MASHAIRI YA JUMAMOSI: Hodi hodi Mombasa
Hodi hodi wasafiri, twakushukuru muumba,
Sifa ni zako kahari, wengine wanajikomba,
Umetuvusha bahari, mabonde milima myamba,
Hodi hodi wa Mombasa, Uwape tumeingia.
Hodi hodi tunabisha kwa kheri, kukaribishwa twaomba,
Umoja wa washairi uwape kutoka Pemba,
Zanzibar ni shuwari, kwetu hakuna mbambamba,
Hodi hodi wa Mombasa, Uwape tumeingia.
Hodi hodi tumekuja kuja kuwatembelea,
Mukiona ipo haja kwetu karibuni pia,
Tuimarishe umoja kwenye hii tasnia,
Hodi hodi wa Mombasa, Uwape tumeingia.
Hodi Malindi ya Kenya, Nairobi na Mombasa,
Ziara tumeifanya, lengo lake kubwa hasa,
Kwenu tujifunze chanya, tufute yetu makosa,
Hodi hodi wa Mombasa, Uwape tumeingia.
Hodi hodi tunotoa ifike mpaka lamu,
Tumekuja kuwajua, magwiji na waalimu,
Wakina Sheikh Pasua, na wenginewe muhimu,
Hodi hodi wa Mombasa, Uwape tumeingia.
Hodi twahodisha kwenu Uwape tu wanagenzi,
Twasifia tungo zenu wenzetu muwabobezi,
Kuifika levo yenu twahitani wakufunzi,
Hodi hodi wa Mombasa, Uwape tumeingia.
Hodi hodi twawasihi, Wakenya tafadhalini,
Tufundisheni fasihi, ya maudhui na fani,
Ikisiri islahi, tuzijue na matini,
Hodi hodi wa Mombasa, uwape tumeingia.
Beti saba zinatosha, iwe mwisho hodi yetu
Isije ikawachosha ikawakimbiza watu,
Sasa twajitambulisha mbele ya wenyeji wetu,
Hodi hodi wa Mombasa, Uwape tumeingia.
Kwa faida ya hadhira, nyote mulo hudhuria,
Namleta baba Sara, aje kuwasalimia,
Mtunzi wa kazi bora, hii munoisikia,
Hodi hodi wa Mombasa, Uwape tumeingia.
SHEHA SULEIMAN JUMA
BABA SARA – UWAPE
MKANYAGENI
Wanazuo someni
Wanazuo vitivoni, someni muwe wajuzi,
Ujuzi na umakini, yawapasa kumaizi,
Tajiriba iyakini, ndo muwe wachapakazi,
Wanazuo msomeni, mpate tele ujuzi.
Jikazeni kisabuni, uvumbuzi kuasisi,
Sisomee mtihani, pasiponi umilisi,
Tajiriba tafuteni, ili muwe maharishi,
Wanazuo msomeni, mpate tele ujuzi.
Leo kisomo chuoni, jaribu kuwa makini,
Tafukuri upeoni, ni lazima darasani,
Masuali yazueni, utafiti kufanyani,
Wanazuo msomeni, mpate tele ujuzi.
Mahaba yalo chuoni, yasiwape hamnazo,
Ni mapenzi ya utani, yalosheheni machezo,
Hayadumu asilani, ni kama yako likizo,
Wanazuo msomeni, mpate tele ujuzi.
Tazama kwenu nyumbani, ubadili hino hali,
Usijigambe chuoni, ukahisi wewe nguli,
Maadili mvaeni, nyendo zenu kuadili,
Wanazuo msomeni, mpate tele ujuzi.
EDWARD LOKIDOR
“BALOZI WA KISWAHILI, TURKANA”
CHUO KIKUU KISHIRIKISHI CHA TURKANA
Harusi ya heri
Kwa jina lake Kahari, muumba vyote Latifu,
Maana ndiye jabari, asiye na mapungufu,
Mjalie dakitari, ndoaye kikamilifu,
Harusi iwe ya heri, ndugu Abdullatifu.
Chaguo lililo zuri, kwa twabia nalisifu,
Kwa penzi lililo shwari, mpe mke pasi hofu,
Ndoa isitiwe shari, kujazwa na usumbufu,
Harusi iwe ya heri, ndugu Abdullatifu.
Pendo lisiwe la siri, kwa mazuri umsifu,
Kwa uwezo wa kadiri, shingo mvishe mkufu,
Nd’o apendeze vizuri, pasi na kumkashifu,
Harusi iwe ya heri, ndugu Abdullatifu.
