Raila na Ruto walihujumu vita dhidi ya ufisadi kwa kuokoa Sakaja
Wote wawili wanaoshirikiana katika Serikali Jumuishi wamekuwa wakishutumu vikali ufisadi hasa katika Bunge la Kitaifa na Mahakama. Lakini swali kuu linalowachoma wananchi ni: Je, wanamaanisha wanachosema, au ni maneno matupu yasiyoendana na vitendo vyao?
Viongozi hao wawili wamekuwa mstari wa mbele kutoa hotuba kali dhidi ya ufisadi. Mara kwa mara, wamewahutubia Wakenya kuhusu haja ya kuondoa ufisadi serikalini, kurejesha maadili ya uongozi, na kuchukuliwa hatua wote wanaohusishwa na ubadhirifu wa mali ya umma bila kujali hadhi na vyeo vyao.
Lakini pale ambapo Gavana Johnson Sakaja, ambaye amekuwa akituhumiwa vikali na madiwani wa Nairobi kwa usimamizi mbovu wa fedha za kaunti, anapojikuta katika hali ya kulazimika kuwajibika, viongozi hao wawili waliingilia kati kwa njia ya kisiasa kumlinda.
Hii inaibua maswali makubwa kuhusu iwapo vita dhidi ya ufisadi vinaendeshwa kwa misingi ya haki na ukweli, au kwa upendeleo wa kisiasa. Je, ni kweli kuwa sheria ni sawa kwa wote, au kuna “watakatifu” wasioguswa kwa sababu wana uhusiano wa karibu na wakubwa serikalini au upinzani?
Kitendo cha kuokoa kiongozi anayetuhumiwa bila kumpa nafasi ya kujibu mashtaka dhidi yake katika majukwaa ya kisheria kinakiuka msingi mkuu wa uwajibikaji wa umma.
La busara ingekuwa kuruhusu taratibu halali zichukue mkondo wake badala ya kuingilia na kuwalemea wawakilishi wa wananchi.
Kwa hivyo, ni wazi kwamba hatua ya Raila na Ruto ya kumuokoa Sakaja wakati wa tuhuma kali kutoka kwa madiwani ambao jukumu lao ni kumwajibisha ni ishara ya wazi ya kusema na kutenda kinyume.
Wanahubiri haki kwa raia, lakini kwa vitendo, wanakinga wale wanaopaswa kuwajibika licha ya wao kulalamika kuwa uovu aliodaiwa kuhusika nao umekithiri nchini.
Ufisadi hauwezi kuisha kama vita vyake vinaendeshwa kwa kigezo cha nani ni wa upande gani wa kisiasa. Kenya haihitaji maneno matamu bali vitendo halisi. Wakati umefika kwa viongozi kuacha siasa za kulindana na kuanza siasa za kuwasimamia wananchi kwa ukweli.