Habari za Kitaifa

Mbunge Farah afurushwa hotelini kufuatia kauli zake za kudhuru Gen Z waliondamana

Na ANTHONY KTIIMO July 13th, 2024 1 min read

MBUNGE wa Daadab, Farah Maalim anaendelea kuonja hasira za Wakenya baada ya kufurushwa kutoka hoteli moja ya kifahari mjini Mombasa alikokuwa akiishi kufuatia matamshi anayohusishwa nayo kwamba angedhuru vijana walioandamana kupinga serikali.

Usimamizi wa hoteli ya Sarova White Sands, ulichukua hatua ya kumtimua mbunge huyo baada ya Wakenya kulalamika kuwa ilimpa hifadhi huku akilaumiwa kwa matamshi yake ambayo yameibua hisia kali kutoka kwa wadau mbali mbali.

Hoteli ya Sarova White Sands ilisema iliamua kumfurusha mbunge huyo ikihofia kuwa vijana wenye ghadhabu wangeivamia. Vijana hao walikuwa wameanza kuandaa kampeni ya “Occupy Sarova Whitesands”, ambako mbunge huyo alikuwa akiishi kwa muda.

Katika ujumbe kwenye mtandao wa X, Mkurugenzi msimamizi wa kundi la hoteli za Sarova Bw Jimi Kariuki alithibitisha kuwa ilimlazimu mbunge huyo kuondoka kwenye hoteli hiyo kwa kuwa kampuni hiyo haingetaka kujihusisha na mtu wa aina hiyo.

“Kwa sasa yeye sio mmoja wa wageni wetu. Tulimuomba aondoke. Hatuungi matamshi ya chuki aliyoyatoa kwa Wakenya na hatutaki kuhusisha biashara na mwonekano wetu na mtu wa aina hiyo,” akasema Bw Kariuki.

Kabla ya Hoteli ya Sarova White Sands kutoa thibitisho, vijana mitandaoni walikuwa wametishia kufika hotelini humo ambako Mbunge huyo alikuwa.

“Nauliza Sarova Whitesands, nikiuliza kwa niaba ya Wakenya wengine wengi, mbona mnamhifadhi mtu ambaye alieleza wazi kuwa angewaua watu 5,000 ambao walikuwa wakiandamana kwa amani?” akauliza Ice Queen kupitia X.

Gazeti la Taifa Leo lilijaribu kumfikia mbunge huyo kwa maoni yake lakini hakujibu simu wala kujibu jumbe alizotumiwa.

Wakenya walimkashifu Bw Maalim baada ya video yake kusambaa mitandaoni wakiitaka Tume ya Kitaifa ya Uwiano na utangamano kumchukulia hatua.

Video hiyo ilichipuka punde tu baada ya maandamano ya Gen Z, ambapo mbunge huyo alikuwa akizungumza kwa lugha ya Kisomali akieleza jinsi angechukua hatua za kikatili dhidi ya waandamanaji.

Alijitetea akisema kuwa video hiyo ilikuwa imekarabatiwa kwa sababu ambazo hakuzielewa.