Maoni

TAHARIRI: Ujenzi na ukarabati viwanjani ukamilike mapema kwa Afcon

June 1st, 2024 2 min read

NA MHARIRI

UJENZI na ukarabati unaoendelea katika viwanja vitakavyotumika kuandaa fainali za CHAN pamoja na Afcon 2027 ni vyema ukamilike mapema kuzuia taifa letu kupoteza nafasi hiyo.

Serikali inapaswa kushirikiana na Shirikisho la Soka Nchini (FKF) kufuatilia kazi inayofanyika, pamoja na miundombinu mingine zikiwemo hoteli, barabara, viwanja vya ndege ili kuridhisha wakaguzi wa Shirikisho la Soka (CAF).

Kenya ni moja ya mataifa matatu yatakayoandaa fainali za Afcon 2027 pamoja na mataifa jirani ya Tanzania na Uganda, hivyo, ni jukumu letu kuhakikisha tunajiandaa mapema tukikumbuka kwamba 2027 sio mbali.

Ni miaka mitatu tu iliyobaki kabla ya michuano hiyo mikubwa barani, hivyo tunapaswa kuhakikisha timu ya taifa inaandaliwa mapema kabla ya kikosi kamili kutajwa, siku chache kabla ya fainali hizo.

Itakuwa vyema iwapo tutakuwa na kikosi imara kitakachotoa upinzani mkali wakati wa fainali hizo zitakazofanyika baada ya zile za 2025, nchini Morocco.

Tulishuhudia fainali za aina yake nchini Ivory Coast ambako timu ya taifa hilo ilipigana vikali na kutinga fainali kabla ya kungoa Nigeria na kutwaa ubingwa, michuano yenyewe ikijumuishwa kati ya ile bora kuwahi kuandaliwa.

Tunaamini maandalizi yanayofanyika, ukiwemo ukarabati na ujenzi kwenye viwanja vyetu utamaliziika mapema kwa manufaa ya wanasoka wetu.
Kutokana na ukosefu wa viwanja vya kimataifa hapa nchini, Harambee Stars itachezea mechi za nyumbani nchini Malawi.

Imepangiwa kukutana na Burundi mnamo Juni7, kabla ya kucheza na Ivory Coast hapo Juni 11 ugani Mbingu Mutharika katika mchujo wa kuwania nafasi ya kufuzu kwa Kombe la Dunia la 2026.

Vijana wetu wanahitaji viwanja vya kujiandalia, wakati idara ya kiufundi ikiangalia talanta miongoni mwa wachezaji wa umri mdogo ambao kufikia wakati huo watakuwa wamekomaa kuchezea timu kuu ya taifa.

Harambee Stars imekuwa ikisuasua katika michuano hii na hakuna wakati imesonga kutoka hatua ya makundi tangu ishiriki kwa mara ya kwanza 1972, lakini Wakenya wanasubiri kwa hamu kushuhudia ikipiga hatua, badala ya kuwa wasindikizaji kama kawaida.

Mbali na kupiga hatua, mataifa yaliyowahi kuandaa fainali hizi yamefanikiwa kwa kiasi kikubwa, mbali na milango yao kufunguka kwa wageni ambao wamechangia katika kuimarisha mapato yao kitalii.

Kwa kushirikiana na majirani zetu Tanzania na Uganda, tunaamini fainali hizi zitaleta msisimko mkubwa na kuinua utalii na biashara katika eneo hili la Afrika Mashariki.