• Nairobi
  • Last Updated April 30th, 2024 6:55 PM
Tamko la Rais litaua motisha wa madaktari hata wakirudi kazini

Tamko la Rais litaua motisha wa madaktari hata wakirudi kazini

Na BENSON MATHEKA

TAMKO la Rais William Ruto Jumapili iliyopita kwamba serikali haina pesa za kutimizia madaktari wanaogoma wakitaka kuongezewa mshahara matakwa yao linaweka nchi katika hali tata ikizingatiwa kuwa huduma katika hospitali za umma zimekwama.

Ni tamko linaloacha maswali kuhusu kujitolea kwa serikali kufanikisha sera yake ya mpango wa afya kwa wote na inachotaka Wakenya kusadiki ni kuwa mpango huo ni kashfa tu.

Sidhani kuna muujiza ambao serikali inaweza kutumia kufanikisha Mpango wake wa Afya ya Jamii maarufu kama SHIF bila ushirikiano wa madakkari na wafanyakazi wote katika sekta ya afya.

Hii ni licha ya kupanga kukata kila mfanyakazi asilimia 2.75 ya mshahara wake kila mwezi kufadhili mpango wa afya ya jamii. Tuseme madaktari watakubali kurudi kazini bila kutimiziwa matakwa yao.

Hili likitendeka, hawatakuwa na motisha wa kufanya kazi na huduma zitadorora. Katika hali hii, ni mgonjwa, ambaye anakatwa mshahara wake kwa lazima kufadhili huduma za afya, atakayeumia.

Hii ndiyo kashfa niliyotaja hapa juu. Serikali iliyo na nia njema ya kufanikisha mpango kama huu, haiwezi kuruhusu mgomo wa wahudumu wake wa afya.

Tuseme ni kweli serikali haina pesa za kutimiza matakwa ya madaktari alivyosema Rais, basi inafaa kueleza inapotoa pesa tunazoona ikifadhili maisha ya kifahari ya maafisa wake.

Ni tamko la kuvunja moyo na linaloenda kinyume na mchakato wa kisheria wa kutatua mzozo huo ambao uko kortini.

Ndio, najua madaktari wamekaidi maagizo ya korti kurejea kazini lakini hii sio sababu ya serikali kupuuza maslahi ya wagonjwa wanaoteseka kwa kukosa huduma katika hospitali za umma.

  • Tags

You can share this post!

Kindiki atangaza Jumatano kuwa siku ya mapumziko,...

Familia 2,600 kufurushwa Mukuru-Mariguini kupisha ujenzi wa...

T L