Mashairi

SOKOMOKO: Tenda wema

June 8th, 2019 Kusoma ni dakika: 4

WAJA ukiwatendeya, wema waishi vicheko,

Daima utapokeya, fanaka kila wendako,

Kwa kuwa wetu Jaliya, aona mchango wako,

Tenda wema wende zako, Mola atakujaliya.

 

Wema ukizingatiya, mfano utoke kwako,

Kila ulodhamiriya, tenda pasi nung’uniko,

Pasipo kutarajiya, malipo kwa wenzi wako,

Tenda wema wende zako, Mola atakujaliya.

 

Pindi wakikutendeya, yalo nazo nufaiko,

Kushukuru sikawiya, na kuonyesha ridhiko,

Ila kuwa wangojeya, sio bora hili shiko,

Tenda wema wende zako, Mola atakujaliya.

 

Tamati naelekeya, mwishilio wa tamko,

Ni heri kuzingatiya, haya kila tuendako,

Watu ukiwatendeya, yafaayo nufaiko,

Tenda wema wende zako, Mola atakujaliya.

MAINAH ALFRED MAINAH

‘Msanifu Makamula’

Mia Moja, Timau

 

Penzi sumu ya bafe

Penzi nitia baridi, halina umaarufu,

Namithilisha waridi, husoza nzuri harufu,

Kisha kunyauka hadi, kuwa nayo udhaifu,

Kadhani penzi sherehe, yakini Sumu ya bafe.

 

Penzi ni upinzani, yamejaa mashindano,

Wapenzi wamo vitani, silaha za mapambano,

Kisima cha shukurani, hutekwa majibizano,

Kadhani penzi sherehe, yakini Sumu ya bafe.

 

Penzi hulipia kodi, hisia za sasa matani,

Waganga wana miradi, ya kuyaleta makini,

Ye humeza hana budi, dawa zenye ushetani,

Kadhani penzi sherehe, yakini Sumu ya bafe.

 

Penzi huunda vikao, yenye jina tangatanga,

Mkeo hana makao,ni mapenzi kusimanga,

Hawabanduki nawao,waume safari Tanga,

Kadhani penzi sherehe, yakini Sumu ya bafe.

 

Mapenzi pia ureda, yataka upodo tu,

Usitie jitihada, kwa kumpiga kitutu,

Kaditama jipe muda, penzi sikutie kutu,

Kadhani penzi sherehe, yakini Sumu ya bafe.

GLADYS KIRISWO

‘Toto shombe’

Eldama Ravine

 

Buriana John Gift

Kifo hakina adabu, kimejawa na kiburi,

Hata hakina aibu, nakuli mburumatari,

Kimetutia ghadhabu, hatujihisi vizuri,

Kaketu John Gift, lala pema penye wema.

 

Ukweli tuseme nini, machozi yanatutoka,

Hututoki mawazoni, kaka tumekasirika,

Mapema hii jamani, kijana umeondoka,

Kaketu John Gift, lala pema penye wema.

 

Vinywa vimetukauka, fahamu tumeduwaa,

Wenzako tumeshtuka, kwa kuiaga dunia,

Umeenda kwa Rabuka, bila sisi kutwambia,

Kaketu John Gift, lala pema penye wema.

 

Nani atatuchekesha, kaka tunakuuliza,

Sasa tunahuzunisha, umetuacha kwa giza,

Bingwa wa kuburudisha, mwenzetu tutakupeza,

Kaketu John Gift, lala pema penye wema.

 

Ulikuwa mwenye chudi, sikulini na nyumbani,

Kwa kumwimbia Wadudi, uliimba si utani,

Nyimbo zako maridadi, ziliongoa jamani,

Kaketu John Gift, lala pema penye wema.

