ADUNGO: Hakika mtu yeyote anayetaka kushabikia Arsenal sharti awe na moyo wa chuma
Na CHRIS ADUNGO
KUKISHABIKIA kikosi cha Arsenal ni jambo linalohitaji mtu kuwa na moyo wenye ugumu wa chuma!
Katika kampeni za mapambano ya kuwania mataji mbalimbali ya soka msimu huu, nimejifunza kwamba sifa kuu inayotofautisha Arsenal na klabu nyinginezo za Uingereza na za bara Ulaya ni kutotabirika kabisa kwa matokeo ya kikosi hicho cha Arsene Wenger katika takriban kila mchuano.
Si bure, huenda huu utakuwa msimu mwingine, na wa pili mfululizo kwa Arsenal kumaliza kampeni za Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) nje ya mduara wa nne-bora na hivyo kukosa fursa ya kucheza soka ya Klabu Bingwa Ulaya (UEFA) msimu ujao.
Mbali na Chelsea ambao kwa sasa wanaelekea kukamilisha kampeni za Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) kwa matao ya juu, Arsenal ndicho kikosi cha pekee ambacho katika mechi moja kina uwezo wa kupiga soka safi ya kuvutia kisha siku chache baadaye ukashangaa sana kukiona kikicheza mpira usioeleweka wala kutamanika kabisa.
Yalikuwa matarajio ya kila shabiki kwa mfano, kwamba ushindi wa 2-1 uliosajiliwa na Arsenal dhidi ya Chelsea katika mchuano wa mkondo wa pili wa nusu-fainali ya League Cup mnamo Januari 24, 2018 ungaliwachochea zaidi kuzimakinikia mechi zao zilizofuatia.
Hata hivyo, kilichoshangaza na kustaajabisha mno ni kwamba Arsenal walikomolewa na Swansea City 3-1 uwanjani Liberty siku sita baadaye, na hivyo kupoteza alama muhimu sana ambazo vinginevyo zingewapa ufufuo na uthabiti wa kukabiliana vilivyo na ushindani mkali dhidi ya wapinzani wao wakuu katika mduara wa sita-bora ligini.
Pandashuka
Siku tatu baadaye, Arsenal waliweka hai matumaini ya mashabiki wao kwa mara nyingine walipojikusuru kuzitegemea huduma za sajili wapya Pierre-Emerick Aubameyang na Henrikh Mkhitaryan kuwadhalilisha Everton 5-1 katika mechi ya EPL iliyotandazwa ugani Emirates.
Lakini punde si punde, kiota hicho cha matumaini ya kutinga mduara wa nne-bora katika EPL msimu huu kilibomolewa ghafla na Tottenham Hotspur ugani Wembley mnamo Februari 10, 2018 licha ya Arsenal kuingia katika mchuano huo wakijivunia huduma za nyota wao wote.
Kwa shabiki yeyote, ushindi wa 2-1 na 5-1 dhidi ya Chelsea na Everton ni matokeo ambayo yalitosha kuwapa Arsenal asilimia 100 ya kuwakandamiza wapinzani wao katika mechi zilizofuata!
Lakini hali haikuwa hivyo. Ina maana kwamba, hata ushindi wa wiki jana wa 3-0 dhidi ya Ostersund katika Ligi ya Uropa, haustahili kabisa kutegemewa na mashabiki kuwapigia Arsenal upatu wa kuwazidi maarifa Manchester City kwenye fainali ya League Cup mnamo Februari 25, 2018.
Safu ya kati
Tatizo kubwa la Arsenal ni ukosefu wa uthabiti katika safu yao ya kati. Asikudanganye mtu, Arsenal inajivunia baadhi ya wachezaji wazuri sana katika takriban kila idara. Ubora ambao umeletwa na ushirikiano mpya kati ya Alexandre Lacazette, Mkhitaryan, Aubameyang na Mesut Ozil si wa kuchukuliwa vivi hivi na mpinzani yeyote!
Hata katika safu za kati na ulinzi, Arsenal si wabaya sana. Sead Kolasinac, Laurent Koscielny, Hector Bellerin, Nacho Monreal, Shkodran Mustafi na nahodha Per Mertesacker hujituma sana nyuma ya ukuta ghali wa Aaron Ramsey, Granit Xhaka, Jack Wilshere na Alex Iwobi katika mifumo ya 4-4-2, 3-4-2-1 au 4-2-3-1.
Ikiwa Arsenal wanapania kweli kurejesha ubora wao wa msimu wa 2003-04, basi itamjuzu Wenger kuwafunza wachezaji wake maana na umuhimu wa kudumisha uthabiti na kuacha kusajili matokeo yenye kukisawiri kikosi chake kama timu dhaifu.