Habari za Kitaifa

Masaibu ya wafanyakazi wa KCC ambao wamefuatilia malipo yao kwa miaka 27

Na MARY WANGARI August 30th, 2024 2 min read

WAAJIRIWA wa shirika la KCC lililovunjiliwa mbali waliofutwa kazi zaidi ya miaka 26 iliyopita, watalazimika kuendelea kusubiri malipo ya marupurupu yao na fedha walizoweka akiba katika shirika la Maziwa Sacco.

Wafanyakazi hao waliwasilisha malalamishi kwa Bunge la Seneti mwezi uliopita, Julai 9, 2024, baada ya juhudi za kufuatilia hela zao kwa karibu miongo mitatu, kugonga mwamba.

Walifutwa kazi 1997 baada ya serikali kukosa kulipa deni la fedha zilizotumika kufadhili mpango wa kuwapa maziwa watoto wa shule za msingi katika miaka ya 1990.

Licha ya misururu ya maamuzi ya korti, wafanyakazi hao walipata pigo kubwa 2020, baada ya korti ya rufaa kufutilia mbali uamuzi wa Mahakama Kuu uliosema New KCC ilipaswa kuwajibikia malipo yao.

Mvutano huo wa muda mrefu ulikumbwa na kizingiti kingine Alhamisi, Agosti 29, 2024 baada ya usimamizi wa New KCC kukaidi kwa mara nyingine, mwaliko wa Seneti kwa lengo la kutatua suala hilo na kuilazimu Kamati ya Seneti kuhusu Leba kutoa mwaliko mwingine.

Seneta Mteule George Mbugua ambaye ni Naibu Mwenyekiti wa Kamati hiyo, alisema mwaliko mpya utaambatana na masharti makali yatakayoagiza New KCC kuwasilisha sajili inayoorodhesha mali iliyotwaliwa kutoka kwa KCC ya zamani, mali ya sasa ya New KCC na hali ya mali hiyo kwa sasa.

“Kwa kuzingatia muda uliwekwa wa kukamilisha vikao vya kusikiza malalamishi yaliyowasilishwa kwa Seneti, tunahitaji kufikiria mbele iwapo tutahitajika kuagiza New KCC kuuza baadhi ya mali yake ili kulipa pesa inazodaiwa,” alisema Seneta Mbugua.

Kanuni za Bunge la Seneti nambari 238(2) inasisitiza kuwa malalamishi yoyote yaliyowasilishwa mbele ya Kamati ni sharti yawe na ripoti iliyowasilishwa kwa Seneti katika muda wa siku 60 kuanzia tarehe ya kusoma ombi husika.

Huku muda ukizidi kuyoyoma, Kamati hiyo iliafikiana kumwalika tena Mshauri Mkuu wa serikali na mawaziri wa vyama vya ushirika, Leba na Hazina ya Kitaifa, waliosusia kikao cha Alhamisi hatua iliyoibua shutuma kali kutoka kwa maseneta.

“Walalamishi walisafiri masafa marefu kuhudhuria kikao hiki kisha tunaosaka majibu kutoka kwao wakakosa kujitokeza. Wanapaswa kushurutishwa wawarejeshee pesa walizotumia walalamishi wanaotafuta haki,” alihoji Seneta Mteule Miraj Hassan.

Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Seneta wa Pokot Magharibi, Julius Murgor vilevile alimwagiza wakili Namada Simoni, kuwasilisha orodha ya waajiriwa wa zamani wa KCC anaowakilisha ili kufafanua idadi ya wahusika katika kesi hii.

“Kamati hii inasimamia haki na tutasimama na wafanyakazi wa zamani kuhakikisha wamepokea makato yao ya Sacco na marupurupu wanayodai,” alisema Seneta Murgor.