Mashairi

MASHAIRI YETU: Mti umeshaanguka

October 22nd, 2025 Kusoma ni dakika: 4

Mtima unaumia, mti umeshaanguka,
Habari metufikia, za Raila kututoka,
Nani wa kutuambia, kwamba halija tendeka?
Mti umeshaanguka, ameshalala Odinga.

Kulikucha Jumatano, kama siku kawaida,
Ikafika saa hino, kwamba kifo metuponda,
Kimetwaa wa maono, kikatuachia shida,
Mti umeshaanguka, ameshalala Odinga.

Alikuwa kweli mtu, mwingi wa mema maono,
Alisheheni na utu, pamwe na uelewano,
Alijali wote watu, nchini kwa mapatano,
Mti umeshaanguka, ameshalala Raila.

Kote aliwatetea, wakubwa hata wadogo,
Masikini walikwea, sauti iso kidogo,
Nao wale milionea, kwake aliwapa gogo,
Mti umeshaanguka, ameshalala Raila.

Kotekote duniani, walimjua Raila,
Hakufika ikuluni, alileta mjadala,
Aliongoka yakini, kwayo sauti aula,
Mti umeshaanguka, ameshalala Raila.

Atakumbukwa daima, kwa uongozi jasiri,
Aliyoyatenda mema, na mazuri yenye heri,
Lini kifo utakoma, kutuletea shubiri,
Mti umeshaanguka, ameshalala Raila.

Lala Raila Odinga, siku yako imefika,
Umetangulia Tinga, baba wa wakenya fika,
Ya Mola hatutapinga, ila tunasononeka,
Mti umeshaanguka, ameshalala Raila.

WANJOHI. P. MUGAMBI
MALENGA KITUNGUU MACHONI

Mgumo watetereka

Malenga ulingo ‘fika, kuwajuza kwa kulumba,
Mgumo umeteguka, manyuni waimbaimba,
Kila Kona ni mashaka, wapasuka na msamba,
Mgumo watetereka, manyuni wayumbayumba.

Awali ulisifika, mgumo kwima ja mwamba,
Kwa matunda kusifika,nyuni kuezeka nyumba,
Kwa sasa metetereka, manyuni walumbalumba,
Mgumo watetereka, manyuni wayumbayumba.

Hasidi waliiteka, mgumo kuweka vumba,
Mti huno kuizunguka, mzizi wakaichimba,
Kwa sasa metetereka, nyuni kote wanatamba,
Mgumo watetereka, manyuni wayumbayumba.

Tambiko meshafanyika, wazee kwake muumba,
Utata hukutatuka, japo walivuta kamba,
Wakongwe wamesumbuka, masaibu mewakumba,
Mgumo watetereka, manyuni wayumbayumba.

Kuna waja wana shoka, mti huno kuuchimba,
Wako ange kutoroka, ndio asali kuiramba,
Wajali kulalamika, manyuni kuyumbayumba,
Mgumo watetereka, manyuni wayumbayumba.

Ni fumbo umefumbika,mewajuza kwa kulumba,
Hadhari kunusurika,wavaa ngozi ya mamba,
Msije kuthirika,na mawi yakawatinga,
Mgumo watetereka, manyuni wayumbayumba.

AGGREY JUMA
MALENGA WA NYIKA
NASOKOL GIRLS – KAPENGURIA

Raila hayu nasi

Mbogholi nasema basi, kama siku zimefika
Ni amri ya Kudusi, duniani kuondoka
Tuliosalia nasi, siku zinahesabika
Pumzika kwa amani, Baba Raila Odinga.

La kufanya hatuoni, sababu umeshaenda
Huko nasi duniani, haki zetu kuzilinda
Umetangulia kwani, Mola wetu kakupenda
Pumzika kwa amani, Baba Raila Odinga.

Umeondoka Raila, umetwacha vinywa wazi
Kinatushinda chakula, twatafuna hatumezi
Na usingizi kulala, kitandani hatuwezi
Pumzika kwa amani, Baba Raila Odinga.

Kinauma kinachoma, kifo chako mbele yetu
Miili inazizima, wala haihisi kitu
Ni matumbo kutetema, kama yamengia kutu
Pumzika kwa amani, Baba Raila Odinga.

Wakenya twaweweseka, miguu haisimami
Mwili wako kuuzika, haki ya mungu sisemi
Moyoni naungulika, nahisi kama uvumi
Pumzika kwa amani, Baba Raila Odinga.

Ukungu tele machoni, twalia twasononeka
Sijui tufanye nini, yatuumiza mashaka
RAILA hatukuoni, kwa kweli tunaumbuka
Pumzika kwa amani, Baba Raila Odinga.

Wala hatujielewi, wafuasi matabaka
Hivi hatujitambuwi, sababu umeondoka
Watuumiza uziwi, ila baba pumzika
Pumzika kwa amani, Baba Raila Odinga.

LUDOVICK MBOGHOLI
AL – USTADH – LUQMAN
NGARIBA MLUMBI
TAITA TAVETA

Umetuwacha vibaya

Kwenye himaya ya fisi, pekeyetu bila baba,
Hatuna hata hirisi, ni hofu imetukaba,
Ni minofu sasa sisi, tunatia mikataba,
Umetuwacha vibaya, Baba Raila Odinga.

Ta’rifa za pantosha, moyoni wamenipanda,
Ninayavuna pankwisha, jisitiri menishinda,
Nikiwaza ninakwisha, eti baba umeenda,
Umetuwacha vibaya, Baba Raila Odinga.

