USHAIRI WENU: Unagongewa!
Mwanangu nakupigia, ni mamako kijijini,
Sababu nakuambia, mambo si mema nyumbani,
Nasema mwenzio dia, karudi tena sokoni!
Jamani rudi nyumbani, mwanangu unagongewa!
Ukiwa huko Malindi, maliyo yashangiliwa,
Ajapo leo Muhindi, asaliyo ajigawa,
Nimeona mengi kundi, mamako nimepagawa!
Jamani rudi nyumbani, mwanangu unagongewa!
Unapotua usiku, kwake naye ni mchana,
Amejigeuza kuku, chumbani hatuwi tena,
Ninayoyaona huku, mwanangu yasinya sana,
Jamani rudi nyumbani, mwanangu unagongewa!
Kugongewa ni lazima, lakini hino mezidi,
Kama mama yaniuma, mkeo ndiye hasidi,
Mwana tena ninasema, usinywe hino likwidi,
Jamani rudi nyumbani, mwanangu unagongewa!
Inazima yangu simu, yabidi nikome miye,
Mwanangu haya fahamu, mke wako tena siye,
Tayari anayo sumu, mtazame tena yeye,
Jamani rudi nyumbani, mwanangu unagongewa!
DOMIANO ADIBA ONYANGO.
MALENGA ADIBA JINA KUBWA.
BUDALANGI, BUSIA
Mirumbe nimehitimu!
Naanza Bismillahi, kwa jina lake Jalia,
Alhamdulilahi, siku leo mewadia,
Sisi sote twafurahi, Rabana katujalia
Nashukuru Mkawini, Mirumbe nimehitimu!
Chereko leo chereko, Mirumbe natabasamu,
Chereko najipa heko, dua naitakadamu,
Nachanua kwa kicheko, Mirumbe nimehitimu,
Nashukuru Maulana, Mirumbe nimehitimu!
Kila refu lina ncha, japo elimu bahari,
Kwa jino hata ukucha, nimekua jemedari,
Mapozi napiga picha, kumbukumbu ya safari,
Nashukuru Rahmani, Mirumbe nimehitimu!
Nawashukuru wazazi, ndugu zangu na jamaa,
Kujituma waziwazi, mnione nikipaa,
Mola awape mbawazi, hakika mlinifaa,
Nashukuru Maulana, Mirumbe nimehitimu!
Nanyi siwaweki kando, wahadhiri wajanjuzi,
Somo lenu kama jando, limevuvia ujuzi,
Wino huno wa upendo, na thawabu za Mwenyezi,
Namshukuru Wadudi, Mirumbe nimehitimu!
Tamati nakata wino, kuyamaliza muhali,
Kichwa hadi kisigino, maleba yapamba mwili,
Bendi zapigwa piano, na mahadhi yakubali,
Nashukuru Maulana, Babu miye nimefuzu!
MIRUMBE P NICKSON
“USTADHI BABU KIJANA”
Siku itafika
Siku moja itafika, milango itafunguka,
Ije mvua ya masika, tuendako tutafika,
Kudura zake Rabuka, juu yetu zitashuka,
Hiyo ndiyo siku moja, tutakayofanikiwa.
Siku moja itafika, njaa itatutoroka,
Na vyakula vitalika, pia vinywaji kunyweka,
Ima siku ikifika, hasidi taaibika,
Hiyo ndiyo siku moja, tutakayofanikiwa.
Siku moja itafika, lawama zitasitika,
Na kero zitaondoka, kubezwa kutapunguka,
Hiyo siku ikifika, kwa wazi tutasifika,
Hiyo ndiyo siku moja, tutakayofanikiwa.
Siku moja itafika, tutakuwa watukuka,
Tukishapata baraka, kotekote tutawika,
Mkono wake Rabuka, utatugusa hakika,
Hiyo ndiyo siku moja, tutakayofanikiwa.
Siku moja itafika, jua kutwa litawaka,
Wenzi wetu watacheka, nyuso hazitavimbika,
Majukwaa wataweka, ili sisi kusikika,
Hiyo ndiyo siku moja, tutakayofanikiwa.
Siku moja itafika, hata mwisho napofika,
Hili nalo nahakika, walokesha kutucheka,
Wakiijenga mipaka, kikomoni watafika
Hiyo ndiyo siku moja, tutakayofanikiwa
ABUTHWALIB LUKUNGU
ABU MALENGA MKALITUSI
CHUO KIKUU CHA RONGO, CHAWAKIRO
Wanawake wasidhulumiwe
Malenga natanguliza, naomba yenu makini,
Kuna jambo natangaza, kwenu nasema usoni,
Kwa siku lajiongeza, lakuwa uhayawani,
Wanawake wana haki, wasidhulumiwe kamwe.
Mwasema eti hasira, zachochea hayo yote,
Sasa ona ni hasara, zatupata sisi wote ,
Hofu wanayo hadhira, dhuruma maisha yote,
Wanawake wana haki, wasidhulumiwe kamwe.
Juzi ‘likuwa Wanjiku, uovu akafanyiwa,
Sitaki kuweka shuku, kifo kilikusudiwa,
Watazamwa kama kuku, dhuruma ikidaiwa,
Wanawake wana haki, wasidhulumiwe kamwe.
Wanawake wana haki, si vita kila uchao,
Tusiwalete hamaki, pia wao wana zao,
Tusiwafanye fariki, na tunataka mazao,
Wanawake wana haki, wasidhulumiwe kamwe.
Kalamu yalia wino, naomba mimi kusita,
Tuishi kwa upendano, ili tutoe matata,
Tulete ushikamano, tusuluhishe kuteta,
Wanawake wana haki, wasidhurumiwe kamwe.