HOSEA NAMACHANJA

‘Chozi la Kunguni’

Tongaren, Bungoma

 

Aanzapo hayahaya

Nawajia wana wangu, niwanasihi yakini,

Metia machoni pangu, kuhusu mkalia ‘ni,

Naomba wa tumbo langu, hili mlifikirini,

Aanzapo hayahaya, tumia guu kupona.

 

Tumia guu kupona, sikufike ya mauti,

Kwani mlivyopendana, uyageuka maiti,

Hutajua sanasana, yafikapo kwa umati,

Aanzapo hayahaya, piga mbio himahima.

 

Piga mbio himahima, kwani mengi yanukia,

Usije kuhemahema, kwa yanayokuvizia,

Dalili kwambie wima, za mawingu ni mvua,

Aanzapo hayahaya, mwana situlie hapo.

 

Usije tulia hapo, tukupate ewe mfu,

Usiuwe yaanzapo, ‘la kimbilia ‘tukufu,

Au ujifanye popo, anazo sifa sufufu,

Aanzapo hayahaya, nakuomba upotee.

WANJOHI PETER

‘Kitunguu Machoni’

Nanyuki

 

Penzi lianzapo

Lisikieni na hili, langu lenyewe tuhuma,

Lauma tena vikali, moyoni pasi huruma,

Kulidadisi ni ghali, nalo laleta lawama,

Penzi lianzapo, lajawa heri pomoni.

 

Penzi lianzapo, lakoroga na kuroga,

Latesa pote ulipo, laweza kukuvuruga,

Chochote baya liwapo, walitowa pasi woga,

Penzi lianzapo, lajawa heri pomoni.

 

Utakacho utapewa, rejareja au ghali,

Sikuzo tatembelewa, hutobaki tena dhuli,

Liwalo tadekezwa, kwa majina mbalimbali,

Penzi lianzapo, lajawa heri pomoni.

 

Penzini mwanzoni, tavalia mtakavyo,

Taandamana sokoni, mkishikana vilivyo,

Mema yote tatamani, kuahidi menginevyo,

Penzi lianzapo, lajawa heri pomoni.

 

Maongezi maridhawa, kwa arafa kiujuzi,

Kwa hakika utalewa, na ukose usingizi,

Penzilo utapewa, kwa vifijo umaizi,

Penzi lianzapo, lajawa heri pomoni.

TONEY FRANCIS ONDELO

‘Malenga Mjali Siha’

Ndhiwa, Homa Bay

 

Mtoto ni yule wako

Mtoto hasai wako, ulomzaa mwenyewe,

Asiye wa ndugu yako, huyo usitegemee,

Awe hasa damu yako, uliyemzaa wewe,

Mtoto ni yule wako, ulomzaa mwenyewe.

 

Hata awe na vituko, ikiwa ni wako wewe,

Moja siku jua iko, yaja umtegemee,

Lakini wa ndugu yako, si wako hilo ujue,

Mtoto ni yule wako, uliyezaa mwenyewe.

 

Mtoto wa ndugu yako, siye wako ulijue,

Huyo ni wa ndugu yako, nawe wako jizalie,

Asikupe hangaiko, natabu ujizuzue,

Mtoto ni yule wako, ulimzaa mwenyewe.

 

Nimeshaona vituko, sababu nielezee,

Na mengi mahangaiko, wa ndugu apendezewe,

Mwisho kanipa sumbuko, sababu nielezee,

Mtoto ni yule wako, uliyezaa mwenyewe.

SIWAJUMBE AMADI

Ngamiani, Tanga Tanzania

 

Wakataa ya wakuu!

Mkataa ya wakuu, huvunja yake maguu,

Ni kweli msemo huu, utayaona makuu,

Wamevunjika maguu, watoto wa wajukuu,

Wakataa ya wakuu, utavunjika maguu.

 

Wameyaona makuu, wazee na wakuu,

Nawaonya vitukuu, enyi wetu wajukuu,

Wasikizeni wakuu, msivunjike miguu,

Mkataa ya wakuu, huvunjika maguu.