Moyoni nafilisika, ya leo yanifilisi,
Mkota wa kuyambuka, faida yangu mikosi,
Kigwagu nasawijika, natandikwa na mapisi,
Umetuwacha vibaya, Baba Raila Odinga.

Jana inaniuliza, taishije hiyo kesho,
Inazidi niumiza, inasema nipo mwisho,
Tena inasisitiza, bila wewe hitimisho,
Umetuwacha vibaya, Baba Raila Odinga.

Chenge mimi najitoa, mezani pa ushairi,
Ninateswa na hisia, japo nyingi misitari,
Lala pema nakwombea, penye wema na wazuri,.
Umetuwacha vibaya, Baba Raila Odinga

ALLAN CHENGE,
KIJIJI CHA KABKARA

Shujaa wetu Raila

Kifo hakina huruma, kimeshatikisa mwamba,
Kifo huzima uzima, umerudi kwa Muumba,
Duniani umehama, ‘metwaa aliyeumba,
Shujaa wetu Raila, daima utakumbukwa.

Mti mkuu umegwa, twayumba wana wa nyuni,
Na kipigo tumepigwa, imetawala huzuni,
Akili tumevurugwa, kifo huoni tu soni
Shujaa wetu Raila, daima utakumbukwa.

Ni mengi uliyafanya, pumzika kwa amani,

Mzaleendo Mkenya, kuonyesha hadharani,
Tena kuziba mianya, kujulikana nchini,
Shujaa wetu Raila , daima utakumbukwa.

Ulipigania nchi, vyama vingi tukapata,
Kutetea mwananchi, katiba tukaipata,
Inaomboleza nchi, ni wapi tutakupata,
Shujaa wetu Raila , daima utakumbukwa.

Mtetezi wa Taifa, tutakukosa daima,
Nani ataziba ufa, makiwa kwa chetu chama,
Mpaka kimataifa, ulitwakilisha vyema,
Shujaa wetu Raila , daima utakumbukwa.

Tukapata ugatuzi, tutakusahau vipi?
Na wa siasa mzizi, sijaligusia lipi?
Ulikuwa kiongozi, mwingine tupate wapi?
Shujaa wetu Raila , daima utakumbukwa.

Umetuacha yatima, siasa itakuwaje
Upweke unatuvuma, taifa tutakuwaje,
Nawazia chetu chama, uongozi utakwaje
Shujaa wetu Raila , daima utakumbukwa.

Nawaza kupiga kura, nani nitampigia,
Kwa miaka yote kura, yangu nilimpigia,
Kifo mbona unakera, unatufanya twalia,
Shujaa wetu Raila, daima utakumbukwa.

LILIAN ALIVIDZA,
MALKIA WA NYIKANI,
KAKAMEGA

Buriani Baba

Oktoba kumi na tano, Kenya katanda huzuni,
Mzalendo wa maono, amegura duniani,
Taigwa kama mfano, puumzika kwa amani,
Kwaheri bingwa Odinga, Kenya yetu imefiwa.

Uhuru wa vyama vingi, nguli alipigania,
Sifa zake zilivuma, taifa lamlilia,
Mshumaa umezima, mbona umetukimbia?
Kwaheri bingwa Odinga, Kenya yetu imefiwa

Waziri mkuu msta’fu, siasa kapanda ngazi,
Kiongozi maarufu, hodari mchapakazi,
Ataigwa kwa wasifu, aila ifutwe chozi,
Kwaheri bingwa Odinga, Kenya yetu imefiwa

Bingwa wetu mtetezi, wa haki za binadamu,
Aliwajali wakazi, na kufadhili elimu,
Mwanasiasa mzazi, historia atadumu,
Kwaheri bingwa Odinga, Kenya yetu imefiwa

Nafariji familia, Mola wape utulivu,
Ndugu Oburu vumilia, aila mpate nguvu,
“Pawa” imeniishia, muwe wastahimilivu,
Kwaheri bingwa Odinga, Kenya yetu imefiwa

RAPHAEL MUGI(TUJU)
CHUO KIKUU CHA MURANG’A

Kwaheri baba Odinga

Raila ametuacha, duniani ‘meondoka,
Huzuni ngumu kuficha, machozi yanatutoka,
Tumebaki nazo picha, za ukombozi hakika,
Kwaheri Baba Odinga, lala pema pa shujaa.

Shujaa ulosimama, kupigania ya haki,
Wanyonge ulijituma, kuwatoa kwenye dhiki,
Mshumaa umezima, yakulia halaiki,
Kwaheri Baba Odinga, lala pema pa shujaa.

Wako wapi wapinzani, wenye nguvu kama zako?
Ulikuwa namba wani, kuwafichua mafuko,
Sasa hupo duniani, na kama wewe hayuko,
Kwaheri Baba Odinga, lala pema pa shujaa.

Umemrithisha nani? Ushujaa wako nchini,
Umemrithisha nani? Ucheshi wa siasani,
Umemrithisha nani? Uzalendowo jamani,
Kwaheri Baba Odinga, lala pema pa shujaa.

Kalamu ‘mekuwa nzito, naomba hapa kukoma,
Machozi yajaa mato, sioni tena nakoma,
Utakumbukwa mzito, kwa mema yako daima,
Kwaheri Baba Odinga, lala pema pa shujaa.

CHRISTOPHER MUSA KALUNDA
MALENGA MWEPESI
AIC VISA OSHWAL-KABARNET
BARINGO