Upinzani umelala tangu Raila aanze kuwania kiti AU
TANGU kiongozi wa Azimio la Umoja Raila Odinga atangaze azma yake ya kuwania uenyekiti wa Tume ya Umoja wa Afrika (AUC), Upinzani umeonekana kukosa makali katika kukosoa serikali.
Kwa mfano, Bw Odinga alijitokeza kuzungumzia mgomo wa madaktari baada ya Wakenya kuhoji katika mitandaoni kuhusu kimya cha Upinzani licha ya mamilioni ya Wakenya.
Hata hivyo, Bw Odinga alionekana kuwa vuguvugu huku akisihi Rais William Ruto kukubali kufanya mazungumzo ya madaktari ili kumaliza mvutano uliopo.
Bw Odinga alitoa taarifa hiyo baada ya kikao cha cha Kamati Kuu (NEC) ya ODM iliyokutana kuzungumzia mambo ya uchaguzi.
Bw Odinga ameonekana kujitenga na vinara wenzake wa Azimio la Umoja tangu alipotangaza nia ya kuwania uenyekiti wa AUC.
Hii inatokana na ukweli kwamba Bw Odinga ameamua kuwa kimya ili asimchokoze Rais William Ruto ambaye amekuwa akimfanyia kampeni za uenyekiti wa AUC kote Barani Afrika.
Rais Ruto tayari amezuru mataifa kadhaa yakiwemo, Uganda, Ghana, Congo, Tanzania na mengineyo kupigia debe Bw Odinga.
Alipokuwa nchini Ghana, Rais Ruto alimmiminia Bw Odinga sifa tele huku akisema kuwa atatekeleza vyema ajenda ya AU. Ghana ilikubali kuunga mkono Bw Odinga katika uchaguzi wa AUC utakaofanyika 2025.
Hatua hiyo ya Rais Ruto imemfanya Bw Odinga kufumbia macho maovu kama vile mbolea feki, ripoti za ufisadi na ukabila serikalini, ubomoaji kiholela wa makazi ya raia kupisha ujenzi wa makazi nafuu kati ya mengineyo.
Kinara wa Wiper Kalonzo Musyoka, hata hivyo, ambaye ameunga mkono Bw Odinga kama mwaniaji mwenza katika uchaguzi mkuu wa 2013 na 2017, hana budi kujifunga kibwebwe na kujifisha kilemba cha mkosoaji mkuu wa serikali.
Mapema mwaka huu, Bw Musyoka alitangaza kuwa atakuwa mshindani mkuu wa Rais Ruto katika kinyang’anyiro cha urais 2027.
Bw Musyoka alisema kuwa ni lazima atawania urais 2027 hata kama vinara wenzake wa Azimio watamtoroka.
Ikiwa kweli Bw Musyoka anataka kushinda urais 2027, anafaa kuongoza upinzani na kuvaa viatu vya Bw Odinga ambaye amegeuka kuwa vuguvugu.
Kalonzo anafaa kuwa katika mstari wa mbele kuongoza juhudi za kukosoa serikali kila mara inapoenda mrama. Kukosoa serikali husaidia serikali kuongeza umaarufu wa viongozi wa Upinzani.
Kabla ya Uchaguzi Mkuu wa 2022, Dkt Ruto alijizolea umaarufu kote nchini kutokana na hatua yake ya kukosoa serikali licha ya kuwa naibu wa rais.
Naye Bw Odinga alipoteza umaarufu kwa kuunga mkono serikali licha ya kuwa kiongozi wa upinzani.
Hivyo, Kalonzo hafai kulaza damu bali ajitokeze kukosoa serikali ili kujiongezea umaarufu.