SOKOMOKO: Wasichana wala hela
WASICHANA ni wazuri, ukikuwa nazo pesa,
Shababi muwe tayari, kwepuka hii mikasa,
Mnatupandisha mori, hamuoni ni makosa,
Tumechoka nazo simu, kila wakati ni hela.
Wasichana mumezidi, wanaume walalama,
Mwavunja hata ahadi, wanabaki kuwasema,
Haja yenu si akidi, moyoni mnatuchoma,
Tumechoka nazo simu, kila wakati ni hela.
Wasichana fikiria, wavulana wajipanga,
Fulusi mwaangalia, mwafikiri ndio mwanga,
Akina dada tulia, maisha ni kujipanga,
Tumechoka nazo simu, kila wakati ni hela.
Wasichana fahamuni, tabia ni ya maana,
Msianguke shimoni, hela ni kama laana,
Mkiweka fikirani, mtajipata mwasona,
Tumechoka nazo simu, kila wakati ni hela.
LIONEL ASENA
‘Malenga Kitongojini’
Seeds High School, Kitale
Uyatima sikuita
Salamu kwenu natuma, wenza wangu viokote,
Niweleze wimawima, nifute machozi yote,
ini laniumauma, yao sumu ni ya mate,
Uyatima sikuita, mbona yanipate haya?
Nilijipata kilema, tano ya kwangu miaka,
Sikuyaelewa jama, kiguu kujafanyika,
Kumbe! Amu nayatema, likata sije rithika,
Uyatima sikuita, mbona yanipate haya?
Mali ya baba na mama, kwa ulafi ‘lichukua,
Nami kuniandama, cha kwangu kukitegua,
Kitwana kachwa waama, pasi haki zingatia,
Uyatima sikuita, mbona yanipate haya?
Ukongo wewe natema, weye nakulaumu,
Saratani siko wima, wazazi sasa hatamu,
Nalia ila hatima, ni kuitika ya sumu,
Uyatima sikuita, mbona yanipate haya?
WANJOHI PETER
Kitunguu Machoni
Mlima Kenya, Nanyuki
Saa yako jogoo
Jogoo ninalo swali, ambalo lanitatiza,
Jogoo ulikabili, jibu lake kunijiza,
Jogoo wawika hali, wakati wafatiliza,
Jogoo sasa nambia, saa waificha wapi?
Jogoo kuitafuta, saa yako nilianza,
Jogoo sikuipata, naona ni miujiza,
Jogoo imi najuta, visa vyako vyashangaza,
Jogoo sasa nambia, saa waificha wapi?
Jogoo kukuchunguwa, manyoyani nalianza,
Jogoo sikuelewa, nikuchinje nikawaza,
Jogoo sijang’amuwa, navyozidi kuchunguza,
Jogoo sasa nambia, saa waificha wapi?
Jogoo natamatisha, njia ninaifuliza,
Jogoo inaniwasha, hii yako miujiza,
Jogoo haya yatosha, nakuomba unijuza,
Jogoo sasa nambia, saa waificha wapi?
MAINAH ALFRED MAINAH
‘Msanifu Makamula’
Mia Moja, Timau
Sitaoa
Bismillahi Karima, ninaanza yangu ngoma,
Niridhike kwa mtima, niondokwe na lawama,
Waziwazi nayasema, na peupe nayatema,
Afadhali waniseme, natangaza sitaoa.
Kuoana na sitaki, ninajua watasema,
Ninanena kwa hamaki, bila hata kulalama,
Ukitaka nishtaki, uniache na alama,
Afadhali waniseme, natangaza sitaoa.
Zangu lulu nimetema, ninataka kuondoka,
Bila hata kutetema, hawa binti sitotaka,
Nnataka aushi njema, niishi mingi miaka,
Afadhali waniseme, natangaza sitaoa.
Napuliza mpulike, ili neno msikie,
Silisemi kwa makeke, huko kwenu mlitie,
Mkitaka mnicheke, ama nyimbo muimbie,
Afadhali waniseme, natangaza sitaoa.
KEN TREVOR DEMWAMBIA
‘Mtoto wa Kitongojini’
Mwanao si kitoweo
Akili yake mnyama, mwanadamu memwingia,
Atendayo siyo mema, ukiona unalia,
Ninenayo si tuhuma, yafanyika nawambia,
Baba mtafuna mwana, si timamu ni wazimu.
Ana mke ameoa, watoto amekopoa,
Sura zinamzingua, hadi awageukia,
Kwa mwanawe nakataa, na kusuta nawambia,
Baba mtafuna mwana, si timamu ni wazimu.
Kina baba nisikie, mijini na vijijini,
Jambo hili mtambue, wanenu waheshimuni,
Wake zenu watumie, bali si wana jamani,
Baba mtafuna mwana, si timamu ni wazimu,
Unaanzaje jamani, bintiyo kumdandia?
Ni wehu siyo utani, sifurahii Hosea,
Mwanao kumwita hani, au bebi nashangaa,
Baba mtafuna mwana, si timamu ni wazimu.
HOSEA NAMACHANJA
Chozi la Kunguni
Bungoma
Nimwitaje?
Nimezamia wazoni, kisogo kucha mekuna,
Nimejikuna jamani, nikifikiri ya mana,
Yanokosesha amani, jinale lilo dhamana,
Nachotaka ni jina, nimruzuku Kahari.
Nataka jina nambeni, asoweza kukana,
Litoke kwenu wandani, pole pasi kung’ang’ana,
Taratibu liwazeni, siwe lile la laana.
Nachotaka ni jina, nimruzuku Kahari.
