WASONGA: Maandamano sio njia nzuri ya kusukuma serikali ya Kenya Kwanza
NIMEWAHI kufafanua kwenye ukumbi huu kuwa serikali ya Rais William Ruto ina wajibu wa kupunguza gharama ya maisha ili raia wapate afueni mwaka huu wa 2024.
Nilielezea umuhimu wa utawala huu kutalii njia mbadala za kukusanya fedha zaidi za kufadhili ajenda zake badala ya kuwaongezea raia ushuru kila mara.
Kwanza, hatua ya kimsingi zaidi ni kuifanyia marekebisho Sheria ya Fedha ya 2023 ili kuondoa au kupunguza viwango vya ushuru vinavyochangia kupanda kwa gharama ya maisha.
Mifano ya aina hizo za ushuru ni VAT kwa mafuta ni ushuru wa nyumba wa asilimia 1.5 ya mishahara ya Wakenya.
Pili, ni kubinafsisha mashirika ya serikali ambayo yamekosa kupata faida. Mashirika hayo yamekuwa yakikombolewa na serikali kupitia pesa za walipa ushuru miaka nenda miaka rudi.
Njia nyingine ni kuziba mianya ya ufisadi ambayo kwayo serikali hupoteza takribani Sh700 bilioni kila mwaka, kuwaandama matajiri wanaokwepa kulipa ushuru na kuzima ubadhirifu kupitia ziara nyingi zisizo na maana ambazo maafisa wakuu wa serikali hufanya ndani na nje ya nchi.
Leo naugeukia upinzani unaoongozwa na Waziri Mkuu wa zamani Raila Odinga.
Japo, nakubaliana na kauli za kinara huyo wa Azimio la Umoja –One Kenya na wenzake Martha Karua na Kalonzo Musyoka kwamba serikali iliyoko mamlakani ndio yenye wajibu wa kupunguza gharama sichelei kuwaarifu kuwa wao pia wanayo wajibu katika kufikiwa kwa hilo.
Wajibu wao ni kubuni na kuwasilisha mawazo na sera mbadala ambazo serikali inaweza kutekeleza ili kushusha gharama ya maisha.
Baada ya kufanya hivyo, wanaweza kuiwekea serikali presha kupitia Bunge na Idara ya Mahakama badala ya kuitisha maandamano alivyotisha Bw Odinga wiki jana.
Kufikia sasa nilitarajia kuwa Azimio ingekwisha kutayarisha mswada wa kuifanyia marekebisho Sheria ya Fedha ya 2023 kwa kuondoa au kupunguza ushuru kandamizi nilizotaja hapo juu, badala ya kulalamika kila mara.
Baadaye mswada huo uwasilishwe katika Afisi ya Spika wa Bunge la Kitaifa Moses Wetang’ula ili usomwe kwa mara ya kwanza bunge hilo litakaporejelea vikao Februari 15, mwaka huu.
Mswada wenyewe upasa kusheheni mapendekezo mbadala kuhusu namna serikali hii itakavyoweza kupata pesa za kuiwezesha kuendesha mipango yake iliyoko kwenye manifesto ya Kenya Kwanza. Endapo wabunge wa mrengo huo watashurutishwa kuuangusha mswada kama huo, basi Wakenya watakuwa na kila sababu ya kulipiza kisasi debeni 2027.
Pili, Azimio inapaswa kuendelea kutumia mahakama kama jukwaa la kupinga sera na mipango ya serikali hii inayowaumiza raia.
Inaridhisha kuwa mrengo huu wa upinzani tayari imeanza kutumia mbinu hii kupitia kesi kesi ilioko mahakamani ya kupinga ubinafsishaji wa mashirika 11 ya serikali. Kesi hiyo iliwasilishwa na chama cha ODM.
Kesi nyingine ni ile ambayo iliwasilishwa mahakamani na Kiongozi wa Wachache katika Seneti Stewart Madzayo kupinga hatua ya serikali kutoza ada kwa huduma zinazotoa kupitia mtandao wa E-Citizen.
Tasnifu yangu ni kuwa hamna haja kwa Bw Odinga na wenzake kurejelea maandamano kama mbinu ya kuikosoa na kuiwekea presha serikali ya Rais Ruto.
Mbinu hii, imebainika kusababisha maafa na hasara kwa raia na taifa kwa ujumla.
Juzi, kwenye mahojiano na runinga ya Citizen nyumbani Bondo, Bw Odinga alifichua kuwa watu 76 waliuawa wakati wa msururu wa maandamano ya Azimioa ya kulalamikia kupanda kwa gharama ya maisha mapema mwaka jana.
Isitoshe, maelfu ya watu wengine walijeruhiwa, huku mali ya thamani kubwa ikiharibiwa.
Waliojeruhiwa vibaya sasa wamelemaa na hawawezi kutoa mchango wowote kwa ustawi wa nchi hii walivyofanya zamani.