliwa wiki jana wanastahili kumeza mate machungu badala ya kuelekea kortini kusaka haki yao.
Wikendi, Kiongozi wa Wiper Kalonzo Musyoka alisema kuwa upinzani unawazia kupinga matokeo ya kura za maeneobunge ya Malava na Mbeere Kaskazini kortini.
Katika eneobunge la Malava, Seth Panyako aliyekuwa akipeperusha bendera ya DAP-Kenya alibwagwa na David Ndakwa wa UDA kwenye kinyang’anyiro kilichokuwa kikali mno.
Katika eneobunge la Mbeere Kaskazini, Leo Muthende alimlambisha sakafu Newton Kariuki maarufu Karish.
Chaguzi hizi zilikuwa na ushindani mkali na upinzani hadi leo unadai kuwa ulifanyiwa hiana huku ukitilia shaka uwazi unaodaiwa kuwepo.
Mwanzo, ni haki ya viongozi ambao wanahisi kwamba walichezewa ngware kwenye uchaguzi huo kuenda mahakamani kuupinga.
Hata hivyo, hiyo huenda ikawa ni kazi bure na kupoteza wakati kwa sababu mkondo wa kupata haki huwa ni mgumu sana hapa nchini.
Itabidi kesi hiyo ifikishwe mahakamani, pande zote ziwasilishe utetezi wao na hata korti inaweza kuamua kura ihesabiwe upya.
Iwapo kweli upinzani utashinda kesi hiyo, upande wa washindi unaweza kukata rufaa na kesi hiyo tena ianze kusikilizwa na kuamuliwa katika mahakama hiyo.
Kikiumana na upinzani upate ushindi tena, kesi hiyo inaweza kufika katika Mahakama ya Juu ambapo pia ushahidi uliopo utatathminiwa na uamuzi utolewe.
Iwapo upinzani utashinda kesi hiyo tena, mchakato mwingine wa kufahamisha Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) iandae uchaguzi wenyewe utafuata.
Vivyo hivyo, wabunge waliochaguliwa wanaogemea upande wa serikali wanaweza kushinda kesi hiyo lakini upinzani ukate rufaa katika mahakama zote hadi ifikie Mahakama ya Juu.
Hapa nchini kesi za uchaguzi huchukua muda mrefu wa hadi miaka miwili kusikilizwa na kuamuliwa kuanzia Mahakama Kuu, ile ya Rufaa na Mahakama ya Juu.
Kufikia kuamuliwa kwa kesi za Bw Panyako na Karish iwapo zitakuwa zimewasilishwa mahakamani, basi uchaguzi mkuu wa 2027 utakuwa umebisha na kutimia.
Pili, hapa nchini kampeni huwa zinaanza mapema sana na ifikiapo Januari 2026, zitaanza kuchacha kwa sababu itakuwa imebaki miezi 20 pekee kabla ya uchaguzi mkuu kuandaliwa.
Badala ya kuweka juhudi zao kwenye mahakama, Karish na Panyako wanastahili kuweka mikakati ya kuwarai wapigakura wawachague mnamo 2027.
Mnamo 2004, aliyekuwa Mbunge wa Kisauni na Waziri Karisa Maitha aliaga dunia na kusababisha uchaguzi mdogo katika eneobunge hilo.
Katika uchaguzi mdogo ulioandaliwa mnamo Desemba 16, 2004, Ananiah Mwaboza wa NAK alimshinda Hassan Joho wa LDP na akakamilisha muhula uliosalia.
Bw Joho ambaye sasa ni Waziri wa Madini, hata hivyo alijikusuru na kujipanga vyema kisha akatwaa kiti hicho mnamo 2007 na akaishia kuhudumu mihula miwili kama gavana wa Mombasa.
Pia kuna baadhi ya wanasiasa walioshinda chaguzi ndogo lakini wakaishia kubwagwa kwenye uchaguzi mkuu na kusahaulika kabisa.
Bw Mwabozo alishindwa na Bw Joho 2007 na hajawahi kupata uhai wa kisiasa. Vivyo hivyo, Davis Nakitare ambaye alirithi kiti cha Saboti baada ya kifo cha Wamalwa Kijana mnamo 2003, hajawahi kuambulia chochote kisiasa.
Siasa hubadilika na badala ya Mabw Karish na Panyako kupoteza muda wakipambana kortini, wajipange vizuri kwa 2027.