• Nairobi
  • Last Updated April 25th, 2024 12:26 PM
SOKOMOKO: Heshimu mama wa kambo

SOKOMOKO: Heshimu mama wa kambo

Heshimu mama wa kambo

ACHA niseme ukweli, tusiwe wa kuhukumu,

Alowaumba Jalali, na siyo kuwahukumu,

Wakikosa nasaili, wapatie ufahamu,

Siyo wote ni wabaya, hawa kina mama kambo.

 

Kunao wenye heshima, popote hutenda mema,

Wafaa kuitwa mama, kama wapo na uzima,

Ila mambo ya tuhuma, hayafai ninasema,

Jama tusiwachukie, siyo wote ni wabaya.

 

Vijana kidomodomo, kumbuka mlikotoka,

Ndo mfungue mdomo, mkaanze kupayuka,

Tieni kweli kikomo, muwaheshimu hakika,

Mama wa kambo ni mama, na siyo wote wabaya.

 

Kama wewe msumbufu, marekebisho kubali,

Usiwe na kinywa chafu, kinachotema makali,

Kuwa mwana mtiifu, kujituma na mkweli,

Wengine wetu viburi, ndipo tunawachukia.

 

Vijana tuzindukeni, hadi tujitathmini,

Moyoni hadi bongoni, penye shida tujuweni,

Tujibaidi na zani, sisi kweli maishani,

Tusitafute laana, kutoka kwa mama kambo.

HOSEA NAMACHANJA

‘Chozi la Kunguni’

Bungoma

 

Makasisi wabakaji

Moyoni nahuzunika, hakika naungulika,

Hapa nimeghadhabika, mtima umeraruka,

‘Kasisi nimewachoka, madai yakisikika,

Makasisi wabakaji, komeni mumepotoka.

 

Watoto ni malaika, mbona munawanajisi,

Mimba munawapachika, pia kuavya vijusi,

Hamuwezi kwaminika, sasa mwaleta utesi,

Makasisi wabakaji, komeni mumepotoka.

 

Maradhi mwawambukiza, kisonono na virusi,

Dunia mwaleta giza, huruma na hamuhisi,

Maovu ndiyo mwaweza, subiri kwa Mola kesi,

Makasisi wabakaji, komeni mumepotoka.

 

Kanisa mwanyenyekea, moyoni munalo fundo,

Pepo mumempokea, matendo yenu uvundo,

Brandi nawakemea, tokomea kwa kishindo,

Makasisi wabakaji, komeni mumepotoka.

BRANDI MSANII

‘Tabasamu la Mnato’

Kakamega

 

Sipendi

Sipendi kuuandika, utungo usio mwema,

Wajuzi wakanicheka, kila wanapousoma,

Kisha nikatamauka, na kutunga nikakoma,

Sipendi kweli nasema, sipendi hivyo hakika.

 

Sipendi kuyatamka, maneno yaso heshima,

Wenzangu wakashtuka, halafu wakaachama,

Wakamba nimepotoka, na wote wakanihama,

Sipendi kweli nasema, sipendi hivyo hakika.

 

Sipendi kudhalilika, pale ninapojituma,

Au jasho kunitoka, bila chochote kuchuma,

Nikawa nasononeka, na kuatuka mtima,

Sipendi kweli nasema, sipendi hivyo hakika.

 

Sipendi kutopendeka, na wana au wazima,

Wakawa wanitoroka, kwao ninaposimama,

Kila baya likituka, nikazibeba lawama,

Sipendi kweli nasema, sipendi hivyo hakika.

 

Sipendi kulazimika, kuzikubali shutuma,

Uchao nikaungulika, na midomo kujiuma,

Yaani nikateseka, bila lolote kusema,

Sipendi kweli nasema, sipendi hivyo hakika,

MARTHA GACERI

‘Sheeri Gee’

Shule ya Ontulili, Meru

 

Natunga mpenzi

Natunga sio matani, matamu ufurahie,

Natunga siwe afkani, utamu unitambie,

Natunga zakowe nduni, penzi hino nilindie,

Natunga ewe hirimu, swahibu nayekuenzi.

