Maoni

TAHARIRI: Usawa wafaa kuzingatiwa katika Supa ligi

June 8th, 2024 2 min read

NA MHARIRI

NI wajibu wa Shirikisho la Soka Nchini (FKF) kuhakikisha marefarii wanaosimamia mechi zilizobakia kwenye Supa Ligi ya Kitaifa (NSL) watatenda haki bila kupendelea timu fulani kama ambavyo imewahi kufanyika hapo awali.

Ni mechi nne pekee zilizobakia kabla ya ligi hii kutamatika ambapo timu mbili za kwanza zitafuzu moja kwa moja kushiriki Ligi Kuu ya Kenya (FKF-PL) huku ya tatu ikishiriki mchujo wa kufuzu, lakini tayari kumezuka gumzo kuhusu uamuzi wa kushangaza katika baadhi ya mechi muhimu.

Ni matumaini yetu kwamba marefarii watakaochezesha mechi hizo watafanya kazi bila kupendelea upande wowote ili mshindi apatikane kihalali badala ya njia ya mkato.

Mbali na baadhi ya uamuzi wa kupendelea kufanyika, vile vile kumekuwa na fujo ambazo zimeanza kuwapa mashabiki wasiwasi kuhusu usalama wao.

Utamu wa mpira ni mashabiki kuingia uwanjani kushangilia timu zao bila kuwa na uoga, hivyo litakuwa jambo la busara iwapo mashabiki wapenda amani watapata uhuru wa kushuhudia timu zikisakata na kushinda au kushindwa kihalali.

Amani ni muhimu viwanjani ili wachezaji wapate fursa ya kusakata soka safi itakayovutia makocha wa timu kubwa, wakiwemo maskauti ambao huzuru nchini kutafuta vipaji.

Mbali na usalama wa mashabiki, kadhalika wachezaji lazima nao wajihakikishie usalama wao ili waondoe wasiwasi na hofu wakati wachezaji wakitoa burudani kuwafurahisha wafuasi wa mchezo huu unaopendwa na wengi.

Kufikia sasa, timu za Mara Sugar FC na Mathare United zinafukuzania tiketi mbili za kufuzu moja kwa moja hadi FKF-PL, wakati Naivas na Nairobi United zikipigania tiketi ya kushiriki mchujo wa tiketi ya mwisho.

Mechi zinazohusu timu hizi zinachangamoto kubwa na itabidi waamuzi watakaopewa jukumu wahakikishe wanafuata sheria ili kusiwe na malalamiko wakati wa mechi hizo muhimu.

Iwapo waamuzi watazichezesha bila kupendelea na wachezaji waachie marefarii kazi yao badala ya kuwafokea kila wakati, ligi itapata umaarufu mkubwa na mashabiki wengi watafika viwanjani kushuhudia mechi hizi kama wametulia.

Kama ilivyo katika mataifa yaliyoendelea kisoka, mashabiki wanapaswa kushangilia timu zao kwa amani na utulivu badala ya kujiingiza kwenye fujo ambazo zinaweza kuchangia timu zao kuadhibiwa vikali.

Tunazitakia kila la heri timu zote tatu zinazopigania nafasi ya kufuzu na kushiriki FKF-PL msimu ujao, huku tukiamini kwamba mashabiki watashuhudia mechi zilizobakia bila kuzua fujo.