Habari za Kaunti

Maswali yaibuka Gavana Mwadime ‘Wakujaa’ akisalia kimya baada ya waziri wake kutimuliwa

April 3rd, 2024 2 min read

NA LUCY MKANYIKA

KIMYA cha Gavana Andrew Mwadime wiki moja baada ya kuondolewa kwa Waziri wa Ardhi na bunge la Kaunti ya Taita Taveta, Bi Elizabeth Mkongo, kimeanza kuibua maswali.

Wiki iliyopita, bunge hilo lilipitisha hoja ya kumng’atua waziri huyo kutokana na tuhuma za utovu wa nidhamu na kushindwa na majukumu yake ya kikazi.

Waziri huyo alikuwa miongoni mwa watu waliokuwa na jukumu kubwa la kumpigia debe gavana wakati wa kampeni za uchaguzi wa 2022, na hivyo kuondolewa kwake kunaonekana kama pigo kwa gavana.

Hata hivyo, Gavana Mwadime ameepuka kujibu tuhuma dhidi ya Bi Mkongo wala kuchukua hatua yoyote.

Katika mahojiano na wanahabari yaliyofanyika mjini Taveta hivi majuzi, Bw Mwadime aliomba tu subira wakati wafanyakazi wake wanapotekeleza ajenda yake.

“Baraza langu la mawaziri linafanya kazi chini ya mikataba thabiti ya utendaji. Mikataba hii inalenga kuhakikisha ufanisi, uwazi, na utoaji wa huduma,” alisema.

“Nina imani kamili na wafanyakazi wangu kwani wana ujuzi na uzoefu na wamejitolea kutumikia watu wa Taita Taveta. Nawasihi kuwapa muda na nafasi ya kufanya kazi yao. Sitasita kufanya mabadiliko ikiwa watashindwa kutekeleza majukumu yao,” akaongeza.

Baadhi ya wanaharakati wa masuala ya ardhi wamejitokeza kumtetea Bi Mkongo huku wakimtaka gavana awalinde mawaziri wake anapoamini hawana kosa.

Walidai masaibu yake yalichochewa kisiasa na kuwa tuhuma dhidi yake hazina ushahidi wa kutosha.

Akiongea mjini Voi, Bw Chombo Shete, mwanaharakati, alisema Bi Mkongo amepiga hatua katika usimamizi wa ardhi na juhudi zake za kuboresha taratibu za masuala ya ardhi.

“Tunajua kinachoendelea na hatuwezi kuruhusu michango yake kudhalilishwa,” alisema.

Kwa upande wake, mwanaharakati wa masuala ya bajeti katika kaunti hiyo, Bi Isabella Kidede, alisema idara ya ardhi imekuwa ikikabiliwa na ukosefu wa fedha za maendeleo.

“Kila wakati fedha za idara hii huchukuliwa na kuwekwa kwa zingine. Kwa hivyo, ni wapi waziri angepata fedha za kuendesha miradi yake,” alisema.

Alisema ni wakati wakazi wa kaunti hiyo kukuza viongozi na kuepukana na kuwadhalilisha viongozi hasa wanawake wachapakazi.

Bw Paul Oling’a, mwanaharakati wa shirika la kutetea ardhi la Clan alimtaka gavana kuvunja kimya na kuwatetea mawaziri wake ili wapewe nafasi ya kufanya kazi.

Wakati wa kupitishwa kwa hoja ya kumtimua Bi Mkongo, Naibu Spika Anselm Mwadime alielezea kusikitishwa na mtazamo wa maafisa wa kaunti kuhusu masuala nyeti ya ardhi na kuonya kuwa madiwani wataendelea kushinikiza uwajibikaji kutoka kwa serikali ya Gavana Mwadime.

Vilevile, alimshauri gavana kumpa waziri huyo nafasi mbadala ili aendelee kutumikia serikali hiyo.