 

Natunga sio matani, matamu ufurahie,

Natunga nideke nani, kama siwe wangu mie,

Natunga tia saini, kiapo tujivishie,

Natunga ewe mwandani, wazazi wataafiki.

 

Natunga sio matani, matamu ufurahie,

Natunga nudhumu hani, kwa wino kunakilie,

Natunga penzi kipini, joyoni ishikilie,

Njoo wangu we mwandani, mpenzi anikoshaye.

GLADYS KIRISWO

‘Toto Shombe’

Eldma Ravine

 

Nakupenda Kiswahili

Nipe fursa nieleze, yaliyo ndani moyoni,

Yasikiye uyameze, yatokapo mdomoni,

Umenifanya nicheze, kwa furaha mtimani,

‘Menisafirisha mbali, nakupenda Kiswahili.

 

Kwa kuzingatia ngeli, nimepata kusafiri,

Kiingereza kwa kweli, nimejua tafsiri,

Nimejipatia mali, kwa kutunga ushairi,

‘Menisafirisha mbali, nakupenda Kiswahili.

 

Umenipa nyingi ‘taji, nikajivika kichwani,

Nikatambua kipaji, ambacho kilifichwani,

Umekuwa kama maji, kutoa kiu juani,

‘Menisafirisha mbali, nakupenda Kiswahili.

FAITH WAIRIMU WERU

‘Mchele wa Chenga’

Chuo Kikuu cha Moi

 

Kilimilimi silete

Kimachomacho nasema, kimasomaso sikiza,

Kimenomeno watema, kindumbwedumbwe hujaza,

Kindakindaki simama, kimbelembele maliza,

Kimuyemuye silete, kilimilimi sikiya.

 

Kimoyomoyo nasema, kilimbilimbi kishike,

Kilimilimi kupima, kinyangarika kiteke,

Kikweukweu kutuma, kwao Kilifi kiweke,

Kimuyemuye silete, kilimilimi sikiya.

 

Kitambakwiri sikiza, kizaazaa uache,

Kizingatine kukaza, kizuizui ufiche,

Kizunguzungu punguza, kutangatanga uache,

Kimuyemuye silete, kilimilimi sikiya.

 

Kingalingali silale, kifyonza-vumbi tumia,

Kigelegele letile, Kimakunduchi sikia,

Kisarawanda ni kile, kimakusudi natia,

Kimuyemuye silete, kilimilimi sikiya.

 

Kitendawili natoa, kisalisali epuka,

Kihadharishi tongoa, kindingapopo pulik ,

Kimbaumbau ondoa, wajibu wako hakika,

Kimuyemuye silete, kilimilimi sikiya.

KEN TREVOR DEMWAMBIA

‘Kitongojini Mutuati’

 

Nipangue Maulana

Jitokeze niridhike, ja Paulo nitulie,

Ili moyo ufunguke, niwe wako uishie,

Unijaze nijazike, pomoni unifikie,

Nipangue Maulana, tufungamane milele.

 

Heri niwe chombo chako, niizidishe thamani,

Sije tena hamaniko, nikose tena amani,

Yatoke mahangaiko, nizame pako guuni,

Nipangue Maulana, tufungamane milele.

 

Nisiwe kimbelembele, nisijekosa neema,

Nipangue siwe vile, nivyokosa usalama,

Hakika popote pale, udumu nami daima,

Nipangue Maulana, tufungamane milele.

 

Sitaki kukukosea, dhambi zangu keshakiri,

Wala baya kutokea, kutukosesha tayari,

Heri weye ondolea, tabia za kikafiri,

Nipangue Maulana, tufungamane milele.

TONEY FRANCIS ONDELO

‘Malenga Mjali Siha’

Ndhiwa, Homa Bay

 

Nifanye nini akome?

Zao hili Simbaume, lanizolea mafuu,

Naomba leo niseme, moyo upate nafuu,

Swali kwenu nilitume, twambizane kama nduu,

Huyu mwizi nanukuu, nifanye nini akome?

 

Nalikesha gumegume, shambani kibahauu,

Nikisubiri achume, miraa sio tambuu,

Nimrukie kwa sime, nimkomeshe bunguu,

Huyu mwizi nanukuu, nifanye nini akome?

