Michezo

Tusker FC lengo kupiga hatua ligini ikialika Western Stima

April 3rd, 2019 Kusoma ni dakika: 2

Na CHRIS ADUNGO

VITA vya kuwania ufalme wa Ligi Kuu ya KPL vinatarajiwa kushika kasi hii leo Jumatano wakati Tusker ambao ni mabingwa mara 11 wa taji hilo watawaalika Western Stima mjini Machakos.

Chini ya kocha Robert Matano, Tusker watashuka dimbani wakipania kujinyanyua baada ya Chemelil Sugar kukizamisha chombo chao kwa kichapo cha 2-1 wikendi iliyopita.

Ushindi kwa Tusker utawapaisha hadi nafasi ya tano jedwalini kwa alama 29 sawa na Kariobangi Sharks ambao Alhamisi watakuwa wenyeji wa Zoo Kericho uwanjani Kenyatta, Machakos.

Kufikia sasa, Tusker wanashikilia nafasi ya tisa huku pengo la alama moja pekee likitamalaki kati yao na Stima.

Katika mchuano mwingine ambao matokeo yake yanatarajiwa kuathiri mpangilio wa vikosi vinavyowania fursa ya kutawala kilele cha jedwali, Bandari watawaalika Mount Kenya United jijini Mombasa.

Vijana wa mkufunzi Bernard Mwalala wanatarajiwa kuchuma nafuu kutokana na wingi wa mashabiki wao wa nyumbani na kutia kapuni alama tatu kirahisi.

Kufikia sasa, miamba hao wa soka kutoka Pwani ya Kenya wanashikilia nafasi ya nne kwa alama 33. Ushindi utawapaisha hadi nafasi ya pili jedwalini japo kwa muda.

Sofapaka ambao kwa sasa wanausoma mgongo wa Gor Mahia wanaoselelea kileleni, watakuwa wenyeji wa Vihiga United hapo kesho uwanjani Kenyatta na ushindi utawadumisha katika nafasi ya pili.

Masogora hao wa kocha John Baraza wamejizolea alama 36 kutokana na mechi 19 zilizopita. Gor Mahia ambao waliwachabanga Nzoia Sugar 2-1 mnamo Jumatatu, wanadhibiti usukani wa jedwali kwa alama 41 baada ya kutandaza jumla ya michuano 18.

Kakamega Homeboyz ambao kwa sasa wanafunga orodha ya saba-bora kwa alama 27, watawaalika Ulinzi Stars uwnajani Bukhungu.

Iwapo watawazidi maarifa wageni wao, Homeboyz watachupa hadi nafasi ya tano japo huenda wakapitwa tena na Sharks ambao wanapigiwa upatu wa kuwakomoa Zoo Kericho hapo kesho.

Ratiba ya KPL

Leo Jumatano:
Tusker na Western Stima (Machakos)
Bandari na Mt Kenya Utd (Mombasa)
KK Homeboyz na Ulinzi Stars (Kakamega)
KCB na Mathare United (Machakos)

Alhamisi:
Sharks na Zoo (Machakos)
Sofapaka na Vihiga Utd (Machakos)
Nzoia na Posta Rangers (Bungoma)
AFC Leopards na Chemelil (Machakos)