MAONI: Trump analenga kufufua ubaguzi wa rangi nchini Afrika Kusini
RAIS wa Amerika, Donald Trump, ameanika unafiki wake kwa kutaka kuwaalika nchini mwake raia wa Afrika Kusini ambao ni vizazi vya makaburu walioendeleza ubaguzi wa rangi dhidi ya Waafrika weusi walio wengi huku akitimua raia wa kutoka nchi nyingine.
Japo anasema anawaalika wanaolengwa na utawala wa Rais Cyril Ramaphosa katika mageuzi ya umiliki wa ardhi ya kilimo Afrika Kusini, akitaka waishi Amerika kama wakimbizi wanaotoroka dhuluma, Rais Trump anaendelea kuwaondoa wahamiaji wa nchi nyingine ambao walitorokea nchi yake kuepuka hali ngumu, hasa vita, katika nchi walizotoka.
Hivyo basi, kwa mtazamo huu, Rais Trump anaendeleza ubaguzi wa hali ya juu zaidi ya anavyodai unaendelezwa na serikali ya Afrika Kusini kwa kuanzisha mageuzi ya ardhi yanayonuiwa kufaidi Waafrika weusi walio wengi.
Ni wazi kuwa kwake, Mwafrika mweusi hana haki ya kumiliki ardhi ya kilimo Afrika Kusini bila hata kujali nchi hiyo ni huru na kwamba anaodai analenga kutetea hawajalalamikia kudhulumiwa kwa kupokonywa ardhi yao, isipokuwa washirika wake wachache wanaolenga maslahi ya kibinafsi.
Unafiki huu wa Rais Trump katika hali kama hii unaweza tu kufasiriwa kama kisingizio na mbinu ya kuingilia mataifa anayohisi yanaenda kinyume na sera zake za kigeni.
Analenga Afrika Kusini kwa sababu ya ukuruba wake na Urusi na kupinga uvamizi wa Israeli ambayo ni mshirika mkuu wa Amerika katika Mashariki ya Kati huko Ukanda wa Gaza.
Inafaa kukumbukwa kuwa ametangaza kutwaa Gaza na kutishia kutwaa nchi nyingine huru na si ajabu unafiki wake ukamfanya atishie kutwaa Afrika Kusini! Anachofanya rais huyo wa Amerika ni kufufua ubaguzi wa rangi Afrika Kusini, hatua ambayo Afrika nzima na ulimwengu kwa jumla unafaa kukataa.