• Nairobi
  • Last Updated April 28th, 2024 7:47 PM
2019: Kenya ilisalia kwenye ‘meza ya wazee’ tena Riadha za Dunia  

2019: Kenya ilisalia kwenye ‘meza ya wazee’ tena Riadha za Dunia  

Na GEOFFREY ANENE

KWA mara ya pili mfululizo, Kenya ilidhihirisha ubabe kwenye riadha ilipomaliza katika nafasi ya pili kutoka orodha ya mataifa 206 katika Riadha za Dunia 2019 zilizofanyika jijini Doha, Qatar.

Mabingwa wa Riadha za Dunia mwaka 2015 Kenya walizoa jumla ya Sh46.3 milioni katika makala ya mwaka 2019 kupitia wanamedali wake 11.

Timothy Cheruiyot (mita 1,500), Conseslus Kipruto, Beatrice Chepkoech (mita 3,000 kuruka viunzi na maji kila mmoja), Hellen Obiri (mita 5,000) na Ruth Chepng’etich (marathon) walishinda medali za dhahabu, Faith Chepng’etich (mita 1,500) na Margaret Chelimo (mita 5,000) wakanyakua nishani za fedha nao Ferguson Rotich (mita 800), Rhonex Kipruto (mita 10,000), Amos Kipruto (marathon) na Agnes Jebet (mita 10, 000) wakazoa medali ya shaba. 

Emmanuel Korir (mita 800), Ronald Kwemoi (mita 1,500), Jacob Krop, Nicholas Kimeli (mita 5,000), Rodgers Kwemoi (mita 10,000), Benjamin Kigen, Abraham Kibiwott (mita 3,000 kuruka viunzi na maji), Eunice Sum (mita 800), Winny Chebet (mita 1,500), Lilian Kasait (mita 5,000), Rosemary Wanjiru, Hellen Obiri (mita 10,000), Edna Kiplagat (marathon) na Hyvin Kiyeng (mita 3,000 kuruka viunzi na maji) walizoa kati ya Sh1.5 milioni na Sh403, 000 kila mmoja kwa kumaliza vitengo vyao kati ya nafasi ya nne na nambari nane.  

Kenya ilianza kampeni yake vyema kwa kushinda mbio za kilomita 42 za wanawake kupitia kwa Ruth Chepng’etich.

Alikuwa mmoja wa watimkaji waliokuwa wamepigiwa upatu kutwaa taji baada ya kushinda Standard Chartered Dubai Marathon sekunde saba nje ya iliokuwa rekodi ya dunia ya saa 2:17:01 ya Mkenya mwenzake Mary Keitany.

Chepng’etich alistahimili joto kali jijini Doha akishindia Kenya dhahabu ya wanawake kwa mara ya kwanza tangu 2013. Malkia wa mwaka 2011 na 2013 Edna Kiplagat alimaliza kitengo hiki katika nafasi ya nne mwaka huu. 

Chepkoech pia alirejesha medali ya dhahabu ya mbio za mita 3,000 kuruka viunzi na maji ya kinadada, ambayo Kenya ilikuwa imeshinda mara ya mwisho mwaka 2015 kupitia Kiyeng. 

Kenya iliendeleza ubabe wake katika mbio za mita 3,000 kuruka viunzi na maji kwa upande wa wanaume kwa miaka 13 wakati bingwa wa Afrika, Jumuiya ya Madola, Dunia na Olimpiki Conseslus alinyakua taji. 

Wakenya wametawala kitengo hiki tangu mwaka 1991. Ni mwaka 2003 na 2005 pekee wakati Kenya ilipoteza taji la kitengo hiki liliponyakuliwa na mzawa wa Kenya, Saif Saaeed Shaheen kutoka Qatar. 

Obiri alihifadhi taji la mbio za mita 5,000 baada ya kuongoza Mkenya mwenzake Chelimo kufagia nafasi mbili za kwanza. Ilikuwa mara ya kwanza kabisa Kenya ilizoa dhahabu na fedha katika mbio hizo za mizunguko hiyo 12 na nusu tangu mwaka 2011. 

Naye Faith Chepng’etich alikubali kuachilia taji lake la mbio za mita 1,500 baada ya kumaliza katika nafasi ya pili nyuma ya Mholanzi Sifan Hassan. Timothy Cheruiyot naye alifuata nyayo za mshindi wa mwaka 2011, 2013 na 2015 Asbel Kiprop na Elijah Manangoi (2017) alipotawala kitengo cha wanaume cha mizunguko hiyo mitatu. 

Kwa mara ya pili mfululizo, Jebet aliridhika na medali ya shaba katika mbio za mita 10,000 za wanawake, huku Rhonex akipata nishani sawa na hiyo katika kitengo cha wanaume. Kenya haijashinda dhahabu ya wanaume katika kitengo hiki kwa miaka 16 sasa. 

Mwaka huu, Kenya ilipoteza taji la wanaume la marathon, ambalo Geoffrey Kirui alishinda mwaka 2017. Amos Kirui alikuwa Mkenya wa pekee kumaliza ndani ya mduara wa tatu-bora aliporidhika na nishani ya shaba naye Kirui akatupwa hadi nafasi ya 14. 

Mabingwa mara 13 Marekani wataandaa makala yajayo ya Riadha za Dunia mjini Eugene mwaka 2021. 

 

You can share this post!

KRISMASI: Serikali kulipa madeni ya wanakandarasi

KRISMASI: Watu 10 wakosa kuona siku muhimu

adminleo