• Nairobi
  • Last Updated April 28th, 2024 12:38 PM
5 kutochezea Gor katika kipute cha nane-bora kimataifa

5 kutochezea Gor katika kipute cha nane-bora kimataifa

Na CHRIS ADUNGO

ANAPOSUBIRI kwa hamu kufanyika kwa droo ya robo-fainali za Kombe la Mashirikisho barani Afrika (CAF Confederations Cup) hii leo Jumatano nchini Misri, kocha Hassan Oktay wa Gor Mahia ni mwingi wa hofu.

Kinachomkosesha usingizi mkufunzi huyo mzawa wa Uturuki ni ulazima wa kuzikosa huduma za masogora watano katika mchuano utakaowakutanisha na miamba wengine wa soka ya Afrika katika hatua hiyo ya nane-bora.

Hofu nyingine ya Gor Mahia ni ulazima wa kukutanishwa ama na Berkane (Morocco), Sfaxien (Tunisia) au Al-Hilal (Sudan) ambao walitawala vilele vya makundi A, B na C mtawalia.

Zamalek ya Misri ambayo iliambulia nafasi ya kwanza katika Kundi D itapangwa katika zizi moja na ama Hassania Agadir (Morocco), Etoile du Sahel (Tunisia) au Nkana FC (Zambia).

Gor Mahia hawawezi kukutanishwa na Agadir, Etoile du Sahel au Nkana katika hatua hii ya nane-bora. Mechi za mkondo wa kwanza za robo-fainali hizi zitatandazwa mnamo Aprili 7 huku marudiano yakifanyika Aprili 14.

K’Ogalo waliingia katika mabuku ya historia ya kabumbu ya humu nchini mwishoni mwa wiki jana baada ya kuwachabanga Petro Atletico de Luanda ya Angola 1-0 na kuweka hai matumaini ya kunyanyua ubingwa wa CAF muhula huu.

Ni mara ya kwanza kwa Gor Mahia kutinga hatua hiyo katika kampeni za kipute hicho licha ya kusalia na wachezaji tisa pekee ugani MISC Kasarani.

Marufuku itakayowaweka nje nyota Jacques Tuyisenge, Harun Shakava, Peter Odhiambo, Ernest Wendo na Shafik Batambuze inamuumiza kicha Oktay.

Tuyisenge ambaye alifunga bao la pekee na la ushindi dhidi ya Petro atakosa mchuano wa mkondo wa kwanza war obo-fainali sawa na Odhiambo na Shakava walioonyeshwa kadi za manjano wikendi iliyopita kwa mara nyingine.

Batambuze na Wendo kwa upande wao watakosa michuano yote ya mikondo miwili baada ya kuonyeshwa kadi nyekundu katika mchuano wa mwisho wa Kundi D dhidi ya Petro ambao walibanduliwa kwa pamoja na NA Hussein Dey kutoka Algeria.

Soko la uhamisho

Ili kumwezesha kukibadilisha kikosi mara kwa mara kwa nia ya kuweka hai matumaini ya kunyanyua mataji kadhaa muhimu msimu huu, Oktay amefichua azma ya kujishughulisha vilivyo katika soko la uhamisho wa wachezaji.

Miamba hao wa soka ya humu nchini wanapania kusajili wachezaji watatu zaidi ili kujaza nafasi za Humphrey Mieno, Ephrem Guikan na Innocent Wafula walioagana nao msimu huu.

“Gor kwa sasa wanahitaji mvamizi wa ziada, winga na kiungo mpakuaji atakayeshirikiana vilivyo na Francis Kahata katika ngome ya kikosi,” akatanguliza Oktay.

“Nitawasilisha maombi hayo kwa usimamizi. Iwapo hayataidhinishwa, basi itatulazimu kuwategemea wachezaji waliopo kwa sasa,” akaongeza.

Baada ya kupoteza 1-0 dhidi ya Hussein Dey nchini Algeria na kupepetwa 4-0 katika marudiano kati yao na Zamalek nchini Misri, Gor walikuwa katika ulazima wa kushinda Petro ili kusonga mbele.

Waliingia mchuano huo wa mwisho wa Kundi D wakivuta mkia kwa alama sita, mbili nyuma ya Zamalek na moja nyuma ya Petro na Hussein Dey.

You can share this post!

Mtihani mgumu kwa Ulinzi ikivaana na Tusker FC ligini

Niko radhi kuacha Chelsea lakini si sigara, adai Sarri

adminleo