Michezo

Falling Waters yajiandalia fainali za Chapa Dimba

March 23rd, 2020 Kusoma ni dakika: 2

Na JOHN KIMWERE

KOCHA wa timu ya wasichana ya Falling Waters, Emman ‘Gullit’ Wambuchi anasema wanapania kujituma mithili ya mchwa kwenye fainali za kitaifa kupigania taji la Chapa Dimba na Safaricom Season Three.

Falling waters awali ikifahamika kama Barcelona Ladies kwa mara nyingine itawakilisha Mkoa wa Kati katika fainali za kipute hicho.

”Bila kupaka mafuta kwenye mgongo wa chupa ninaelewa bayana timu zote zimejipanga kushusha soka la kufa mtu,” alisema na kuongeza kuwa kikosi chake kimetosha mboga hasa kukabili upinzani wowote msimu huu.

Anasisitiza kuwa anaamini chipukizi wake wamekaa fiti kupiga shughuli zao kibiashara wala sio kwenda kulaza damu.

Hannah Namuya (kulia) wa Falling Waters akishindana na Damaris Akinyi wa Limuru Starlets katika fainali ya wasichana kuwania taji la Chapa Dimba na Safaricom Season Three 2019/2020 katika Mkoa wa Kati. Picha/ John Kimwere

NUSU FAINALI

Kwenye ngarambe ya kitaifa muhula uliyopita warembo hao walibanduliwa katika nusu fainali na Kitale Queens iliyoibuka malkia. Vigoli hao chini ya nahodha, Miriam Lutomia walibeba taji la eneo hilo walipoteremsha soka safi na kuchoma Limuru Starlets kwa magoli 3-1.

”Katika mpango mzima kawaida yangu nataka kukuza wasichana wengi tu waibuke kati ya wachezaji watakaopaisha soka la Kenya miaka ijayo,” kocha huyo alisema na kuongeza kuwa mechi za kipute hicho zimechangia wachezaji wengi kuanza kumakinika michezoni kinyume na misimu iliyopita.

HARAMBEE STARLETS

Kwenye fainali za muhula huu katika Mkoa wa Kati, wachezaji watatu walibahatika kubeba tuzo za kibinafsi. Kwa mara nyingine, Jane Njeri aliyetingia kikosi hicho mabao mengi msimu uliyopita aliibuka mfungaji bora alipotikisa wavu mara sita.

Jane Njeri wa Falling Waters akipokezwa tuzo ya kuibuka mfungaji bora kitengo cha wasichana katika fainali za Chapa Dimba na Safaricom Season Three 2019/2020 katika Mkoa wa Kati. Picha/ John Kimwere

Nao Eunice Alele na Miriam Lutomia walituzwa kama mnyakaji bora na mchezaji anayeimarika mtawalia.

Kadhalika ingawa ni Jane Njeri aliyeteuliwa katika kikosi cha mwisho kilichosafiriki nchini Uturuki kwa mashindano yaliyofanya mwaka huu pia Miriam Lutomia alikuwa katika kambi ya timu hiyo mpaka siku ya mwisho.

TANO ZIMEFUZU

Timu tano za wasichana tayari zimejikatia tiketi ya kushiriki fainali za kitaifa mwaka huu. Orodha hiyo inajumuisha:Wiyeta Girls (Bonde la Ufa), Falling Waters Mkoa wa Kati, Beijing Raiders (Mkoa wa Nairobi), Isiolo Starlets (Mkoa wa Mashariki) na Kwale Ladies malkia wa taji hilo katika Mkoa wa Mombasa.

Hata hivyo kama ilivyo kwa shughuli zingine nyingi tu kote nchini kufuatia mlipuko wa virusi vya korona, mechi za kipute hicho pia zimepigwa breki.

Mercy Tarus (kushoto) wa Itigo Girls akishndana na Metrine Nanjala wa Kitale Queens katika fainali za Chapa Dimba na Safaricom Season Two katika Mkoa wa Ritf Valley. Picha/ John Kimwere

Kabla ya kuzuka kwa maambukizi ya virusi hivyo, fainali za kitaifa zilikuwa zimepangwa kuchezwa mwezi Juni mjini Mombasa. Mabingwa wa kitaifa (wavulana na wasichana) kila moja hupokea zawadi ya Sh1 milioni.

Falling Waters imeundwa na wachezaji hawa: Eunice Alele na Elizabeth Ripilo (wanyakaji), Eunice Ariviza, Martha Nafula, Marion Analo, Wiita Nafula, Purity Wamuyu, Delness Nashipae na Christine Awuor (mabeki).

Miriam Lutomia, Hannah Namuya, Esther Wanjiru, Margaret Wangui na Alice Chepkorir (viungo). Safu ya washambuliaji inajumuisha: Jane Njeri, Pauline Achuchuka na Naomi Nanjala.