Maoni

MAONI: Raila atulie, Gen Z watatufikisha Canaan

Na CECIL ODONGO June 25th, 2024 Kusoma ni dakika: 2

KINARA wa Azimio la Umoja, Raila Odinga, anastahili kufyata ulimi na awache kizazi cha vijana maarufu kama Gen Z kutufikisha Canaan.

Wiki mbili sasa, vijana wamekuwa wakiandaa maandamano makubwa ya kupinga Mswada wa Fedha 2024.

Hii leo, Jumanne, Juni 25, 2024 wabunge watakuwa wakipigia kura tena mswada huo kwa mara ya mwisho na mbivu na mbichi itafahamika kama utapita au utaangushwa.

Kutokana na hali hii, vijana wanatarajiwa kuandaa maandamano makubwa tena katika miji mbalimbali nchini kuwasuta wabunge dhidi ya kupitisha mswada huo unaokabiliwa na utata na unaopendekeza nyongeza ya ushuru.

Tangu taifa hili lijinyakulie uhuru, familia ya Jaramogi Oginga Odinga ndiyo imekuwa ikifahamika kutokana na kuendeleza maasi dhidi ya serikali.

Mzee Oginga alipigania maslahi ya raia tangu enzi za mbeberu hadi mauti yake mnamo 1994.

Baada ya kupigana na kuhakikisha Kenya imejinyakulia uhuru, marehemu Oginga aliishia kunyanyaswa na tawala za Mzee Jomo Kenyatta na Rais Daniel Arap Moi.

Alihangaishwa kiasi cha kuwa mara nyingi alikuwa akiwekewa kifungo cha nyumbani na pia familia yake ilikuwa ikiandamwa naye Raila akafungwa miaka tisa gerezani.

Licha ya jasho na juhudi zake kupigania haki za raia, Bw Jaramogi aliaga dunia bila kuonja matunda hayo huku waliomnyanyasa wakiendelea kufurahia jasho la raia.

Tangu kifo cha babake, Bw Raila Odinga, ambaye kwa sasa ndiye kiongozi wa ODM, amekuwa sura ya upinzani nchini, lakini ikifika kura anapoteza kwa njia tatanishi.

Si mara moja, Waziri Mkuu huyo wa zamani na wafuasi wake wamejitokeza kushiriki maandamano baada ya uchaguzi mkuu.

Kinaya ni kuwa katika maandamano hayo, ukabila umekuwa ukishamiri huku jamii ya Raila ikirejelewa kama inayozua fujo.

Mara si moja kiongozi huyo wa ODM amekuwa akijitokeza na kuwapigania raia, lakini matokeo yake huwa kurushiwa vitoza machozi na wafuasi wake kunyoroshwa na polisi.

Mateso haya yote yametosha na nia na ndoto ya kigogo huyo wa siasa za upinzani zitatimia kupitia vijana hawa wa Gen Z ambao sasa wanaendeleza maasi dhidi ya serikali.

Nina imani kuwa vijana hawa wataweza kuwafikisha Wakenya Canaan, mahali ambapo Bw Odinga hakufaniwa kuwafikisha.

Hata katika Bibilia, Musa aliteseka na Waisraeli kwenye safari ambayo ilikuwa na changamoto tele lakini hakufanikiwa kufika Canaan.

Kama tu Musa, Bw Odinga alionyeshwa Canaan japo huenda asifike lakini hiki kizazi cha Gen Z kimeonyesha kuwa kuna mwamko mpya katika kupigania maslahi ya nchi.

Mwamko huu mpya wa vijana haufai kupuuzwa na ni vyema serikali isikize kilio cha hawa vijana na kutimiza ahadi ilizotoa kwa raia.

Kizazi hiki si kama Bw Odinga ambaye mbinu zake za kuandaa maandamano zilieleweka, na polisi walikuwa wakitumika kuwazima wafuasi wake kutokana na amri ya walio kwenye utawala.

Hii ni kinyume na hawa Ma Gen Z ambao hawana fujo na wanatumia teknolojia kueleza ghadhabu zao dhidi ya utawala wa sasa.

Kwa hivyo, Raila anastahili kukimya tu na awaache vijana waendeleze maasi yao jinsi ambavyo wanataka.

Akizungumza tu basi ataharibu mambo na kutakuwa na fikira anashirikiana nao kutekeleza shughuli zao.

Enzi za Raila kuongoza maandamano zimeisha na sasa vijana watambe ili kuhakikisha kuwa raia wanapata haki.

Pengine kihistoria, kizazi hiki ndicho kiliandikiwa kuwa kingewapa Wakenya ukombozi kutoka kwenye minyororo ya ukabila, ufisadi na uongozi mbaya.