Wanaotumia urafiki na Rais kumwaamrisha Gachagua, wamelewa mamlaka
Na CECIL ODONGO
NAIBU Rais Rigathi Gachagua wiki jana aliteta kuwa kuna baadhi ya viongozi walio karibu na Rais William Ruto wasiomheshimu serikalini.
Bw Gachagua alikiri kuwa uhusiano wake na baadhi ya wandani wa Rais sio mzuri kwani wanasiasa hao wanatumia urafiki wao na Rais kumtaka afuate amri zao ilhali ni wadogo wake ndani ya utawala huu.
Kwa mujibu wa itifaki, katiba na mfumo wa kuendesha serikali, Bw Gachagua ni kiongozi wa pili mwenye mamlaka ya juu zaidi nchini baada ya Rais Ruto.
Kutokana na hilo, anastahili kufuata tu amri ya Rais lakini anaweza kumshauri bosi wake kuhusu masuala mbalimbali ya usimamizi wa nchi hasa pale anapoona mambo hayaendi sawa.
Inashangaza kuwa sasa kuna baadhi ya wanasiasa wa mrengo wa Kenya Kwanza ambao hawataki kumheshimu Bw Gachagua na wamefanya alalamike kuwa wanataka afuate amri zao.
Ingawa hakuwataja wanasiasa hao hadharani, ni dhahiri kuwa baadhi ya wale ambao wamekuwa wakimshambulia Bw Gachagua hadharani ndio wanahusika na tabia hii.
Kiongozi wa wengi Bungeni Kimani Ichung’wah, Waziri wa Utumishi wa Umma Moses Kuria, mwenzake wa uchukuzi Kipchumba Murkomen, Waziri wa Usalama wa Ndani Profesa Kithure Kindiki na wabunge Oscar Sudi (Kapseret) na Silvanus Osoro ni kati ya viongozi ambao wamekuwa wakimshambulia vikali naibu rais.
Wanasiasa hao wanaohudumu katika nyadhifa muhimu serikalini, wamekuwa wakipinga mfumo wa ugavi wa mapato unaozingatia idadi ya watu ambao umekuwa ukirindimwa na Bw Gachagua.
Baadhi wakionekana kuhamaki, wamekuwa wakimsawiri naibu rais kama anayepigania maslahi ya wakazi wa Mlima Kenya badala ya kujisawiri kama kiongozi wa taifa kutokana na uzito na umuhimu wa wadhifa anaoushikilia.
Ingawa hivyo, ni vyema wanasiasa wanaomdharau Bw Gachagua wabadilike na kumheshimu. Ni vyema Bw Gachagua amezungumzia suala hili hadharani kwa sababu kumechipuka minong’ono kila mara kuwa anasumbuliwa serikalini.
Enzi za kuwa na naibu wa rais ambaye ni kibaraka na babu zimepitwa na wakati kwa sababu serikali siku hizi huundwa kupitia miungano ya kisiasa.
Hata Rais Ruto katika muhula wa pili wa utawala wa Jubilee, alikosana na baadhi ya mawaziri kama Fred Matiang’i na aliyekuwa katibu katika wizara ya usalama wa ndani Karanja Kibicho, aliodai walikuwa wakimtatiza serikalini.
Katika utawala wa Kenya Kwanza, eneo la Mlima Kenya ambako naibu rais ana ushawishi, lilichangia asilimia 47 ya kura zote ambazo Rais Ruto alizipata mnamo 2022.
Kwa hivyo, hii ni serikali ya muungano kati ya Rais na naibu wake na kila mrengo lazima unufaike. Hii dhana kuwa Bw Gachagua hakupaswa kuwa mgombeaji mwenza wa Rais Ruto 2022 na kuwa nafasi hiyo ilistahili kuendea Profesa Kindiki ni hadaa tupu.
Iwapo uongozi wa Kenya Kwanza haukuthamini mchango wa Bw Gachagua na ushawishi wake katika siasa za Mlima Kenya, basi mbona haukumpa tu Profesa Kindiki nafasi hiyo.
Nina hakika kuwa iwapo ni Profesa Kindiki ndiye angekuwa mgombeaji mwenza wa Rais Ruto, basi kura nyingi kutoka eneo la Kati hasa jamii ya Agikuyu zingemwendea Raila Odinga ambaye mgombeaji mwenza wake alikuwa Martha Karua.
Kwa hivyo, Bw Gachagua ana haki ya kutoa maoni yake kuhusiana na masuala yanayoendeshwa na serikali kwa sababu kiuhalisia, yeye na Rais wana mchango sawa katika kubuni utawala huu.
Wandani wa rais hawana mamlaka yoyote ya kumwaamrisha Bw Gachagua kuhusu jambo lolote na badala yake wanastahili kumheshimu na kushauriana naye.
Baadhi ya wanaotishia kuwa naibu rais atatimuliwa kupitia hoja ya kutokuwa na imani na uongozi wake nao wanaota. Tatizo lao ni gere kutokana na wadhifa ambao Bw Gachagua anaushikilia na wanafahamu kuwa juhudi zozote za kumng’atua zitazua ghadhabu kutoka kwa wapigakura wa Mlima Kenya.
Bw Gachagua anastahili heshima hata kutoka kwa wanasiasa ambao ni marafiki wa Rais.