 

Wanadharau mkuu, anayejua ya kale,

Wewe bado mjukuu, bado hujaona mbele,

Hujayaona makuu, waliyoona wavyele,

Mkataa ya wakuu, atavunjika miguu.

 

Wanakuonyesha mbele, nayo sasa vilevile,

Fuata yao wavyele, uishi vyema milele,

Waliyaona ya kale, ndiposa wakuambile,

Mkataa ya wakuu, Atavunjika maguu.

JUSTIN GUNGACHEA

Mariakani

 

Yamerudi malumbano

Faida ya malumbano, kulumbana gazetini,

Hupata yalo manono, kukufaa akilini,

Yahadithiwa vigano, na misemo ya zamani,

Yamerudiwa malumbano, ya watungugaji mabingwa.

 

Kunayo mengi mavuno, ya watunzi wa zamani,

Kina Shamte mfano, mtunzi mwenye thamani,

Mimi humpenda mno, kwa yake mengi makini,

Yamerudiwa malumbano, ya watungugaji mabingwa.

 

Tuwaombea malenga, zamani waliotunga,

Waliojua kunga, mashairi kuyapanga,

Mola uwape muanga, na peponi kuwapanga,

Yamerudiwa malumbano, ya watungugaji mabingwa.

 

Malumbano tusayapenda, twaburudi wasikilizaji,

Fikira njema twaunda, ambazo zatufariji,

Na mili yetu yawanda, huku kuliko vijiji,

Yamerudiwa malumbano, ya watungugaji mabingwa.

 

Tutoe mema mifano, kuridhisha mashabiki,

Hatutaki malumbano, yenye matusi n chuki,

Tuwe na majibizano, tupendeze halaiki,

Yamerudiwa malumbano, ya watungugaji mabingwa.

MOHAMED YUSUF

Kisauni, Mombasa

 

Natamani kulia

Nimejazwa na uchungu, ninatamani kulia,

Moyoni mengi machungu, natamani kujiua,

Nawauliza wenzangu, lipi mtaniambia,

Rohoni nina machungu, ninatamani kulia.

 

Naogopa bwana Mungu, si vizuri kujiua,

Kwa sababu ya machungu, humu katika dunia,

Vitabu vyote vya Mungu, vyakataza kujiua,

Rohoni nina machungu, ninatamani kulia.

 

Najiona peke yangu, imenizoea dunia,

Wote marafiki zangu, ambao nategemea,

Hata na watoto wangu, wote wamenikimbia,

Rohoni nina machungu, ninatamani kulia.

 

Sijui ubaya wangu, sababu kunikimbia,

Kuniacha peke yangu, uzee umeningia,

Nakuomba bwanan Mungu, wewe kunisaidia,

Rohoni nina machungu, ninatamani kulia.

KUZUSHI MAMBO SUDI

Taita-Taveta

 

Kuziepuka ajali

Hatari barabarani, zimezidi pikipiki,

Ukienda kila mahali, chunga sana pikipiki,

Zasababisha ajali, njiani hakupitiki,

Kwa kuepuka ajali, ziogope pikipiki.

 

Vilema wengi mijini, sababu ni pikipiki,

Si mchana sijioni, zimeleta sana dhiki,

Kwa mimi sizitamani, siipandi pikipiki,

Kwa kuepuka ajali, ziogope pikipiki.

 

Hakuna cha afadhali, ukipanda pikipiki,

Mvu uishia mwilini, ujuu ya pikipiki,

Hata kwenye jua kali, mwili wako pikipiki,

Kwa kuepuka ajali, ziogope pikipiki.

 

Unapopata ajali, uko juu pikipiki,

Utaujua kwelii, faida ya pikipiki,

Mwilio ndilo jabali, unalipanda pikipiki,

Kwa kuepuka ajali, ziogope pikipiki.

CHARO KAZUNGU DENA

Kaloleni