MACHO KWAO: Manchester City waanza safari ya kutetea taji la EPL dhidi ya West Ham
Na MASHIRIKA
LONDON, Uingereza
MANCHESTER City inatarajiwa kuanza kuonyesha meno yake makali mapema itakapoanza kampeni yake ya kutetea ubingwa wa Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) dhidi ya West Ham jijini London, leo Jumamosi.
Vijana wa kocha Pep Guardiola, ambao wanafukuzia taji lao la tatu mfululizo ligini msimu huu, wameshinda West Ham katika mechi tisa zilizopita zikiwemo saba kwenye ligi hii.
City huaibisha West Ham inapoalikwa London ikiwemo kuichapa kwa zaidi ya mabao matatu katika mechi tano zilizopita na mambo hayatarajiwi kuwa tofauti inapojiandaa kuanza kampeni zake vyema.
Mabwanyenye Manchester City walipepeta wenyeji wao West Ham mabao 5-0 katika Kombe la FA, 4-0 ligini na 3-0 katika mechi ya kirafiki mwaka 2017 na kuwalima ligini 4-1 na 4-0 mwaka 2018.
Mara ya mwisho klabu hizi zilikutana ni mwezi uliopita katika mechi ya kirafiki ambayo City ilitoka chini bao moja na kudhalilisha West Ham 4-1 kupitia mabao ya Sterling (mawili), David Silva na Lukas Nmecha aliyepachika penalti.
Mark Noble alitangulia kufungia West Ham kabla ya City kupata mabao manne.
David Silva na Raheem Sterling walichangia bao moja kila mmoja naye Leroy Sane akafunga mabao mawili wakati City ilipozuru uwanja wa nyumbani wa West Ham, Olympic jijini London mara ya mwisho mnamo Novemba 24 mwaka jana.
Takwimu hizi za ana kwa ana zinaonyesha kuwa City itaanza na asilimia kubwa ya kufanya vyema ugenini leo Jumamosi.
Baadhi ya wachezaji ambao City itategemea kutafuta alama tatu ni mvamizi matata Sterling, ambaye amekuwa akiimarika msimu baada ya mwingine tangu alipowasili kutoka Liverpool, mshambuliaji hatari Sergio Aguero, Kevin De Buryne na kipa Eder, ambaye amejitokeza kuwa mmoja wa makipa wazuri kwenye EPL.
Eder amechangia pakubwa katika kusambaza mipira vyema uwanjani na pia amedhibiti kisanduku chake. Guardiola atakosa huduma za Sane na Benjamin Mendy wanaouguza majeraha.
Mark Noble mkekani
West Ham ya kocha Manuel Pellegrini itakuwa bila mchezaji Mark Noble.
Yuko mkekani na jeraha.
Hata hivyo, Lukasz Fabianski anatarajiwa kurejea michumani baada ya kukosa mechi mbili zilizopita za kujipima nguvu. Sajili mpya Sebastien Haller ni mmoja wa wachezaji West Ham itaweka matumaini yake kwake.
Alifungia Eintracht Frankfurt mabao 15 msimu uliopita kabla ya kujiunga na West Ham, ambayo ilimaliza msimu uliopita katika nafasi ya 10.
Jumla ya mechi sita zitasakatwa leo. Tottenham, ambayo imeajiri Mkenya Victor Wanyama, itaalika washiriki wapya Aston Villa. Mchuano huu unatarajiwa kuwa mtihani mgumu kwa Villa ambayo inazuru Tottenham. Spurs inajivunia kushinda mechi za kufungua msimu 20 kati ya 21 dhidi ya washiriki wapya tangu msimu 2000-2001.
Vikosi vitarajiwa vya West Ham na Manchester City: West Ham – Fabianski; Fredericks, Diop, Balbuena, Cresswell; Rice; Antonio, Fornals, Lanzini, Anderson; Haller.
Manchester City – Ederson, Kyle Walker, John Stones, Aymeric Laporte, Oleksandr Zinchenko, Rodri, Kevin De Bruyne, David Silva, Bernardo Silva, Sergio Aguero, Raheem Sterling.