Upinzani usipojanjaruka utayumbishwa na fuko wa serikali
Upinzani wa wakati huu unafaa kujanjaruka. Muda umefika wa kukoma kuwa mwepesi wa kugawanyika na kudhoofishwa kutoka ndani.
Kuna fuko wa serikali wanaojifanya wako kwa ajili ya mabadiliko, lakini kazi yao kubwa ni kusambaratisha upinzani kwa niaba ya wale walio mamlakani. Mimi sio nabii, huu ndio ukweli mchungu ambao huenda wasikubaliane nao hasa fuko wenyewe. Na siwajui hata. Naapa.
Katika nyakati hizi ambapo wananchi wanatafuta matumaini ya kweli kupitia sauti mbadala, ni aibu kwa upinzani kuwa dhaifu kwa sababu ya watu waliopenyezwa, wanaojifanya kuwa wapinzani wa serikali.
Fuko hawa ni hatari kuliko adui anayeonekana. Wanajifanya wangwana, wanakaa meza ya kupanga mikakati, lakini ni wajasusi wa serikali.
Hali hii imeonekana wazi wakati wa maandamano ya Gen Z na matukio ya karibuni ya kisiasa. Badala ya kuonyesha umoja, baadhi ya sauti zilianza kuyumbayumba, wengine walitoa kauli zenye mashaka, wengine walitumia majukwaa ya mitandao kwa njia ya kuchafua wenzao. Ni kazi ya fuko waliopewa maagizo ya kuvuruga kutoka ndani.
Upinzani usipoua hujuma hizi mapema, utasalia kuwa na majina makubwa bila nguvu halisi. Na huo utakuwa ushindi kwa serikali.
Upinzani lazima ujipange, ujisafishe, na ujijenge kwa misingi ya nia safi na umoja wa kweli. Bila hivyo, fuko wataendelea kuwa na ushawishi, na wananchi wataendelea kusalitiwa bila wao kujua.
Upinzani usijipe moyo kwa idadi ya wanachama, bali kwa uthabiti wa nia. Fuko mmoja tu anayevuruga misingi ya mabadiliko ni hatari kubwa.
Huu si wakati wa kuamini kila mtu hata wanaoonekana jasiri na kujitolea kwa dhati, wananeji wa haja. Hao wanaweza kuwa maajenti wa serikali kukusanya habari za kuyumbisha dau la upinzani. Mkizingatia ushauru huu nyinyi wa upinzani wa dhati, mtanishukuru baadaye. Ni hayo kwa sasa.