Mashairi

MASHAIRI YETU: Buriani Raila

October 22nd, 2025 Kusoma ni dakika: 1

Jemedari wa mageuzi, tulomuenzi Tinga,
Wa siasa za uwazi,Agwambo tukampanga,
Ni huzuni na majonzi,wakenya tunamuaga,
Buriani Raila Odinga, Baba wa demokrasia.

Ulionja kizuizi,mateso kubwa gharama ,
Kinayahe mtetezi,vyama vingi kusimama,
Ulipambana mjuzi,halaiki kuandama,
Buriani Raila Odinga,Baba lala salimini

Mwanzilishi ugatuzi,kuteteya wetu Jimbi,
Makabwela wakaenzi,ustawi siuambi,
Barabara kwa ujuzi,baipasi tumbitumbi,
Buriani Raila Odinga,lala salama Kinara.

Historiya ya Kenya,ukurasa lifunguwa,
Ya demokrasi kupenya,tukawa mbele kifuwa,
Hili hukulikanganya,wajibuo sawasawa,
Buriani Jemedari,Agwambo tunakuaga

Ulipenda maandamano,walipoasi ya haki,
Tiyagasi na maneno,vitisho hukushiriki,
Halaiki na hayano,kakupenda mstahiki,
Buriani Baba Raila,Wakenya tutakukosa.

Nyingi zako handisheki,kitafuta uwiano,
Na Amani kuhakiki,kuleta maridhiano,
Uchumi tukaafiki,chaguzi zake maneno,
Hakika tutakukumbuka,Kipenza Raila Amolo.

Buriani Baba buriani,ni kipindi cha mpito,
Paziya i sakafuni,Shujaa wa nyingi mito,

Si jamhuri si barani,wakenya waihisi joto,
Ela lala salama Agwambo,Simba aliyenguruma!

Safari ya mwisho India,likopata matibabu,
Habari zilipowadia,za tanziya sababu,
Vyombo vinanadia,za kifo wote kutubu,
Kwaheri Waziri Mkuu,Baba tuliyekuenzi!

Kaditama rambirambi,za jasiri mtetezi,
Hakika leo siimbi ,ya galacha na mjuzi,
Jogoo na wetu jimbi,meteleza yetu ngazi,
Kwaheri Baba Kwaheri,Mola akulaze pema.

YITZHAK MWAGO
MSOMI- MTALII
KARATINA,NYERI.