USHAIRI: TUKOSOENI TUKIKOSEA
Washairi wa zamani, mloanza mbele yetu,
Nawaomba samahani, mzisome tungo zetu,
Kwa makini zisomeni, nyinyi ndio mboni zetu,
Muonapo twakosea, tafadhali tukosoe.
Kina Muchai Hasani, na Thomasi Kosgei,
Mimi namheshimuni, ndio ma’na nawarai,
Hukumu kwetu toeni, kama tungo hazifai,
Samahani mkiona, twakosea tukosoe.
Kunao mitandaoni, washairi ainati,
Tungo zao za kubuni, hazieleweki ati,
Huenda si hatuoni, tunapitisha wakati,
Muonapo twakosea, tafadhali tukosoe.
Nyamosi, Obwocha Dani, na Chotara Mswahili,
Nawaomba jongeeni, mniunge jimbo hili,
Mwanasarifu Mu’mini, sikusahau kwa kweli,
Muonapo twakosea, tafadhali tukosoe.
Beti mzipitieni, muone tunapofeli,
Mhesabu na mizani, kama kweli ni kamili,
Vina vya nje na ndani, vyote viwe ‘weli weli’,
Muonapo twakosea, tafadhali tukosoe.
Ikiweza sikieni, mashairi tunoghani,
Yachambue hadharani, mtambue kiini,
Bwa Ngatia wambieni, watufae jamani,
Kama kweli twakosea, tafadhali tukosoe.
Mwisho naweka riboni, nimefika ukingoni,
Watangulizi nawaombeni, tungo zetu zisomeni,
Ili tunapokoseni, na moyo mtutieni,
Muonapo twakosea, tafadhali tukosoe.
Mtunzi: Abuthwalib Lukungu,
Abu Malenga Mkalitusi,
Chuo Kikuu cha Rongo (CHAWAKIRO)