Wavyele wako wazuri, ukamjua Latifu,
Dini ‘mesoma vizuri, kwenye hii tasnifu,
Ukaielewa shwari, kaka Abdullatifu,
Harusi iwe ya heri, ndugu Abdullatifu.
Twakuonea fahari, ndugu zako twakusifu,
Fathi, Adamu ni heri, wakupenda pasi hofu,
Mohamedi ni jasiri, mdogo kwa tawasifu,
Harusi iwe ya heri, ndugu Abdullatifu.
Baba yuko kwa Kahari, muumba mbingu Latifu,
Dhambi zote za kaburi, amswamehe Latifu,
Mola amwepushe shari, mja si mkamilifu,
Harusi iwe ya heri, ndugu Abdullatifu.
Nakusihi dakitari, ndoa linda ja sarafu,
Usipatwe na habari, za kukutia upofu,
Penzi utie shubiri, ulimwage kwenye safu,
Harusi iwe ya heri, ndugu Abdullatifu.
EDISON WANGA,
SON BIN EDI,
MWANA WA MAMBASA,
MOMBASA
Usihamaki Rais
Kama kweli takosea, naomba radhi mapema,
Mabaya kiniwazia, hizo ni zako lawama,
Kwa jinsi uliongea, nilibaki kutazama,
Raisi usihamaki, ni sisi likuchagua,
Kwa kuwa tulikwamini, tukakupa kura zetu,
Lijua tatudhamini, tukitoa hoja zetu,
Hatimaye ‘meamini, kumbe wewe si mwenzetu,
Raisi usihamaki, ni sisi likuchagua.
Kwa kuwa ‘likuchagua, mambo yetu sikiliza,
Kwa wema tukikwambia, uchumi huu punguza,
Lisije kukuzingua, na hasira kukujaza,
Raisi sihamaki, ni sisi likuchagua.
Hata mambo ya Adani, ni kweli tulikataa,
Tukakweleza kindani, puresha ikakujaa,
Ukasema mashetani, hadharani ‘kakemea,
Raisi usihamaki, ni sisi likuchagua.
Na Sadaka kanisani, si kwamba tumekataa,
Ni kweli twaidhamini, ila wengi wanalia,
Hawanacho cha dhamani, cha tumboni kukitia,
Raisi usihamaki, ni sisi likuchagua.
Kile tunacho manisha, tuwajali masikini,
Shida zao zikiisha, ndipo tuje kanisani,
Sadaka kulainisha, na zawadi za hisani,
Raisi usihamaki, ni sisi likuchagua.
Shairi naliandika, litundikwe gazetini,
Najua kwako ‘tafika, ulisome kwa makini,
Kwenye vyombo ukifika, zikutoke samahani,
Raisi usihamaki, ni sisi likuchagua.
MWALIMU SIKUJUA
MALENGA WA KANISANI
MATUNDA- MOIS BRIDGE
Siku ya Jamhuri
Desemba kumi na mbili, kumbukumbu ya uhuru,
Mashujaa kukabili, na kushinda wa beberu,
Walishika na wawili, ndipo tupate uhuru,
Twafurahi Jamhuri, kupata uhuru wetu.
Mkoloni katutesa, huku atuita nyani,
Kisha akuza anasa, atutia gerezani,
Wakenya awanyanyasa, awatia mashakani,
Twafurahi Jamhuri,kupata uhuru wetu.
Heko kwenu mashujaa, kuwan’goa wakoloni,
Neema iliwajaa, kutoka kwake Rabani,
Bendera yatu kupaa, Kenya uhuru jamani,
Twafurahi Jamhuri, kupata uhuru wetu.
Na mateso kukithiri, mashujaa hajitoa,
Kwa moyo kujipa ari taifa kulikomboa,
Ni bora kufa kafiri,na nchi kuikomboa,
Twafurahi Jamhuri,kupata uhuru wetu.
Mashujaa kupigana, na mateso kuteseka,
Ndiyo mana twajivuna, mkoloni kutoweka,
Hakika wamepigana, hatimaye wakatoka,
Twafurahi Jamhuri, kupata uhuru wetu.
Voongozi wetu Raisi, tano idadi kufika,
Jomo wa kwanza Rais, Moi wa Nyayo kufika,
Mwai fanaka Raisi, nne Uhuru kafika,
Twafurahi Jamhuri, kupata uhuru wetu.
Wa tano Raisi Ruto, kwako kunatumaini,
Ututoe kwenye moto, maisha juu jamani,
Busara unazo Ruto, twakuombea Manani,
Twafurahi Jamhuri, kupata Uhuru wetu.
JAMES OBIERO
MTOTO WA MAMA
KAKAMEGA, SHIKHAMBI