Habari za Kitaifa

Mgomo: Inyangala awataka wahadhiri wafike katika meza ya mazungumzo

Na GEORGE MUNENE September 20th, 2024 1 min read

KATIBU wa Idara ya Elimu ya Juu Beatrice Inyangala, ametoa wito kwa wahadhiri na wafanyakazi wengine wa vyuo vikuu kurejea kwenye meza ya mazungumzo ili kusuluhisha mvutano unaoendelea kati yao na serikali.

Akiongea Ijumaa katika Chuo Kikuu cha Embu wakati wa sherehe ya tisa ya kufuzu, Dkt Inyangala alisisitiza kuwa mazungumzo ndio njia ya pekee ya kusuluhisha mgomo huo unaoathiri masomo ya wanafunzi.

Aliwataka wafanyakazi wote wa vyuo vikuu vya umma kuweka kando maslahi yao ya kibinafsi na kuweka mbele maslahi ya wanafunzi katika mvutano huu.

Dkt Inyangala alisema serikali imepiga hatua katika mazungumzo kati yake na Chama cha Kutetea Maslahi ya Wahadhiri (UASU) na kile cha kutetea maslahi ya wafanyakazi wengine wa vyuo hivyo (KUSU).

“Makubaliano yamefikiwa kuhusiana na masuala kadhaa, yakiwemo nyongeza ya mishahara ya kima cha asilimia saba, umri wa kustaafu, kuanzishwa kwa mkopo nafuu wa kununua magari na kubuniwa kwa Kamati ya Kitaifa ya Utelekezaji wa mkataba mpya wa makubaliano (CBA) uliotiwa saini.

Kauli ya Katibu huyo ilijiri wakati ambapo sekta ya Elimu ya Juu nchini inakabiliwa na changamoto kubwa hasa uhaba wa fedha uliochangia migomo.

Dkt Inyangala alikariri kujitolea kwa serikali kuimarisha mishahara na mazingira ya utendakazi ya wafanyakazi wa vyuo vikuu, wakati huu ambapo uchumi wa nchi unakabiliwa na changamoto mbalimbali.

Hata hivyo, Dkt Inyangala aliwakumbusha wahadhiri na wafanyakazi wa vyuo vikuu kuwa serikali itakabiliwa na wakati mgumu kufadhili matakwa yao yote kwa wakati mmoja.

Alisema huku serikali ikitimiza matakwa hayo itafanya hivyo ikizingatia kwamba sharti wanafunzi waendelee na masomo bila kutatizwa.