Habari za Kitaifa

Mashahidi wadai Mackenzie aliwahadaa kwa ardhi za Sh3,000

Na BRIAN OCHARO July 10th, 2024 2 min read

MASHAHIDI katika kesi ya mauaji ya Shakahola dhidi ya mhubiri mwenye utata Paul Mackenzie na washukiwa wenzake 93 wamesimulia jinsi alivyowahadaa kwa kuwauzia ardhi bei rahisi na baadaye kugundua kuwa alikuwa akianzisha ‘ufalme’ wa kikatili.

Katika kesi ya mashtaka yanayohusiana na ugaidi iliyoanza Jumatatu, mashahidi ambao utambulisho wao unalindwa na serikali waliieleza mahakama kuwa, washtakiwa walikuwa kama shirika la uhalifu lililojipanga vyema kupitia kwa kanisa chini ya uongozi wa Mackenzie.

Mahakama ilielezwa kuwa lengo lao mahususi lilikuwa ni kukiuka haki ya kuishi, ambayo ni haki ya msingi na takatifu inayolindwa na sheria.

Mahakama iliambiwa kuwa washtakiwa walifanikisha hilo kupitia udhibiti madhubuti wa shughuli za kundi hilo ambazo zilifanyika katika eneo lililotengwa la msitu wa Shakahola.

Kulingana na mashahidi wa serikali, Mackenzie alinunua ardhi katika eneo la Shakahola na kuhamia huko mnamo 2020.

Kupitia kundi la WhatsApp, Mackenzie anadaiwa kuwataka waumini wa kanisa hilo kuungana naye na kuishi katika msitu wa Shakahola.

Waumini hao walitakiwa kununua sehemu za ardhi kutoka kwake kwa bei nafuu kuanzia Sh3,000.

Wanunuzi walifanya malipo kwa Mackenzie kupitia M-Pesa au kwa pesa taslimu. Kwa kiasi kidogo cha Sh3,000 mtu angeweza kupata ekari mbili za ardhi.

Baada ya kununua vipande hivyo vya ardhi, wafuasi wa dhehebu lake kisha walijenga nyumba zilizoezekwa kwa udongo na paa za makuti, zenye vyumba viwili na sebule.

“Nilihamia msituni na familia yangu mnamo 2022 na kukaa huko. Nilianza kuona tabia na sheria zisizo za kawaida za kimaisha baada ya kukaa huko kwa muda,” shahidi aliarifu mahakama.

Ndani ya msitu huo unaojulikana mahakamani kwa jina la Kwa Mackenzie, ilidaiwa kuwa mafundisho ya Mackenzie yalikatisha tamaa watu kujilimbikizia mali, huku pia akichochea kukataliwa kwa mamlaka ya serikali, hasa katika masuala yanayohusu elimu ya watoto na afya.

Mackenzie alitekeleza imani yake kwa kuwakataza watoto kuhudhuria shule, kuzuia mwingiliano kati ya majirani, na kukataza kushiriki rasilimali au kutafuta msaada kutoka kwa mtu mwingine.

Wafuasi wa dhehebu waliotamani kujihusisha na kilimo na ufugaji walikatishwa tamaa kwani Mackenzie alidaiwa kupiga marufuku ufugaji na majaribio yoyote ya ustawi ndani ya jamii.

Mikutano iliandaliwa ili kuwahutubia wakazi, huku matangazo yakitolewa kwa wafuasi na wajumbe wakuu wa ‘baraza la mawaziri’, wakiongozwa na mtu aliyejulikana kwa jina la Paulo, ambaye alikuwa msimamizi wa ratiba za mikutano na kusimamia masuala ya mahali palipojulikana kama Galilaya ndani ya msitu.

Kando na Galilaya, msitu huo ulikuwa na maeneo mengine yenye majina ya Kibiblia kama vile Bethlehemu, Yudea miongoni mwa maeneo mengine.

“Mimi binafsi nilihudhuria mikutano miwili kama hiyo iliyofanywa karibu na Bethlehemu na Yudea, chini ya Mti wa Mitora karibu na makazi ya James,” shahidi mmoja alisimulia.

Wanawake na wanaume walikaa pande tofauti, mke wa Mackenzie, Rhoda Mumbua Maweu aliyefahamika kwa jina la mke wa Mchungaji akiwa ule upande wa wanawake.

Kwa upande wa wanaume, karibu viti 10 vilipangwa, huku Mackenzie akiwa mbele ya waumini, akiwa amezungukwa na ‘baraza la mawaziri’, akiwemo Evans Sila, Smart Nderi Mwakalama, Stephen Muye Alias Steve, Katana wa Julia, miongoni mwa wengine.