Wasiotaka mazungumzo ya Raila hawaoni mbele
KUNA mwenendo unaoelekea kuzoeleka ambapo baadhi ya viongozi sasa wanamkashifu Kinara wa Upinzani Raila Odinga kama kikwazo cha suluhu kwa masaibu mengi yanayoshuhudiwa nchini.
Hivi majuzi Bw Odinga amekashifiwa kwa kupendekeza mazungumzo yanayoshirikisha vijana kuhusiana na changamoto ambazo zinaendelea kushuhudiwa nchini.
Mazungumzo hayo ambayo Raila anapendekeza yatawashirikisha vijana na kutoa mwongozo aula jinsi ambavyo masuala yao yanaweza kushughulikiwa.
Kwa muda sasa vijana wamekuwa wakiandamana wakilalamikia changamoto mbalimbali nchini wengi wakimshinikiza Rais William Ruto awajibike.
Mazungumzo hayo yatatoa mapendekezo ya kuongeza nafasi ajira, kusawazisha ulipaji wa madeni ya nchi, kupiga jeki sekta ya elimu, uvumbuzi ambao utaongeza nafasi za ajira pamoja, vijana kushirikishwa katika masuala ya uongozi na masuala mengine muhimu.
Aidha, mazungumzo hayo pia yatajikita katika mbinu aula ya kupambana na visa vya utekaji nyara na watu kupotea kiholela pamoja na masuala mengine yatakayochangia maslahi ya vijana kushughulikiwa.
Ukweli ni kwamba masuala ambayo vijana wanayataka hayawezi kutimizwa pasipo mazungumzo. Ndio wameshiriki fujo tangu mwaka jana, lakini matokeo yake yamekuwa maafa, majeraha na makovu.
Kuna wale ambao wanasema kumekuwa na ripoti ya kamati au majopo mbalimbali yaliyowahi kuandaliwa na haya mazungumzo anayoyapendekeza Raila ni kazi bure.
Ukitathmini ripoti hizo, nyingi zilitokana na ghasia za baada ya uchaguzi na zilijikita sana kwenye kuzima wizi wa kura.
Kuna ripoti ya Kriegler ambayo ilijikita sana katika kuboresha mfumo na utaratibu wa kura zetu.
Hata hii ya juzi ya Kamati ya Kitaifa ya Maridhiano (NADCO) ilijikita sana katika kupata suluhu ya kutatua masuala ibuka kama gharama ya maisha, ugavi wa rasilimali na uwazi kwenye kura.
Ukweli ni kwamba hakuna mazungumzo ambayo yamewahi kujikita katika masuala ya vijana pekee na mara nyingi mambo yao huchanganywa na siasa wala hayapewi kipaumbele.
Mazungumzo ambayo Raila anapendekeza yatafaa hasa wakati huu ambapo vijana wamegutuka na wanafahamu haki zao.
Wakati wa kuandaa ripoti za nyuma, masuala ya vijana yamekuwa yakipuuzwa kwa sababu wanachukuliwa kama watu wasiomakinikia upigaji kura na uongozi wa nchi.
Kinaya ni kwamba wale ambao wanapinga mazungumzo haya ya Raila wamekuwa katika siasa kwa kipindi kirefu na wanafahamu kuwa vijana wamepuuzwa.
Kiongozi wa Wiper Kalonzo Musyoka amekuwa katika siasa tangu mapema miaka ya 80 lakini sera zake za uongozi zimewanufaisha vijana kivipi?
Amewapigania kivipi na wapi kiasi kuwa sasa anajifanya malaika?
Ni juzi tu aliyekuwa Naibu Rais Rigathi Gachagua wakati wa maandamano ya baada ya uchaguzi wa 2023, alikuwa ‘akisherehekea’ kupigwa kwa vijana.
Sasa ndiyo huyo amekengeuka akijifanya anawatetea na kuwachochea dhidi ya serikali baada ya kuondolewa tonge mdomoni.
Wasiotaka mazungumzo haya wanafikiria kuwa watatumia ujanja wao kupata kura za Gen Z ila wasikojua ni kuwa hata wao hawatakiwi na vijana hao hao.
Nini kipya, Mabw Gachagua, Kalonzo, Eugene Wamalwa, Justin Muturi, Mukhisa Kituyi, Dkt Fred Matiangí na viongozi wengine wa upinzani watawapa vijana kama wanawachochea wasishiriki mazungumzo?
Hili ndilo tapo la viongozi ambao kivyovyote vile wana nafasi finyu sana ya kupata kura za Gen Z.
Badala ya kuyakataa mazungumzo hayo, vijana wasishiriki, wajikite katika masuala yao pekee kisha washinikize serikali iyatekeleza masuala hayo.
Ikishindikana hapo ndipo sasa watasema serikali haiwajali.