SAMUEL MUNGAI
MALENGA MHENGA
CHUO KIKUU CHA MURANG’A
Heshima
Watoto nawausia, ya muhimu kusikia,
Yale nitawaambia, yanaweza kukufaa,
Na heshima ukijua, kwa maisha utapaa,
Ukiwa nayo heshima, mbali nayo utafika.
Heshima nayo maana, popote ukitembea,
Na Mungu anakuona, ni vizuri kusikia,
Hivyo basi ni maana, heshima kuzingatia,
Ukiwa nayo heshima, mbali nayo utafika.
Ukiwa hata shuleni, heshimu wako mwalimu,
Utapenya maishani, uwe mtu wa muhimu,
Nawasaha sikizeni, usije kujilaumu,
Ukiwa nayo heshima, mbali nayo utafika.
Kumbuka pia nyumbani, kuzingatia heshima,
Heshimu baba nyumbani, mkumbuke pia mama,
Nawaambia jamani, usiweze kulalama,
Ukiwa nayo heshima, mbali nayo utafika.
Ni ujumbe nimesema, kwa watoto wasikie,
Wasikie yale mema, heshima wazingatie,
Nimefika kaditama, ujumbe uwafikie,
Ukiwa nayo heshima, mbali nayo utafika.
MALENGA KITONGOJINI,
LIONEL ASENA VIDONYI
TONGAREN, NDALU
Naiokoa semia!
Naomba mnisamehe, nisowaitika simu,
Si ati nipo sherehe, eti nimezima simu,
Siwezi enda sherehe, wa mtihani msimu,
Naiokoa semia, hilo nomba muelewe.
Baba nawe mama yangu, nomba msiwe na hofu,
Nipo tu chumbani mwangu, semia yanipa hofu,
Mkononi simu yangu, nafungua pidihefu,
Naiokoa semia, hilo nomba muelewe!
Sitaki nije kufeli, nina magumu masomo,
Ndio maana silali, siishiriki migomo,
Taniruzuku Jalali, nijapo fika kikomo,
Naiokoa semia, hilo nomba muelewe.
Msinitumie jumbe, sina muda wa kujibu,
Nimejua nyie kumbe, ndinyi mnaniharibu,
Na macho niyafumbue, nisiwaone karibu ,
Naiokoa semia, hilo nomba muelewe!
Nijapo tua mzigo, natia dua kwa Mola,
Mambo siwe mbagombago, niiitimishe makala,
Sherehe zipa kisogo, nisijegeuka fala,
Naiokoa semia, hilo nomba muelewe!
JAPHETH NZOMO
ZAO LA HEKIMA
CHAKIMUT
Sigara
Namaliza mshahara, tena unanipa shida,
Namaliza mshahara, kuzilipa zako ada,
Namaliza mshahara, ninatoa ushuhuda,
Sigara wewe sigara, I wapi yako faida?
Unanipea madhara, mwilini kikuhifafadhi,
Unanipea madhara, yakunifisha maradhi ,
Unazidisha madhara, yakunishushia hadhi,
Sigara wewe sigara, niipi yako faida?
Nikuvutapo sigara, unanipa kikohozi,
Nikuvutapo sigara, yani dobera maozi,
Nikuvutapo sigara, ninatukana wazazi,
Sigara wewe sigara, niipi Sasa faida?
Nikuvutapo sigara, ninawaza ubakaji,
Nikuvutapo sigara, ninakuwa mkabaji,
Nikuvutapo sigara, nafanya nisotaraji,
Sigara wewe sigara, niipi yako faida?
Umenifanya fukara, mavazi ni matambara,
Umenifanya fukara, nadra Mimi kung’ara,
Umenifanya fukara, kila kitu ni hasara,
Sigara wewe sigara, niipi yako faida?
Nenda ongea sigara, pamoya rafiki zako,
Nenda ongea sigara, Bangi hadi na tobako,
Nenda ongea sigara, wambe na gura mliko,
sigara wewe sigara, Lau hauna faida !
Nakutaliki sigara, kwa kuwa huna msada ,
Nakutaliki sigara, nakana zako Ibada ,
Nakutaliki sigara, Tena sitakupa muda,
Sigara wewe sigara, Lau hauna faida!
SAM MTSUFA
MALENGA MCHANGA
MALINDI
Naisifu Longa Longa
La ngomani likigonga,tu tayari kusikiza,
Kiswahili tunabonga, Taifani twatukuza,
Nyie kwetu ni wahenga kila neno mnaguz,a
Kongoleni Longalonga, Kiswahili kutujuza.
Kwenye lugha nyi bwenyenye, mwatukosha runingani,
Mgusapo ndipo penye, twaipenda burudani,
Hamfanyi kenyekenye, mambo yeni si utani,
Kongoleni Longalonga,Kiswahili kutujuza.
Kwenu upo ufanisi, Kiswahili kukitunza,
Bila shaka tunahisi, lugha yetu taikuza,
Siwashike ibilisi, mkaanza kupuuza,
Kongoleni Longalonga, Kiswahili kutujuza.
Munene nipe nikupe, yatutoa bumbuwazi,
Nawe Nuhu situtupe, shairini tenda kazi,
Tawaganda kama kupe, nyie chai si andazi,
Kongoleni Longalonga, Kiswahili kutujuza.
Kikomoni natuia, na uchafu ninakoga,
Samiati mechambua, kwetu sisi kuwa mboga,
Nyoyo zetu twafungua, twasema bila yoga,
Kongoleni Longalonga, Kiswahili kutujuza.
CHARLES WAMBUA
TAVETA