 

Jibu hili mlitume, linitoke hili buu,

Nimpe sumu akome, au chambo jungu kuu,

Kilishika hili dume, hadi kwa chifu mkuu,

Huyu mwizi nanukuu, nifanye nini akome?

 

Beti nne nituame, hapo nalikata guu,

Swala hili mlipime, mnijuze maafuu,

Washairi mlitume, usipite mwaka huu,

Huyu mwizi nanukuu, nifanye nini akome?

MAINAH ALFRED MAINAH

‘Msanifu Makamula’

Mia Moja, Timau

 

Malipo yapo

Mwandani njoo upesi, matongo weze kutoa,

Usije fanya uasi, maadili kipotea,

Njema utuige sisi, mazuri yakakujia,

Tenda utendayo sana, kijua malipo yapo.

 

Nawe mwana tusikie, wazaziwe twayajua,

Njia mbovu sipitie, masaibu yamejaa,

Yetu mema yasikie, angaa usije lia,

Tenda utendayo sana, kijua malipo yapo.

 

Mke acha za kaumu, wamejaza za uongo,

Watakuweka lawamu, kikujaza na matongo,

Ikupotee hamumu, umwache bila ya bongo,

Tenda utendayo sana, kijua malipo yapo.

PETER WANJOHI

‘Kitunguu Machoni’

Thika

 

Sina pupa

Ya Rabi kutoka kapa, mjawo ninaogopa,

Kazi nitakazo chapa, waja wasije zikopa,

Kisha zisikome hapa, zifike hadi Yuropa.

Nilisema sina pupa, Mungu yupo atanipa,

 

Iwe nyama ama fupa, kidumu au jipipa,

Neno hili sitatupa, hini dhima nimejipa.

Enda yangu nyapanyapa, taratibu ninadupa,

Nazidi kuchapa lapa, Mola usije nitupa,

 

Kiapo leo naapa, mpaka sitauchupa.

Tamati kunao papa, Rabi siwezi wakwepa,

Kwa hivi wanavyotapa, dagaa sitanenepa,

Mola naomba wachapa, ili wapate nihepa.

DOTO RANGIMOTO

‘Jini Kinyonga’

Morogoro

 

Yatima fakiri

Mtoto wa masikini, huwa sawa na yatima,

Hawanacho duniyani, cha kuita chao chema,

Dhiki huwapiga honi, siyo mbele siyo nyuma,

Maisha ya uyatima, mkombozi ni Jalia.

 

Taabu hukunyeshea, mwilini kukaukia,

Na ngozi kukulowea, uwele kukupatia,

Na mizongo kuzongea, ya mawazo dabalia,

Maisha ya uyatima, mkombozi ni Jalia.

 

Makonde ya matatizo, panchi kwako hutulia,

Pasipo mazungumzo, maumivu kufikia,

Mizoroto mzomzo, ya kiafya hukwachia,

Maisha ya uyatima, mkombozi ni Jalia.

RAMADHAN ABDALLAH SAVONGE

‘Malenga wa Nchi Kavu’

 

Bado sijafika

Vina ninaokoteza, kutunga huu mshororo,

Najaribu kueleza, katika lugha nyororo,

Bado mi najikoleza, kwa wa jana huu uporo,

Mie bado sijafika, ila kwanza najaribu.

 

Sijawa bado malenga, sinivishe cha ukoka,

Mie bado ni mchanga, ndio kwanza naibuka,

Nishajitoa mhanga,ushairi kuandika,

Mie bado sijafika, ila kwanza najaribu.

 

Kama tu kuku mgeni, ndio kwanza nazoea,

Najua kwenye hii fani, wapo waliobobea,

Nami pia natamani, nikaweze kupepea,

Mie bado sijafika, ila kwanza najaribu.

 

Ushairi nayo ni fani, isokuwa na mchezo,

Lazima jua mizani, vipande na kibwagizo,

Pia uweze kughani, ujue vingi vigezo,

Mie bado sijafika, ila kwanza najaribu

AYIEKO JAKOYO

‘Malenga wa Bara’

Mumias

You can share this post!

Matusi ya pasta Ng’ang’a yashtua Wakenya

Burundi kukatiza uhusiano wake na Umoja wa Mataifa

adminleo