Liwe bora duniani, yeyote siwe meona,
Jina lile la thamani, kuliko lake Yohana,
Lisiwe hata mbinguni, liwe lake tenatena,
Nachotaka ni jina, nimruzuku kahari.
Jinalo nalitamani, kama lile la Hosana,
La kushindana vitani, nayo mawele ya zina,’
La kututoa wafuni, tuzidishe kufaana,
Nachotaka ni jina, nimruzuku kahari.
TONEY FRANCIS ONDELO
‘Malenga Mjali Siha’
Ndhiwa, Homa Bay
Heko kigogo
Natamani tukutane, nikupe uso kwa jicho,
Mambo kadha tukanene, nikwambiye nitakacho,
Nipe myadi tupatane, nitakupa upendacho,
Wamitila nakuhara, michangoyo ni adhimu.
Kazi nyingi zilochanya, za kukuza kiswahili,
Ni bidii ulofanya, utafiti kusahili,
Jina lako limepenya, heko wazistahili,
Wamitila nialike, nije kwako unifunze.
Kwa fasihi umetamba, kila mtu akujua,
Wapwani na wakamba, huko kote umetua,
Hata kwazo simutamba, kisakura tanijia,
Wamitila ndiwe gwiji, koja mie nakuvisha.
Nakutaja kwa sauti, wasojua wakujue,
Wenye vyepeo sharti, wakikwona wavivue,
Mazuge wendamatiti, kijaliwa wazingue,
Wamitila nitungaye, jina langu ni Barasa.
AGGREY BARASA
‘Bongopevu’
MMUST Kakamega
Wengu haiwi ini
Mama sasa kaburini, kiwa hoi mewaacha,
Mamakambo usukani, sasa malezi kuchacha,
Upendo si samahani, dharau kilakukicha,
Ni wengu haiwi ini, taratibu sikizeni.
Mkewe kakutoroka, kwa tabia sokomoko,
Kamleta wafanaka, kisura mwenye upako,
Kumbe njia huziruka, hufiyonza vile viko,
Ni wengu haiwi ini, taratibu sikizeni.
Mafanikio ajira, sehemu za mashinani,
Kainakili shajara, Mjomba madarakani,
Kukadiria hasara, kwa kukosa umakini,
Ni wengu haiwi ini, taratibu sikizeni.
Wakati kakupa tunda, tunu kawa nyingi Mali,
Mwishowe kuvisha sanda, majonzi halisi hali,
Waliorithi matunda, kauza bila kujali,
Ni wengu haiwi ini, taratibu sikizeni.
GLADYS KIRISWO
‘Toto Shombe’
Eldma Ravine
Mwalimu nakushukuru
Ugani ninaingia, mwalimu kumsifia,
Mema alonitendea, naomba kusimulia,
Tangu pale chekechea, yote nitaangazia,
Mwalimu ninashukuru, mema ulonitendea.
Kalamu kushikilia, tabu ilinipatia,
Wazo lilinipitia, nyumbani kutorokea,
Mwalimu ulinijia, moyo ukanipatia,
Mwalimu ninashukuru, mema ulonitendea.
Nasaha ulinipea, nami nikapokea,
Nimekuwa abiria, aliyepata afua,
Ninatimiza rajua, nasaha kushikilia,
Mwalimu ninashukuru, mema ulonitendea.
Nidhamu ulinitia, nisije nikapotea,
Ingawa nilichukia, sasa ninajivunia,
Popote ninatembea, watu wanisifia,
Mwalimu ninashukuru, mema ulonitendea.
FADHILI FARJALA
‘Samaki wa Jangwani’
Chuo Kikuu cha KeMU
Maisha
Twaishi haya maisha, ila yote yanaisha,
Uhai wa mtu hwisha, chuma huliwa huisha,
Yana mitihani tosha, kwa mabega hukuchosha,
Naisha leo naisha, uliko nawe takwisha?
Mwenzenu yamenichosha, yitwayo haya maisha,
Mitihani inabisha, ngo! ngo! ikitisha,
Milango na madirisha, mitihani kafungisha,
Naishi leo naisha, uliko nawe takwisha?
Taabu jama zachosha, niliko nasema tosha,
Kila leo nachemsha, dhiki zanibingirisha,
Katoboka la maisha, gurudumu la maisha,
Naisha haya maisha, uliko nawe takwisha?
Dhiki wa kuamurisha, kwangu kuziondosha,
Ningampa vya kutosha, hadi vikamuemesha,
Mradi aniondosha, kwa haya gumu maisha,
Naishi leo naisha, uliko nawe takwisha?
RAMADHAN ABDALLAH SAVONGE
‘Malenga Wa Nchi Kavu’
Tenda wema
Naja tena mzalendo, ni imara ja jabali,
Niisute mienendo, ile isiyo halali,
Niweleze mi Omwando, yanyoke yalo muhali,
Nahimiza tenda wema, dunia hii mapito.
Kwa viongozi fisadi, nawaeleza bayana,
Acha wenu uhasidi, huo sio uungwana,
Zenu dhuluma mezidi, mwajipalia laana,
Nahimiza tenda wema, dunia hii mapito.
Polisi nanyi sikia, kurunzi nawamulika,
Mnaposhika doria, sitishe ongo hakika,
Acheni hiyo tabia, wananchi wahangaika,
Narudia tenda wema, dunia hii mapito.
Majaji mahakamani, hasa wale wenye hila,
Mwaleta purukushani, mbona hamna fadhila?
Na kesi mwarundikani, na maovu kutawala,
Narudia tenda wema, dunia hii mapito.
EZEKIEL OMWANDO MOGAKA
‘Mkuki wa Bara’
Kenya Muslim Academy, Nairobi