TAHARIRI: Tuzingatie msemo wa tahadhari kabla ya hatari
NA MHARIRI
MASWALI nomi yameibuka kuhusu mapuuza ya tamathali ya msemo kuwa tahadhari kabla ya hatari.
Fikra hii imeibuliwa na hatua zinazochukuliwa kwa sasa na taasisi za serikali kuhusu mahangaiko yanayotokana na mafuriko.
Kwa mfano, serikali ilisubiri hadi Jumanne kuanza kutekeleza hitaji la kisheria kuwa wananchi wasijenge makao karibu na mito.
Serikali ilianza kutekeleza hitaji hilo la kisheria baada ya mafuriko kuangamiza mamia ya Wakenya hasa wanaoishi karibu na maeneo ya mito.
Hatua hiyo ilitekelezwa bila kutafuta mahali mbadala ambapo watu hao wangehamia.
Wengi wa waathiriwa wa hatua hiyo ni wakazi wa jiji la Nairobi ambao ni wapangaji wa nyumba.
Hii ikiwa na maana kuwa nyumba hizo zina wamiliki, yamkini matajiri, walionyakua ardhi ya serikali na kujenga hapo halafu wakawa wanajipa hela kwa njia haramu.
Japo serikali ya Rais William Ruto iliahidi kuipokeza kila familia iliyoathiriwa Sh10,000, yakini wakiwemo wanaobomolewa makao, kupata nyumba ya kukodi Nairobi si lele-mama.
Unaposahaulia mbali upatikanaji wa nyumba, Sh10,000 ni pesa ndogo sana ambazo hazitoshi kulipa kodi kwa miezi mitatu jinsi serikali ilivyosema.
Inapokumbukwa kuwa wengi wa waathiriwa watakaopokea pesa hizo ni waliopoteza mali zao baada ya mafuriko ‘kufagilia’ mbali nyumba zao na mali zao zote kupotea, usaidizi huo wa serikali unakuwa mdogo zaidi kuweza kumnyanyua mhasiriwa.
Naam, huenda wapo Wakenya wenye nia njema watakaochanga pesa na mali ili kuzipa nafuu familia hizo. Hata hivyo, serikali iliyotahadhari kabla ya hatari inapaswa kuwa na hazina ya majanga ambayo inaweza kutumiwa kwa wakati kama huu.
Ikumbukwe pia kwamba serikali ilikuwa imetangaza kutenga takribani Sh32 bilioni kwa ajili ya El Nino. Japo huenda kiwango hicho kilipunguzwa, maswali yanaulizwa kuhusu zilikoenda pesa hizo.
Tumejifunza nini kutokana na mkasa huu uliosababishwa na mvua kubwa? Kwamba taasisi zetu zilizotwikwa jukumu la kushughulikia dharura hasa mafuriko, ambazo kwa hakika ni nyingi tu, zinafaa kuzinduka kwenye usingizi wa pono ili kutoa “kinga badala ya tiba”.
Iwapo taasisi hizi zinazozidi sita zingekuwa ange, maafa mengi yaliyoshuhudiwa, ambayo yanaendelea kushuhudiwa nchini, hayangetukia kwa kiwango hicho.
Ni wakati mwafaka wa taasisi hizo kujipiga ubongo na kuwajibika ipasavyo.